WAKANDARASI ACHENI KULIPUA ZINGATIENI VIWANGO - MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 16 March 2019

WAKANDARASI ACHENI KULIPUA ZINGATIENI VIWANGO - MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa hospitali ya WilayaRuangwa Machi 16.2019 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakandarasi wanaojenga majengo mbalimbali nchini yakiwemo na ya Serikali wahakikishe wanazingatia viwango na waache kulipua kazi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wawafundishe kazi mafundi wasaidizi wanaowatumia katika ujenzi wa miradi malimbali ili waweze kunufaika kwa kuongeza ujuzi.

Ametoa wito huo  Machi 16, 2019 alipotembelea miradi mbalimbali ya ujenzi wilayani Ruangwa mkoani Lindi, ukiwemo wa Hospitali ya wilaya.

Amesema Serikali inatoa pesa kulingana na kazi inayotakiwa kufanyika, hivyo amewataka wakandarasi wafanyekazi wanazopewa kwa kufauata taratibu za kiufundi na si ‘kulipua lipua’.

Pia, Waziri Mkuu amewaagiza wakandarasi hao kuwatumia mafundi wasaidizi waliopo kwenye maeneo ya karibu na miradi husika ili nao waweze kupata ajira.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka mafundi wasaidizi wahakikishe wanafanyakazi kwa bidii na uadilifu ili wawe mabalozi wazuri, jambo litalalowawezesha wengine kupata kazi.

"Nataka niwaambie mkifanya kazi kwa uaminifu wakandarasi watawachukua na kuwapeleka katika maeneo mengine wanayopata mradi. Jitumeni acheni uvivu mtafika mbali."

Amesema Serikali inatengeneza ajira kwa vijana kupitia wakandarasi wanaotekeleza miradi, hivyo wakandarasi wanatakiwa wawatumie mafundi wasaidizi walioko kwenye maeneo ya miradi.

Waziri Mkuu amesema amefarijika sana kuona vijana wanapata ajira na amewataka  watumie nafasi hizo kujifunza ufundi ili nao waje kuwa mafundi wakubwa na kuajiri wenzao.

Naye,  fundi msaidizi wa jengo la utawala katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa,Hamisi Ali amesema wanaishukuru Serikali kwa kuwapelekea miradi mkubwa ambayo inawapatia ajira.

Ali ametoa wito kwa vijana wengine waache kukaa mitaani na badala yake wajitokeze na wachangamkie fursa za ajira zilizopo kwenye maeneo yao na wafanye kazi hizo kwa bidii.

Waziri Mkuu ametembelea ujenzi wa hospitali ya wilaya, ghala, Ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Shule ya Seondari ya  Wasichana Lucas Maria.

No comments:

Post a Comment