Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Dk. Raphael Chegeni amezitaka Taasisi za Umma na Ofisi za Serikali ambazo bado hazijaanza kutumia huduma za Mawasiliano zinazotolewa na Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL kuanza mara moja kutumia Huduma hizo.
Dkt Chegeni amesema, Taasisi za Umma zina wajibu mkubwa wa kutumia Huduma za TTCL ikiwa ni kuunga mkono Jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kufufua Mashirika ya Umma.
Dk Chegeni ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari muda mfupi baada ya kamati yake kufanya ziara kwenye miradi inayoendeshwa na kusimamiwa na TTCL iliyopo jijini Dar es Salaam.
"..Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Kituo cha kutunza kumbukumbu 'Data Center' vinafanya kazi vizuri sana, Mkongo unawezesha Mawasiliano bora kwa Nchi nzima na Majirani zetu huku taarifa mbalimbali zikihifadhiwa katika kituo cha Data Centre lakini Miundombinu hii haitumiki ipasavyo. "Sisi kama Kamati tumebaini kwamba taasisi nyingi za Serikali bado hazijalitumia vizuri Shirika letu la TTCL na huduma zinazotolewa.
Hali hii inaonesha wazi kwamba bado hatujatoa msisitizo wa kutosha kwa Wizara, Idara za Serikali na Taasisi zote kwa ujumla kuwa Wateja wa TTCL ili Shirika letu liweze kujiendesha kwa Tija na Taifa kufaidika.
Aidha Kamati hiyo imeshauri taasisi hizo kutumia sasa mitandao na huduma za data za TTCL jambo ambalo ni muhimu kuliunga mkono shirika hilo la Umma. "...Kamati inaona ni vizuri taasisi za Serikali kutumia huduma hizi vizuri, kwani uwekezaji uliofanywa unatumika chini ya matarajio. Serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana na kama tunashindwa kutumia huduma hizo tunapasa hasara" alisisitiza Mwenyekiti huyo.
Kamati pia imeshauri gharama za uwekezaji unaofanywa na Shirika la TTCL ichukuliwe na Serikali kwa lengo la kuiondolea mzigo shirika. Uwekezaji huu mkubwa unapoachiwa katika shirika linashindwa kufanya kazi kwa ufanisi na kujikuta linabeba mzigo mkubwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Mhandisi Omari Rashid Nundu alisema Mwaka 2019, TTCL Corporation imejipanga vyema kuhakikisha kuwa Huduma za Shirika ina sambaa zaidi kote Nchini huku tukisimamia ubora na unafuu wa gharama kwa Wananchi wote.
"Tumekusudia kuendelea kufanya mageuzi makubwa ndani ya Shirika ili kuli wezesha kushindana kikamilifu katika Soko la Huduma za Mawasiliano Nchini sambamba na kutimiza wajibu wa kimsingi wa kuwa mchangiaji muhimu katika Pato la Taifa," alisema Mhandisi Rashid Nundu.
|
No comments:
Post a Comment