ASKOFU ATOA MANENO 'MAKALI' MSIBA WA DK. MENGI MOSHI...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 9 May 2019

ASKOFU ATOA MANENO 'MAKALI' MSIBA WA DK. MENGI MOSHI...!

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT), Dk. Fredrick Shoo.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua katika kaburi la Marehemu Dk. Reginald Abraham Mengi mara baada ya kuzikwa katika makaburi ya familia, eneo la Mkuu, Kisereni Machame, mkoani Kilimanjaro leo.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kushoto) akitoa pole kwa wanafamilia wa Mzee Mengi kwenye ibada ya kumuombea iliyofanyika kanisa la KKKT Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT), Dk. Fredrick Shoo amewataka viongozi anuai kutumia kwa busara nafasi za uongozi na madaraka waliyopewa huku wakizingatia maslahi ya jamii zaidi kuliko binafsi.

Kiongozi huyo wa kiroho amesema viongozi wanaopewa nafasi hawapaswi kufanya ubaguzi wa kimakabila, kidini ama kuwabagua walio na uwezo au wasio nao kwani dhambi hiyo ni mbaya inaweza kuligawa taifa na kuleta mpasuko.

Askofu Dk. Shoo ameyasema hayo leo alipokuwa akiongoza ibada ya kumuombea aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi iliyofanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, KKKT Uasharika wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro kabla ya mazishi yaliyofanyika baadaye kijijini.

"...Viongozi tuliopewa madaraka tusiwabague wengine, tusiwe maskini wa kiroho na hata kufanya dhambi ya ubaguzi, ukiwa na cheo au nafasi itumie kuwasaidia wengine...hasa vijana mnaopewa madaraka tutumie kwa unyenyekevu kuwasaidia wengine...usijitutumue kama chatu, Mungu atakushusha," alisema Askofu Shoo akihubiri katika ibada hiyo.

Alisema Marehemu Dk. Mengi alikuwa mfano mzuri wa watu waliojaliwa kuwa na uwezo, lakini maishani mwake alijishusha, alisaidia kila mtu kwa kadri ya uwezo wake na hasa watu wenye ulemavu.

Aidha aliongeza kuwa mwanadamu hapaswi kumuhukumu mwenzake kana kwamba yeye ni msafi kuliko wote na kuwaomba wananchi kutumia maisha ya Dk. Mengi kama funzo kwa yale mazuri aliyotenda wakati wa uhai wake.

Akitoa salam za Serikali, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema marehemu Dk. Mengi atakumbukwa kwa mchango mkubwa alioutoa nchini kiuchumi na kijamii na pia kwa kundi la watu wenye ulemavu kwa kushirikiana na Serikali.

Alibainisha Serikali itaendelea mkumbuka marehemu kama mwasisi wa viwanda nchini na pia kampuni alizozianzisha zimetoa mchango mkubwa ndani na nje ya nchi kimaendeleo. Serikali itaendelea kuchangia na kuenzi shughuli alizokuwa akizifanya ikiwemo kushirikiana na taasisi ya kuwasaidia walemavu alioianzisha Dk. Mengi ( Dk. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation).

"...Tutaendelea kutoa ushirikiano kwa jambo lolote mtakalo tushirikisha (familia) na hata mkiitaji msaada wetu milango ipo wazi muda wote, nifuateni mimi, mawaziri na hata mkimtaka Rais (Dk. John Magufuli) nitawapeleka.

Akitoa salam za rambirambi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally alieleza kuwa watamkumbuka Dk. Mengi kama mzalengo aliyejenga taifa kimazingira, aliyetoa mchango mkubwa kuendeleza lugha ya taifa kupitia vyombo vyake vya habari.

Dk. Ally pia alitumia fursa hiyo kumuombea radhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhusiana na kauli yake aliyoitoa juzi akiwa jijini Dar es Salaam ambayo ilitafsiriwa vibaya juu ya kabila la wachaga.

Alisema kauli za utata zinazotolewa na viongozi vijana ni kuteleza kutokana na kukosa fursa za kuwaandaa vijana kuingia katika uongozi. "Kwa niaba yake naomba kumuombea msamaha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam...aliteleza tu kutoa kauli ile," alisema Dk. Ally.

Juzi akitoa salam za mkoa kwenye hafla ya kuuaga mwili wa Dk. Mengi jijini Dar es Salaam Makonda alisema ni vigumu kuona mchaga akitoa hela yake kusaidia watu wasiojiweza kauli ambayo ilitafsiriwa tata, inaweza leta ubaguzi. Hata hivyo alijitokeza na kuomba kwamba isitafsiriwe vibaya kwani alikuwa na nia njema.

Ibada hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali, taasisi anuai, wawakilishi mbalimbali, wananchi na viongozi wa kiroho na baadaye mashizi ya Dk. Mengi yaliyofanyika katika eneo la Mkuu, Kisereni-Machame.

 

No comments:

Post a Comment