Muonekano wa jengo la mzani
mpya unaojengwa Dakawa Mkoani Morogoro. Mradi huo umekamilika kwa asilimia 98.
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Elias Kwandikwa, akifafanua jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu
kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kituo cha
Mizani kinachojengwa Dakawa Mkoani Morogoro, wakati kamati hiyo ilipokagua
mzani huo. Wa nne kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Suleiman Kakoso.
KAMATI ya
Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kujenga nyumba za watumishi kwenye
mzani mpya unaojengwa Dakawa Mkoani Morogoro ili kuwapunguzia adha wafanyakazi
watakaokuwa wakifanya kazi kituoni hapo.
Akizungumza mara baada ya
kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Sulemani Kakoso ameipongeza
Wizara na kuhakikisha kuwa pamoja na kujengewa nyumba hizo, pia Wizara
iwasimamie watumishi wa mzani vizuri ili kuepuka vitendo vya rushwa.
"Serikali imetumia
fedha nyingi kujenga mzani huu, nawapongeza sana lakini sasa ni muhimu
watumishi wa mzani huu wakasimamiwa vyema ili kuepuka vitendo vya rushwa
vinavyofanywa na watumishi wasio waaminifu" amesema Mwenyekiti. Kakoso.
Mwenyekiti Kakoso, ametoa
wito kwa wafanyabiashara wote nchini kuhakikisha wanazingatia sheria za mizani
kwa kupakia mizigo isiyozidi kiwango ili kulinda miundombinu ya barabara nchini.
Kwa upande wake Naibu Waziri
wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Serikali imejipanga
kuhakikisha changamoto zote zilizowasilishwa zinatatuliwa mapema ili kuongeza
ufanisi.
Naibu Waziri huyo ameieleza
kamati hiyo kuwa ujenzi wa mzani huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi
Machi mwaka huu kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 14.
Naye Mkuu wa Kitengo cha
Usalama na Mazingira kutoka Sekta ya Ujenzi Mhandisi Julius Chambo, amesema
ujenzi wa mzani huu unatokana na mzani wa Kihonda kuzidiwa na msongamano wa
magari kwa kuwa ni wa upande mmoja.
Ameeleza kuwa ukamilikaji wa
mzani huu utasaidia kuokoa muda kwa wasafirishaji na kuondosha msongamano uiopo
sasa katika mzani wa Kihonda kwani mzania huu utapima tu yale magari yanayoonekana
yamezidi uzito tu.
No comments:
Post a Comment