Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Selemani Kakoso (aliyevaa shati nyeupe
na bluu) akijadiliana jambo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa
(katikati) na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Asumpta Mshama (wa kwanza kulia)
wakati Kamati hiyo ikikagua utekelezaji wa mpango wa anuani za makazi na
postikodi Kibaha, Pwani.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Elias Kwandikwa (wa
pili kushoto) akimpokea Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu,
Moshi Selemani Kakoso wakati akiwasili na Kamati yake kukagua utekelezaji wa
mpango wa anuani za makazi na postikodi, Kibaha mkoani Pwani.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Moshi Selemani Kakoso (aliyevaa shati ya
mistari ya bluu na nyeupe) akiambatana na Kamati yake, viongozi kutoka Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Ofisi ya Mkoa wa Pwani kukagua utekelezaji
wa mpango wa anuani za makazi na postikodi, Kibaha mkoani humo.
Kaimu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Jim
Yonazi akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu
wakati wa ziara yao ya kukagua utekelezaji wa mpango wa anuani za makazi na
postikodi Kibaha mkoani Pwani.
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mpango wa anuani za makazi na postikodi Kibaha Mkoani Pwani na kubaini kuwa utekelezaji wa mpango huo utafungua uchumi wa viwanda mkoani humo.
Hayo yameelezwa na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Moshi Selemani
Kakoso wakati wa kikao cha pamoja baina yake na wajumbe wa Kamati hiyo baada ya
kuhitimisha ziara yao ya kukagua utekelezaji wa mpango huo ambapo uongozi wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakiongozwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa,
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Mawasiliano), Dkt. Jim Yonazi na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Asumpta Mshama na
watendaji wengine kutoka Wizarani na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo walishiriki.
Kakoso amesema kuwa
anuani za makazi na postikodi ni muhimu kwa kuzingatia kuwa mkoa wa Pwani ni
mkoa ambao una uwekezaji mkubwa wa sekta ya viwanda kwa hiyo ni vema kukawa na
anuani za makazi kama tulivyoshuhudia.
Kakoso amesema kuwa wameiomba
Serikali iwekeze fedha za kutosha kwa ajili ya mradi kama huu kwa kuwa
utasaidia kutoa utambuzi kwenye maeneo mbali mbali hata wale wageni watakaokuja
kuwekeza huku watakuta miundombinu imeshaandaliwa ambayo itasaidia kufahamu
kwamba eneo hili limewekwa miundombinu ya Sekta ya Mawasiliano.
Pia, ameishauri
Serikali waendelee kulinda miundombinu inayowekezwa kwa kuwa watanzania walio wengi
wana asili ya uharibifu hasa kwenye miundombinu na wanachukulia kama chuma
chakavu, uwekezaji uweze kulindwa na Serikali ielimishe wananchi wafahamu na
kutambua kuwa mradi huu ni wa kwao.
Kakoso amefafanua kuwa
kazi ya Bunge ni kuangalia fedha zilizowekezwa ambazo zimepitishwa na Bunge na
tunapokuja kwenye ziara tunaangalia na kuhakikisha fedha zimefanya kazi ipi na
halmashauri ipi imenufaika ili tuweze kupitisha fedha nyingine wakati wa bajeti
ya Serikali.
Naye Naibu Waziri wa
Ujenzi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa ameishukuru
Kamati kwa kutembelea mradi wa anuani za makazi na postikodi ambapo hadi sasa
utekelezaji umefanyika kwenye halmashauri 12 na baadae utekelezaji utafikia
halmashuri 18.
“Mradi huu una faida
nyingi ambazo zimesemwa ambapo tunahitaji kuhama tupate huduma za kimtandao
ambapo tunapodumbukia kwenye uchumi wa kati na nchi ya viwanda, wazalishaji wetu
waweze kuuza kupitia njia ya mtandao, kama tunavyoona hata sasa hivi vijana
wengi wanafanya biashara kupitia njia ya mtandao, tunataka tuone kama Wizara
tunatoa mchango mkubwa kwa kuboresha anuani za makazi na postikodi kufanya
shughuli mbali mbali ziweze kwenda,” amesema Kwandikwa.
Kaimu Katibu Mkuu,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Jim
Yonazi amesema kuwa utekelezaji unaendelea ambapo mkandarasi ambaye ni Chuo cha
VETA, Dodoma kinafanya kazi ya kujenga miundombinu ya anuani za makazi na
postikodi na itasaidia kufungua Tanzania ili iweze kushiriki kikamilifu katika
uchumi wa kidunia kama ambavyo watu wanaweza kununua vitu kutoka nchi za mbali,
tunataka watu waweze kununua huduma na bidhaa kutoka nchini kwetu.
“Mpango wa anuani za
makazi na postikodi utasaidia sana utambuzi wa mahali bidhaa na huduma zilipo,
uzalishaji na viwanda vilipo hata kama mtu anatoka China, Urusi, Ujerumani
anaweza kujua kabisa kitu anachotafuta kiko wapi na mahali halisi ambapo tayari
pameshapewa anuani za makazi. Tunaamini baada ya muda si mrefu, nchi yetu nayo
itakuwa ni moja ya nchi ambazo itakuwa inaongoza kwa utambuzi wa mahali, makazi
ya watu, maeneo ya viwanda na maeneo mbali mbali ili biashara iweze kukua na
kuleta tija kwa uchumi wetu,” amesisitiza Dkt. Yonazi.
Akizungumza kwa niaba
ya wananchi wa Mkoa wa Pwani ambapo utekelezaji wa mpango wa anuani za makazi
na postikodi unaendelea, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Asumpta Mshama amesema
kuwa uwepo wa mpango huo utawasaidia kujua mtu gani yuko wapi, kitu gani kiko
wapi kwa kuwa mkoa wa Pwani ni ukanda wa viwanda na kwa kitendo hiki tumeingiza
Tanzania katika ulimwengu hivyo itarahisha mambo mbali mbali ya kibiashara na
itakuza uchumi wetu.
Mkuu wa Chuo cha VETA,
Dodoma, Ramadhani Mataka, amesema kuwa ameishukuru Wizara kwa kuipa VETA kazi
ya kuwa mkandarasi wa utekelezaji wa mpango huo
ambapo kazi wanayoifanya imewanufaisha wanafunzi kwa kuwa uchumi wa
viwanda hauwezi kusimama bila VETA. Pia, ameongeza kuwa VETA wametoa ajira kwa
mafundi waliopo kwenye jamii na wamechangia mapato ya Serikali kwa kulipa kodi
ya Serikali kiasi cha shilingi milioni 218.
Naye Mkurugenzi wa
Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Clarence
Ichwekeleza amesema kuwa hadi sasa
utekelezaji umefanyika kwenye kata 112 nchini kwenye maeneo mbali mbali
ambapo hadi sasa tumepata na kutumia shiilingi bilioni mbili kutekeleza mpango
huo na kazi hiyo inaendelea. Mhandisi Ichwekeleza anawahimiza na kuwaomba
wananchi, wakazi na madiwani wa maeneo mbalimbali waendelee kutoa ushirikiano
kwa mkandarasi VETA ili kuweza
kukamilisha utekelezaji wa mpango wa anuani za makazi na postikodi kwa kutoa
majina ya mitaa na idadi ya nyumba.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment