WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa tahadhari kwa wadau wote wa madini kuwa atakayekamatwa anatorosha madini, atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo utaifishaji wa madini atakayokuwa akiyatorosha.
Pia amewataka viongozi na watendaji wote wa Serikali wasimamie kwa weledi, uaminifu na uadilifu, sheria, kanuni na miongozo kuhusu sekta ya madini kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa madini hususan dhahabu kwenda nje ya nchi.
Waziri Mkuu ametoa tahadhari hiyo Machi 17, 2019 wakati akifungua soko la madini la Mkoa wa Geita. Ufunguzi wa soko hilo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli alilotoa tarehe 22.01.2019 la kuitaka mikoa yote ianzishe masoko ya madini.
Waziri Mkuu ameitakaWizara ya Madini, Tume ya Madini, Serikali ya Mkoa, Idara na Taasisi nyingine za Serikali zinazohusika na maendeleo ya sekta ya madini waheshimu mipaka ya majukumu yao ili waweze kulisimamia vizuri soko hilo na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
“Wizara ya Madini ishirikiane na vyama na mashirikisho ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuandaa mpango kazi mahsusi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya soko hili ili lisigeuke kuwa kikwazo kipya kwa wachimbaji na wafanyabishara wa madini”
Waziri Mkuu ameviagizaVyombo vya Ulinzi na Usalama vihakishe soko hilo linapata ulinzi wa kutosha muda wote ili watendaji, mali zitakazokuwemo, vitendea kazi na miundombinu yote iwe salama muda wote. “Mkuu wa mkoa na Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, nawaagiza hakikisheni Suala hili mnaliandalia utaratibu haraka iwezekanavyo”.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuielekeza mikoa mingine yenye kiwango kikubwa cha uzalishaji wa madini hususan ya metali na vito iharakishe uanzishwaji wa masoko ya madini sanjari na miundombinu yote muhimu ili masoko hayo yaanze kufanya kazi kabla ya kwisha kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019.
Amesema anaamini kwamba, usimamizi mzuri wa soko hilo na masoko mengine ya madini yanayoendelea kuanzishwa nchini utaimarisha makusanyo ya kodi za Serikali na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa.
Vilevile, amesema wafanyabiashara wa madini, hususan kutoka nje ya nchi wataongezeka kwa sababu tutakuwa tumewaepusha na matapeli na vikwazo vingine vya kibiashara. “Uimara wa soko hili pia, utaboresha uhusiano kati ya wadau wa biashara ya madini na Serikali”.
Waziri Mkuu amesema Serikali imefuta baadhi ya tozo na kodi ambazo zilikuwa kero kwa wafanyabiashara wa madini hususan wachimbaji wadogo. Miongoni mwa tozo zilizofutwa ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Zuio ya asilimia tano ya mwisho (final withholding tax) inayotozwa kwenye bei ya kuuzia madini ya aina zote.
Amesema baada ya kufutwa kwa kodi na tozo hizo Serikali inatarajia kuwa utoroshwaji wa madini utapungua, pia kutasaidia wachimbaji wadogo kutambuliwa kupitia uanzishwaji wa masoko ya madini; kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za wachimbaji wadogo na kuongeza wigo wa mapato kwa nchi.
“Nitoe wito kwa wachimbaji wote wadogo kwamba endeleeni kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali katika kutekeleza majukumu yenu kwa kufuata taratibu, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali”.
AmesemaSerikali inachukua hatua zote hizo si kwa lengo jingine bali kuziba mianya ambayo imekuwa chanzo cha utoroshwaji wa madini, ukwepaji kodi, na hivyo, kusababisha biashara nzima ya madini kufanyika kiholela katika maeneo mengi ya nchi yetu.
Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga vema katika kuhakikisha vikwazo vyote vilivyomo katika mnyororo wa biashara ya madini vinaondolewa kwa lengo la kukuza sekta hiyo na kuwanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.
Amesema Serikali imeamua kutoa mwelekeo mpya katika usimamizi na maendeleo ya sekta ya madini. “Utekelezaji wa dhamira hii unakwenda sambamba na kuweka mazingira mazuri na miundombinu itakayowezesha kuimarika kwa sekta ya madini nchini”.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema wachimbaji wadogo wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa masoko ya uhakika ya madini ambao umekuwa sababu ya utoroshwaji madini, hivyo kuanzishwa kwa soko hili kunawahakikishia wachimbaji wadogo masoko na kukua kwa kipato kutokana na shughuli za madini.
Waziri Mkuu amesema kwa muda mrefu sasa, kumekuwepo na malalamiko ya kudhulumiwa au kupunjwa kutoka kwa baadhi ya wachimbaji wadogo, vitendo hivyo vimekuwa vikiwahusisha wafanyabiashara wa madini wasiokuwa waaminifu.
“Ndugu wachimbaji wadogo, soko hili linakwenda kuwa mwarobaini wa tatizo hilo kwani litasheheni vifaa vya kupimia uzito na ubora wa madini kabla hayajauzwa. Naielekeza Tume ya Madini, isimamie ipasavyo vifaa na taratibu za vipimo kwenye soko hili na kuhakikisha hakuna manung’uniko juu ya utendaji kazi wa vifaa hivyo”.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa soko hilo pia litaondoa uwezekano wa wanunuzi wa madini kuibiwa na wajanja wachache wanaojifanya kuwa na madini wakati hawana. “Nawasihi wanunuzi wa madini kulitumia soko hili kikamilifu ili kuepuka udanganyifu na matapeli”.
Pia ameiagiza Tume ya Madini kuratibu bei za madini ndani ya soko hilo na ihakikishe mchimbaji anapata stahiki zake, Serikali inapata mapato yake na mfanyabiashara naye ananufaika. “Tunaimani kabisa tatizo la kudhulumiana na kupunjana linaenda kwisha kabisa. Na kwa kweli ikitokea mtu amepunjwa, atakuwa amejitakia mwenyewe”.
“Ndani ya soko hili kutakuwa na huduma zote muhimu kwa mfanyabiashara ikiwemo huduma za Tume ya Madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mabenki na nyinginezo, hivyo kuokoa muda na gharama nyingine katika kuendesha biashara hii ya madini.
Amesema soko hilo litasaidia sana katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali na takwimu za biashara ya madini. Hivyo, niwasihi wachimbaji wa madini kulitumia soko hili na kuacha vitendo vya utoroshaji wa madini. Serikali kwa upande wake, haitomvumilia mtu yeyote yule atakaye jihusisha na utoroshaji wa madini.
Ufunguzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Wabunge wa mkoa wa Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robertt Gabriel, wakuu wa mikoa jirani na maafisa wa Serikali.
No comments:
Post a Comment