DK. MENGI 'ALINING'ATA' SIKIO, NIKAENDA NCHINI INDIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 7 May 2019

DK. MENGI 'ALINING'ATA' SIKIO, NIKAENDA NCHINI INDIA

Marehemu, Dk. Reginald Abraham Mengi.

ILIKUWA Siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa India na kuutangaza Utalii wa nchi hiyo katika Hoteli ya Serena ya jijini Dar es Salaam Mwaka 2004. Dk. Reginald Abraham Mengi (marehemu kwa sasa) alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yaliyowashirikisha raia wa India waishio nchini Tanzania pamoja na baadhi ya watu mashuhuri.

Ilikuwa kila anayeingia kwenye ukumbi alikuwa anaweka 'business card' yake kwenye chombo maalumu kilichoandaliwa kwa ajili ya baadaye kuchezeshwa bahati nasibu.

Marehemu Dk. Mengi alibaini kuwa baadhi ya wanahabari waliohudhuria kwenye maadhimisho hayo walikuwa wanakipita chombo hicho bila kuweka chochote, kwani walikuwa hawana 'business card' za kuweka katika chombo hicho.

Baada ya kubaini hivyo na kuona bahati nasibu hiyo tutaikosa, aliniita pembeni na 'kuning'ata sikio' yaani kuninong'oneza kuwa Mimi na Wanahabari wenzangu tuandike haraka majina na namba zetu kwenye karatasi tukaziweke kwenye chombo hicho.

Mimi na wenzangu tukafanya hivyo, lakini bila kujua kwamba yeye ndo atachezesha Bahati nasibu hiyo. Muda ulipowadia wa kuchezesha bahati nasibu,  kilichukuliwa chombo hicho na kukabidhiwa Mengi achezeshe.

Mengi aliingiza mkono na kuibuka na kikaratasi na kulisoma jina langu kuwa ndo mshindi namba moja, nilifurahi sana nikaitwa mbele na kupongezwa na viongozi walioketi meza kuu.

Akaingiza tena mkono kwenye chombo akatoka na business card safari hii mshindi alikuwa mhindi, waalikwa walishangilia sana tofauti na nilipotangazwa mimi, kitendo kilichoashiria waandaji hawakufurahishwa na ushindi Wangu.

Mengi aliingiza tena mkono kwenye chombo cha bahati nasibu akatoa kikaratasi chenye jina la Mwandishi wa Habari wa The Guardian, Juma Dihule aliyetangazwa mshindi wa Tatu, lakini naye hakushangiliwa.

Awali kabla ya kuchezesha draw hiyo,  MC wa hafla hiyo, alieleza kuwa watakaoshinda  watanufaika kwa kupata tiketi ya Ndege ya kwenda India na kurudi, malazi pamoja na kutembelea vivutio vya kitalii kwa muda wa wiki moja.

Cha ajabu siku ya pili yake tulipatiwa tu tiketi na kutueleza kuwa malazi tutajitegemea na ziara ya kutembelea vivutio vya Utalii vimefutwa.

Mwenzangu Juma Dihule aliamua kuuza tiketi, lakini mi niliamua kwenda kumueleza Mengi yote yaliyojiri, likiwemo la hata Mimi kutaka kuuza tiketi. Mengi alinijibu kuwa alijua hayo yatatokea kwani kitendo cha sisi black man kushinda kiliwaudhi sana.

"Usithubutu kuuza tiketi, lazima uende India ukasafishe macho, utajifunza mengi ya huko , usihofu mi nitakupa hela ya matumizi," aliniambia Mengi.

Muda huo huo akaingiza mkono kwenye koti na kunipatia dola 1000. Nilifurahi sana nikashukuru na kuagana naye. Alinitakia safari njema. Nilimshukuru sana kwa msaada wa huo ulioniwezesha nifike kwa mara ya kwanza katika Jiji la kibiashara la Mumbai, India. Ni kweli tembea uone nilijifunza mambo mengi.

Kwa Heri Dk. Mengi, Mungu ailaze roho yako milele mahali pema peponi, Amen.

No comments:

Post a Comment