Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb). |
SERIKALI imesema kuwa imekusanya Sh. Milioni 3,010.5 kwa mwaka fedha 2016/17 na Sh. Milioni 2,545.6 kwa mwaka wa fedha 2017/18 za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika taulo za kike(sanitary pads) zilizozotengenezwa nchini na zilizoingizwa kutoka nje ya nchi.
Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Upendo Peneza (Chadema) aliyetaka kujua Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyokusanywa na Serikali katika mwaka wa fedha wa 2016/17 na 20017/18.
Dkt. Kijaji alisema kiasi hicho cha kodi kilikusanywa kabla ya kuondolewa kwa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)Juni, 2018.
Katika maswali ya nyongeza, yaliyoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Dkt. Immaculate Swale kwa niaba ya Mhe. Peneza, alisema pamoja na Serikali kuondoa baadhi ya kodi katika uzalishaji wa taulo za kike lakini bado bei ya bidhaa hiyo ipo juu, na kutaka kujua mkakati wa Serikali kushusha bei ya bidhaa hiyo ili kuhakikisha inawafikia walengwa.
“Kama Serikali imeshindwa kusimamia kushuka kwa bei, haioni kwamba iendeleze zile kodi za awali lakini kodi hii ikusanywe na iwe refinance ili kuweza kununulia hizi taulo za kike na izigawe bure mashuleni”, aliongeza Dkt. Swale.
Akijibu maswali hiyo, Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali haijashindwa kusimamia bei ya bidhaa hizo na kwa sasa inaendelea kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi ili kuona namna bora ya kuwafikia walengwa.
Alisema Serikali inaendelea kufanya tafiti mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuona namna ya kuwasaidia watoto wa kike ila kuna changamoto kodi inakusanywa ikiwekwa kwa ajili ya kununua na kugawa taulo za kike mashuleni.
“Yapo makundi mengine ambayo kodi zinazotozwa kwenye bidhaa zinazotumika na makundi hayo, tutatengeneza ombwe la kila kundi kuja kuomba kodi inayotozwa kwenye makundi hayo waweze kupewa wao”, alisema Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji alishauri kuwa kinachotakiwa kufanywa ni kubuni njia nyingine ili kuona watoto wa kike wanaweza kupata bidhaa hii bila kuhusisha kodi, au tozo zozote zinazotozwa katika bidhaa hii kwasababu imebainika kuwa inapoondolewa kodi wanaonufaika ni wazalishaji kwa kuwa taifa lipo katika soko huria.
Imetolewa na;
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
No comments:
Post a Comment