Mchoraji kutoka Tingatinga Arts, Agnes Mpate
akimuonesha picha ya kuchora Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Albert
Jonkergouw wakati wa Kongamano la wafanyabiashara Business Club Ilala
lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Albert Jonkergouw akiangalia moja ya bidhaa za Mkurugenzi wa Malaika Home essentials, Rachael Moyo wakati wa Kongamano la wafanyabiashara Business Club Ilala lililofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha biashara, Donatus Richard. |
NA MWANDISHI WETU
KATIKA kuwaongeza
uelewa, maarifa na elimu ya kujenga nidhamu ya fedha kwenye biashara zao, Benki
ya NMB imeahidi kuwapeleka China kwa masomo na warsha wafanyabiashara 10 kutoka
Klabu za Biashara za Benki hiyo ‘NMB Business Club,’ baadaye mwaka huu.
Ahadi hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha
Biashara wa NMB, Donatus Richard, wakati wa Kongamano la Wafanyabiashara Wadogo
na wa Kati (MSE), wanaounda Klabu za Biashara za NMB, lililofanyika kwenye
Ukumbi wa Kardinali Rugambwa, Oysterbay.
Richard alibainisha kuwa, lengo la ziara hiyo ya mafunzo ni
kuimarisha uelewa wa masuala ya fedha miongoni mwa wafanyabiashara wanaounda
klabu hizo, lengo likiwa ni kuwaongezea elimu ya kuhakikisha mtiririko wa fedha
kwenye biashara zao, unakuwa mnyoofu.
Akisisitiza ahadi hiyo, mbele ya wafanyabiashara zaidi ya 300
walioshiriki kongamano hilo, Richard alisema kuwa mchakato wa namna ya kuwapata
wateule wa ziara hiyo utatangazwa miongoni mwao,ili kwenda kupata fursa za
kimataifa, safari ikitarajiwa kufanywa Oktoba mwaka huu.
“Ushindani kibiashara nchini umekuwa mkubwa, nasi ndio maana
tunatumia klabu hizi kufundisha mifumo, njia na mipango rafiki ya kuimarisha
biashara za wateja wetu hawa ambao pia ni mabalozi wetu kwa jamii. Tutawapeleka
China kujiongezea maarifa juu ya hilo,” alisema Richard.
Awali akifungua kongamano hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
NMB, Albert Jonkergouw, alisema watayafanyia kazi mapendekezo yote
yatakayotolewa na wafanyabiashara wanaohudhuria makongamano yao kutoka klabu
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na punguzo la gharama za uendeshaji wa akaunti ya
biashara.
Jonkergouw alibainisha ya kwamba, Klabu za Wafanyabiashara ni
nzuri na muhimu sio tu kwa wanachama wake na Benki ya NMB, bali pia kwa ustawi
na ukuaji wa uchumi wa Taifa na kwamba wafanyabiashara hao ni kati ya mabalozi
wema wa benki hiyo.
“Kongamano hili ni kati ya fursa tunazozitumia kusikiliza
changamoto zenu, kujadiliana namna ya kuzitatua na mwisho wa mwezi kwenda
pamoja katika kasi ya uchumi wa mteja mmoja mmoja, benki kama taasisi na taifa
kwa ujumla wake,” alisisitiza Jonkergouw.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara waliohudhuria,
aliishukuru NMB kwa kuwakabidhi baadhi yao vyeti vya ubalozi mwema wa benki kwa
wafanyabiashara wa kupigiwa mfano, Award Mpandila, aliitaka Serikali kuwasaidia
ujenga mazingira rafiki ya kibiashara.
Mpandila alifafanua kwamba, moja ya changamoto zinazokwaza
biashara zao ni tozo zisizo wazi hususani bandarini, ambazo zinawakwamisha na
kusababisha kutorejesha mikopo yao kwa wakati, kutokana na kuchelewesha kwa
uondoshaji mizigo bandarini.
No comments:
Post a Comment