IFAD KUENDELEA KUISAIDIA TANZANIA KUENDELEZA SEKTA YA KILIMO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 23 May 2019

IFAD KUENDELEA KUISAIDIA TANZANIA KUENDELEZA SEKTA YA KILIMO

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akimkabidhi  zawadi ya picha, Rais  wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Bw. Gilbert Fossoun Houngbo, baada ya Mkutano ulioangazia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini na namna ya kutatua changamoto zake, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akipeana mkono na mgeni wake Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Bw. Gilbert Fossoun Houngbo, katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.

Rais  wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Bw. Gilbert Fossoun Houngbo, akiipongeza Serikali ya Tanzania kwa ukuaji wa Sekta ya Kilimo kwa takribani asilimia 6, kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika, wakati wa Mkutano kati yake na  Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), kushoto ni Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. John Rubuga. 

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) na Ujumbe wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Bw. Gilbert Fossoun Houngbo (kulia), ukiwa katika mkutano ulioangazia Maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini na namna ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.

Na Peter Haule, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Gilbert Houngbo, na kuiomba Taasisi hiyo kusaidia kuendeleza zaidi Sekta ya Kilimo kupitia mpango wake mpya wa awamu ya  11 wa kuendeleza kilimo nchini.
Dkt. Mpango ameyataja baadhi ya maeneo ya kipaumbele kuwa ni uzalishaji wa mbegu bora, kusaidia kilimo cha umwagiliaji, kutafuta masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima, kusaidia upatikanaji wa mitaji kwa wakulima na kuanzisha taasisi za utafiti wa kilimo za kikanda.
Aidha, Dkt. Mpango alimwomba kiongozi huyo kusaidia pia mbinu za kupunguza upotevu wa mazao wakati na baada ya mavuno ili kuchochea na kuongeza tija katika sekta ya kilimo ambayo amesema inaajiri zaidi ya asilimia 66 ya Watanzania.
”Takiribani asilimia 66 ya watanzania wanategemea kilimo na kilimo ndio mwajiri mkuu hivyo kwa kuwa IFAD ina program mpya, tumeamua kushauriana ili wajue vipaumbele vya Serikali na fedha tutakazo zipata tuzielekeze katika maeneo hayo”, alieleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisema kuwa Serikali inaunda kikosi kazi kitakacho husisha Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ili kuweka nguvu ya pamoja kwa kuangalia maeneo ya vipaumbele ambavyo Mfuko wa IFAD utasaidia.
Kwa upande wake Rais wa IFAD Bw. Gilbert Houngbo, alisema kuwa Taasisi yake itashirikiana na Tanzania katika jitihada zake za kupunguza umasikini wa wananchi kupitia kilimo kwa kuyapatia ufumbuzi masuala kadhaa ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa mbolea na mbegu bora za kilimo na mifugo, masoko ya bidhaa, upatikanaji wa mitaji, kuongeza ujuzi wa wakulima, kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na kuwashawishi vijana wengi kujihusisha na kilimo.
Alielezea kufurahishwa kwake na mwamko pamoja na mwitikio wa baadhi ya wakulima na wafugaji walionufaika na awamu zilizotangulia za uendelezaji sekta ya kilimo na mifugo kupitia taasisi yake aliowatembelea, ambao amesema wanamtazamo mzuri wa kilimo cha kibiashara kinachozingatia uongezaji wa mnyororo wa thamani, suala ambalo ni moja ya lengo la Mfuko huo katika kuendeleza Sekta hiyo.
Mfuko wa IFAD ulianza kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi ya maendeleo ya kilimo kuanzia mwaka 1978, ambapo hadi sasa imesaidia miradi 15 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 385.80 na katika awamu mpya ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2019/2021, IFAD imetenga zaidi ya dola za Marekani milioni 58.8 kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.
Miongoni mwa miradi  hiyo ni pamoja na kuwasaidia wakulima kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo na mifumo ya masoko, kuhamasisha Sekta binafsi katika uwekezaji na kuwasaidia wakulima wadogo na wavuvi kuongeza kipato na kupunguza umasikini kwa kuzingatiakuongeza  mnyororo wa thamani ya mazao husika.
Sekta ya Kilimo nchini inachangia asilimia 30.1 ya jumla ya pato la ndani (GDP), asilimia 26 ya mapato ya kigeni, ajira takribani asilimia 65.5, inachangia malighafi za viwandani kwa takribani asilimia 65 na  inachangia kwenye mahitaji ya chakula kwa asilimia 100.

No comments:

Post a Comment