TAIFA STARS YAFUZU AFCON, 2019 NI ZAMU YETU..! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 24 March 2019

TAIFA STARS YAFUZU AFCON, 2019 NI ZAMU YETU..!

Mchezo wa Tanzania na Uganda

TIMU ya Taifa ya Taanzania imefanikiwa kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya kuifunga mabao 3-0 Timu ya Taifa ya Uganda mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo Tanzania na Uganda kutoka Kundi L ndio wamefuzu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019. Mabao ya Simon Msuva anayechezea timu ya Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, na mabeki, Erasto Edward Nyoni wa Simba SC na Aggrey Morris wa Azam FC yanaipeleka Taifa Stars AFCON.

Tanzania inakuwa mshindi wa pili wa kundi L akiwa na pointi zake nane, nyuma ya Uganda iliyomaliza na pointi 13 huku wakiziacha Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.   

Mchezo huo uliochezeshwa na refa Eric Arnaud Otogo Castane aliyepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Moussounda Montel na Marlaise Ditsoga Boris wote kutoka Gabon, hadi mapumziko Taifa Stars ilikuwa mbele kwa bao 1-0.

Bao hilo lilifungwa na Msuva, mchezaji wa zamani wa Yanga dakika ya 21 kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi ya mshambuliaji wa Simba SC ya nyumbani, John Raphael Bocco aliyeuwahi mpira uliowapita walinzi wa The Cranes kufuatia krosi ya beki wa kushoto Garidel Michael Mbaga.

Na kipindi cha pili, Taifa Stars baada ya kuongezewa maarifa na kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike ikaenda kuongeza mabao mawili. Alianza beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Nyoni kufunga kwa penalti dakika ya 51 baada ya Kirizestom Ntambi kuunawa mpira uliopigwa na Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta, mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji.

Aggrey Morris kufunga kwa kichwa dakika ya 57 akimalizia krosi nzuri ya mchezaji mwenzake wa zamani wa Azam FC, Bocco kutoka upande wa kulia.  Uganda wakapoteana baada ya bao hilo na kuwapa nafasi Tanzania kutawala zaidi mchezo huo, lakini wakaishia kukosa tu mabao ya wazi.

Mechi nyingine ya mwisho ya Kundi L leo, Cape Verde imelazimishwa sare ya 0-0 na Lesotho mjini Praia. Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kufuzu AFCON kihistoria, baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria na kwa ushindi huu, kila mchezaji atapatiwa donge nono la Sh. Milioni 10, ahadi ya Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde, chini ya Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. 

Tanzania iliwakilishwa na; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Simon Msuva/Thomas Ulimwengu dk89, Mudathir Yahya, John Bocco/Feisal Salum dk81, Mbwana Samatta na Farid Mussa/Himid mao dk70.

Huku Uganda; Dennis Onyango, Nico Wadada, Godfrey Walusimbi, Allan Kyambadde, Moses Waiswa, Farouk Miya, Kirizestom Ntambi, Dennis Awany, Thadeo Lwanga, Emmanuel Okwi na Patrick Kaddu.

No comments:

Post a Comment