Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kulia) akimkabidhi
Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa kompyuta 25 kwa ajili ya sekondari za Wilaya ya
Ludewa, Njombe wakati wa ziara yake Wilayani humo. Anayeshuhudia katikati yao
ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Albert
Richard.
Mkuu wa Wilaya ya
Ludewa, Njombe, Mheshimiwa Andrea Tsere akimshukuru Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa tatu kulia aliyeketi) kwa niaba ya
wananchi kwa kuzipatia shule za Wilaya hiyo kompyuta 25 wakati wa ziara yake
Wilayani humo.
Nditiye amekabidhi
kompyuta hizo kwa Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa kwa niaba ya wananchi wa Wilaya
ya Ludewa ili ziweze kutumika kwenye shule mbali mbali zilizopo Wilayani humo.
“Nimeleta kompyuta 25
ili zigawiwe kwenye shule mbalimbali ili watoto wajifunze kutumia TEHAMA pamoja
na waalimu waliopewa mafunzo ya TEHAMA na taasisi yetu ya Mfuko wa Mawasiliano
kwa Wote (UCSAF)”, amesema Nditiye. Kompyuta hizo zimetolewa na UCSAF ambayo
inahusika na ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na
mvuto wa kibiashara.
Nditiye ameongeza kuwa
Wilaya ya Ludewa inafahamika katika kipindi cha miaka ya nyuma kwa kuwa moja ya
Wilaya saba nchini ambapo wanafunzi wake wana kipaji cha akili ukilinganisha na
Wilaya nyingine zilizopo nchini ambapo ameona ni vema kuwapatia wanafunzi wa
shule za Wilaya hiyo kompyuta hizo ili waweze kuongeza ufaulu, kujenga uelewa
na kupata maarifa ili waweze kuwa wanafunzi vinara kama iliivyokuwa imezoeleka
katika kipindi cha miaka ya nyuma. Pia, amesema kuwa Tanzania inaongoza katika
matumizi ya TEHAMA katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mara baada ya kupokea
kompyuta hizo kwa niaba ya wananchi, Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa alimuomba
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere kuwa, kuwe na kituo kimoja cha kutunga mitihani
Ludewa ili waalimu watunge mtihani wa aina moja na waweze kumaliza kufundisha
masomo ya kiada na ziada kama walivyopanga kwa muhula husika wa masomo ili
waweze kuwapima wanafunzi wote kwa pamoja.
Naye Mkuu wa Wilaya
hiyo, Andrea Tsere alimueleza Nditiye kuwa wataweka intaneti kwenye kompyuta
hizo ili waalimu na wanafunzi waweze kupata notisi. Pia, amesema kuwa kompyuta
hizo zitatumika kuinua kiwango cha elimu na zimefika muda muafaka.
“Mmetusaidia sana,
umeingia kwenye akili yangu ya kuinua kiwango cha elimu Ludewa,” amesisitiza
Tsere wakati akimshukuru Nditiye kwa kuzipatia shule za Wilaya yake kompyuta
25. Tsere amewataka waalimu wakuu wa shule kuzitunza kompyuta hizo na
kuzifanyia matengenezo pindi inapohitajika badala ya kuacha ziharibike na
pasipo kuzipanga vizuri kwa sababu ni vifaa vya Serikali badala yake wanapanga
lini wavichukue badala ya kuzitunza vizuri ili zisaidie wanafunzi wengi na kwa
muda mrefu. Aidha, amesisitiza kwa waalimu hao kuwa kompyuta zikipotea na wao
wapotee.
Katika hatua nyingine,
Nditiye amewaeleza wananchi hao kuwa, Wizara yake ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano kupitia UCSAF imetoa ruzuku kwa kampuni ya simu ya Halotel na
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ili wajenge minara 11 kwenye maeneo ya
mwambao kwa wananchi waishio Wilayani Ludewa kwa kuwa hawana mawasiliano.
“Tunahitaji Ludewa
iwasiliane na dunia,” amesisitiza Nditye. Amefafanua kuwa minara tisa imejengwa
na kampuni ya Halotel na miwili ni ya TTCL.
Vile vile, ameongeza
kuwa, ujenzi wa meli ya abiria waishio Ludewa kwa ajili ya usafiri wa Ziwa
Nyasa umekamilika ambapo kwa sasa meli hiyo inafanyiwa majaribio kabla ya
kuanza safari zake na Serikali inakamilisha ujenzi wa gati za kushusha na
kupakia abiria kwenye mwambao wa ziwa hilo kwenye maeneo ya Manda, Lupingu,
Nsele, Yiga na Nkanda ambapo meli hiyo inatarajiwa kuanza safari zake za kutoka
Ludewa, Njombe hadi Kyela, Mbeya mwezi Aprili mwaka huu.
“Tunataka Lupingu hadi
Matema watu wapite kwa lami,” amefafanua Nditiye. Ameyasema hayo wakati
akiongea na wananchi wa Ludewa mjini na kuwaeleza kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni
kuhakikisha kuwa barabara ya Lusitu – Mawengi yenye urefu wa kilomita 50 inajengwa
kwa kiwango cha zege kwa gharama ya shilingi bilioni 159 ambapo tayari
mkandarasi wa kutoka nchi ya Korea yupo na anaendelea na ujenzi wa barabara
hiyo ili iweze kupitisha madini ya Mchuchuma na Liganga.
Ngalawa amewaeleza
wananchi kuwa anamshukuru Nditiye kwa kuwa alifanya ziara kutoka Lupingu hadi
Manda mwaka jana mwezi wa tatu akiwa na miezi minne tu tangu alipoteuliwa kuwa
Naibu Waziri na kushuhudia ukosefu wa mawasiliano kwa wananchi waishio mwambao
na sasa minara 11 imejengwa ambapo tayari minara mitatu ya Nkanda, Mawengi na
Mahong’olo imewashawa na meli ya abiria pia itaanza safari zake.
Tsere alimshukuru Ngalawa
kwa kumleta Nditiye ambapo alisafiri na boti siku nzima Ziwani mwaka jana mwezi
wa Machi na kushuhudia ukosefu wa mawasiliano kwa kuwa tangu dunia iumbwe
wananchi wa mwambao hawajawahi kupata mawasiliano na sasa wanawasiliana.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment