WAHANDISI WANAWAKE WASISITIZA WASICHANA KUCHANGAMKIA SAYANSI, HISABATI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 3 April 2019

WAHANDISI WANAWAKE WASISITIZA WASICHANA KUCHANGAMKIA SAYANSI, HISABATI

Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara, Bi. Upendo Sanze, akielekeza jambo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya KwaMtoro wilayani Chemba mkoani Dodoma, kuhusu umuhimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwa Mtoro wilayani Chemba mkoani Dodoma, Bi. Neema Muna (mwenye miwani), akieleza changamoto zinazoikabili shule hiyo kwa Wahandisi wanawake kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara, walipofika shuleni hapo kuhamasisha umuhimu wa usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wasichana.

Mwanafunzi Siminza Mambo, kutoka Shule ya Sekondari ya KwaMtoro wilayani Chemba mkoani Dodoma, akitoa maoni kwa Wahandisi wanawake kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) walipofika shuleni hapo kuhamasisha usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wasichana.
Na Siti Said


WAHANDISI
wa kike wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kupitia Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara, wamewataka wanafunzi wa kike mkoani Dodoma, kuchangamkia fursa za usomaji wa masomo ya Sayansi  na Hisabati ili kuongeza wataalam katika fani ya Uhandisi.
Akizungumza kwa niaba ya wahandisi hao katika shule ya Sekondari ya KwaMtoro, Wilayani Chemba mkoani Dodoma, Mhandisi  Rahma Mwinyi , amesema kuwa  sekta hiyo bado ina uhaba wa wataalamu wa kike hivyo inahitaji wanafunzi kusoma masomo hayo ili kuongeza idadi ya wataalamu hao na kuweza kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025.
“ Hakikisheni mnasoma masomo ya Sayansi na Hisabati kwa bidii, ufaulu wa masomo haya utategemea  ufanyaji wa  maswali na mazoezi ya kujipima mara kwa mara ambayo yatawajengea uelewa na kupelekea kufaulu vizuri, Serikali bado inahitaji wataalam wa fani hii na pia fursa za ajira kupitia fani hii zipo nyingi, kazi kwenu kujipanga ili mfikie malengo yenu”, amesema Mhandisi Mwinyi.
Aidha, Mhandisi Mwinyi amewataka wanafunzi hao kuachana na dhana potofu ya kuwa masomo hayo ni magumu na badala yake kutafuta njia mbadala ikiwemo ya kupanga ratiba ya masomo  yao vizuri na kuzingatia yale wanayofundishwa na walimu darasani.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya KwaMtoro, Bi. Neema Muna, kwa niaba ya walimu wenzake ameishauri Serikali kuhakikisha wanapeleka vifaa vya maabara kwa shule ambazo hazina vifaa hususan vijijini kwani ufaulu wa masomo hayo hutegemea sana kufanya mazoezi kwa vitendo.
Ameongeza kuwa ipo haja ya Serikali kuajiri na kupeleka walimu wa kutosha katika shule zilizopo vijijini kulingana na idadi ya wanafunzi na pia huduma za maji na umeme ziboreshwe ili kukidhi mahitaji ya ufanyaji wa mazoezi kwa vitendo kupitia katika maabara zao.
Naye, Mwanafunzi Siminza Mambo wa shule hiyo, ameiomba Serikali kuongeza walimu wa kike wa sayansi shuleni hapo kwani kwa sasa shule hiyo ina mwalimu mmoja tu wa jinsia hiyo hali inayowakatisha tamaa wanafunzi wa kike kujiunga na masomo hayo.
Pia, Mwanafunzi Lucy Isack, kutoka shule hiyo ameiomba Serikali kuongeza walimu wa sayansi na hisabati, vitabu na kuboreshea miundombinu ya maabara ikiwemo vifaa vya kupimia kemikali.
Ziara ya wahandisi hao katika shule mbalimbali za Sekondari za mkoa wa Dodoma inalenga kuhamasisha usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wasichana ambapo leo wametembelea shule ya KwaMtoro, Dalai na Mondo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment