Kaimu Mkurugenzi wa Idara
ya Barabara na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mhandisi John
Ngowi, akitoa
taarifa kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu
maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mtwara-Mnivata yenye urefu wa KM 50, wakati
kamati hiyo ilipotembelea mradi huo, Mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Elias Kwandikwa,
akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu
hatua za maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mtwara-Mnivata yenye urefU wa KM 50,
wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi huo, Mkoani Mtwara.
Mkurugenzi wa Viwanja
vya Ndege kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi),
Eng Emmanuel Raphael, akitoa taarifa kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Miundombinu kuhusu hatua za awali za uboreshwaji wa Kiwanja cha Ndege cha
Mtwara kutoka Daraja 3C kwenda Daraja 4E, wakati kamati hiyo ilipotembelea
mradi huo, mkoani Mtwara.
KAMATI ya Kudumu ya Bunge
ya Miundombinu imeishauri Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano kupeleka fedha kwa mkandarasi anayejenga barabara ya Mtwara -
Newala - Masasi (KM 210), sehemu ya Mtwara - Mnivata yenye urefu wa KM 50 ili
kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo.
Kamati hiyo imeonesha kutokuridhishwa na kasi ya mradi huo ambao mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 47 kwa sababu changamoto ya fedha kutolipwa kwa wakati.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Moshi Selemani Kakoso, amezungumza hayo wakati wa majumuisho ya ziara ya ukaguzi wa miundombinu mkoani Mtwara jana ambapo walitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unaojengwa na mkandarasi Dott Services kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 89.
"Kama kamati sijaridhishwa na maendeleo ya mradi huu na sababu kubwa ya kucheleweshwa imesemwa hapa ni kuchelewa kwa malipo ya mradi huu, hali hii itachelewesha maendeleo katika mikoa hii hivyo Wizara mjitahidi fedha zije ili mradi ukamilike na wananchi wapate maendeleo' amesema Mwenyekiti Kakoso.
Aidha kamati imetoa wito kwa Serikali katika kuuendeleza mkoa huo hasa katika uimarishaji wa miundombinu ya barabara ili kuunganisha mkoa huo na mikoa jirani na kurahisisha usafirishaji wa korosho zinazolimwa mkoani humo.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo anayesimamia masuala ya ujenzi, Mhe.
Elias Kwandikwa ameihakikishia kamati hiyo wizara itatenga fedha katika bajeti
ya mwaka 2019/20 ili ziweze kulipa madeni yanayodaiwa na mkandarasi huyo na
mradi huo ukamilike ili kukuza uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla kupitia
barabara hiyo.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo kwa kamati, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Barabara na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mhandisi John Ngowi, ameieleza kamati hiyo kuwa mkandarasi huyo anatakiwa kumaliza mradi mwezi Agosti mwaka huu na ameshaweka tabaka la kwanza la lami KM 8.5 na la tabaka la pili la lami KM 4.
Ameongeza kuwa mkandarasi amemaliza kazi ya ujenzi wa makalvati madogo 31, makalvati makubwa 4 na kazi zinaendelea ili kuhakikisha anakamilisha kwa kipindi cha mkataba.
Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imetembelea na kukagua kiwanja cha ndege cha mtwara ambacho kipo katika hatua za awali za uboreshwaji wake ambapo Serikali imepandisha hadhi ya kiwanja hicho kutoka Daraja 3C kwenda Daraja 4E kwa viwango vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
Mwenyekiti
wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Kakoso ameiagiza Seikali kumsimamia na kuhakikisha
mkandarasi M/S Beijing Construction Engineering Group anaongeza kasi ya ujenzi
ili aweze kukamilisha kwa wakati ambapo kazi zote zinatarajiwa kukamilika Mwezi
Septemba, 2020.
Kamati pia imeielekeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kuhakiisha wanapata hati miliki ya viwanja vyote hapa nchini ili kuepusha migogoro na wananchi wanaovamia maeneo ya viwanja vya ndege.
Uboreshwaji wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara ukikamilika utaimarisha usafiri wa anga, huduma za kibiashara, na kuchochea shughuli mbalimbali za ukuaji wa kiuchumi na kijamii katika ukanda wa kusini mwa nchi.
Kamati
imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kutekeleza mradi
wa upanuzi wa gati ya mtwara na kusisitiza mradi huo usimamiwe kwa kuzingatia
kanuni na taratibu za utekelezaji wa mradi.
No comments:
Post a Comment