TARI-TORITA YABAINI NJIA YA KUPUNGUZA GHARAMA KILIMO CHA TUMBAKU - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 17 September 2026

TARI-TORITA YABAINI NJIA YA KUPUNGUZA GHARAMA KILIMO CHA TUMBAKU

Na Godwin Myovela, Dodoma

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania kupitia kituo chake cha utafiti wa tumbaku (TARI-TORITA) imeendelea na juhudi za kisayansi kutafuta njia zitakazosaidia kupunguza gharama za uzalishaji wa tumbaku, kuongeza tija na kulinda afya ya udongo.


Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Kituo cha TARI-TORITA, Kilichopo Tumbi, Tabora, Dk. Jacob Bulenga Lisuma, wakati yeye pamoja na wataalamu wake walipokutana na wadau wa mnyororo wa zao la tumbaku katika Hoteli ya Rafiki, Dodoma.


Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuwafahamisha wadau kuhusu matokeo ya tafiti zilizofanywa na TARI-TORITA katika msimu wa 2025/2026, pamoja na kupata maoni yao kuhusu namna teknolojia hizo zinavyoweza kuwasaidia wakulima.


Utafiti huo uliongozwa kitaalamu na wataalamu mbalimbali wa TARI-TORITA, akiwemo Magdalena Raphael Ntatilwa, chini ya usimamizi wa Dk. Lisuma.


Virutubisho vyenye lengo la kupunguza gharama


Miongoni mwa tafiti zilizowasilishwa ni matumizi ya Eco Plus, kirutubisho kinachowekwa kwenye majani ya mmea.


Kwa mujibu wa wataalamu, matumizi yake yanaweza kusaidia kuongeza virutubisho kwenye mmea na kuupa uwezo wa kustahimili changamoto zinazohusisha magonjwa na mashambulizi ya wadudu.


Utafiti huo pia umeangalia namna ya kupunguza kiwango cha mbolea kinachotumika bila kushusha matokeo yanayotarajiwa.


Matokeo ya awali yameonyesha kuwa matumizi ya gramu 24 za NPK pamoja na teknolojia hiyo yanaweza kutoa matokeo mazuri yanayokaribiana na matumizi ya kiwango cha kawaida cha gramu 30 za NPK.


Kwa mkulima, jambo hili lina maana kubwa kwa sababu kupunguza matumizi ya pembejeo bila kupunguza tija kunaweza kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji.

Carbon ya kuboresha afya ya udongo


Utafiti mwingine umehusisha Reacted Carbon Product, yenye asilimia 22 ya carbon, asilimia 7 ya nitrogen na asilimia 0.64 ya zinc.


Bidhaa hiyo huwekwa kwenye udongo siku tatu baada ya kupandikiza miche.


Wataalamu wanasema matumizi yake yanaweza kusaidia udongo kushikamana vizuri na hivyo kuongeza uwezo wa kuhifadhi virutubisho vinavyowekwa shambani.


Kwa mantiki hiyo, mbolea inapowekwa kwenye udongo wenye uwezo mzuri wa kushikilia virutubisho, uwezekano wa virutubisho kupotea kwa haraka unapungua.


Hili ni eneo ambalo watafiti wanaona linaweza kuwa muhimu si tu katika kuongeza tija, bali pia katika kuboresha afya ya udongo kwa ajili ya kilimo endelevu.


Richfarm Booster nayo yafanyiwa utafiti


TARI-TORITA pia imefanya utafiti kuhusu Richfarm Booster, ambayo imekuwa ikitumika sambamba na mbolea huku kiwango cha mbolea kikishushwa kwa kiasi.


Kwa mujibu wa matokeo yaliyowasilishwa, teknolojia hiyo imeonyesha matokeo mazuri katika majaribio yaliyofanyika.


Hata hivyo, wadau walitaka jambo moja liwekwe wazi zaidi: gharama halisi za matumizi ya teknolojia hizo.


Walisema ni muhimu kujua bei ya kila kirutubisho, gharama ya matumizi kwa ekari na kiasi ambacho mkulima anaweza kuokoa ili waweze kufanya uamuzi wa matumizi yake kwa uhalisia wa kiuchumi.


TARI-TORITA: Utafiti haujaishia hapa


Akizungumza kuhusu hatua zinazofuata, Dk. Lisuma alisema mkutano huo haukuwa mwisho wa mchakato.


Alisema TARI-TORITA itachukua maoni yaliyotolewa na wadau na kuyafanyia maboresho kabla ya kuwasilisha hatua zinazofuata kwenye vikao vya Halmashauri Kuu ya Tumbaku.


Alieleza kuwa maboresho hayo yataanzia kwenye Kamati ya Ufundi ya Halmashauri Kuu ya Tumbaku, ambayo itapata nafasi ya kutoa mapendekezo kuhusu bidhaa au teknolojia ipi inaonekana kufaa zaidi kuanza kutumika katika zao la tumbaku.


Kwa mtazamo huo, utafiti haupaswi kubaki kwenye maabara au kwenye karatasi pekee, bali unapaswa kuunganisha mtafiti, mkulima, kampuni, wataalamu na taasisi zinazohusika ili teknolojia inayopendekezwa iwe na tija kwa mtumiaji wa mwisho.


Mbegu mbili bora kutoka TORITA


Mbali na utafiti wa pembejeo, TARI-TORITA pia imefanya hatua nyingine muhimu kwa kuzalisha aina mbili za mbegu bora za tumbaku.


Aina hizo ni mbegu ya tumbaku inayokaushwa kwa mvuke na nyingine inayokaushwa kwa hewa.


Mbegu hizo, zinazojulikana kama TRF na TRB, zimeonyesha matokeo yanayoweza kulinganishwa na baadhi ya mbegu zinazotoka nje ya nchi ambazo bado hazijasajiliwa.


Dk. Lisuma alisema kituo hicho kimefurahishwa na maoni chanya kutoka kwa wadau, hasa taarifa kwamba mbegu zinazozalishwa na TARI-TORITA zimekuwa zikikubalika na wakulima.


Kwa mujibu wake, changamoto iliyobaki ni kuongeza uelewa na kuzitangaza zaidi ili mnyororo mzima wa sekta ya tumbaku uzifahamu.


Mbegu halali zitambulike kwa lebo


Dk. Lisuma alieleza kuwa kwa utaratibu uliopo, TARI-TORITA huingia mikataba na kampuni za mbegu ambazo huwasambazia wakulima mbegu kwa mujibu wa makubaliano.


Kwa mbegu mpya zilizofanyiwa utafiti na TARI-TORITA, amesema maandalizi ya uzalishaji na uuzaji yanaendelea kwa msimu ujao.


Amesema TARI-TORITA tayari imeomba lebo kutoka TOSCI, ambayo itatumika kutambulisha mbegu hizo rasmi.


Wakulima wametakiwa kuwa makini na kuzipata kupitia njia rasmi na kampuni zilizoingia mikataba husika, ili kuepuka mbegu zisizo na ubora au zisizotambulika.


Kapoma: Carbon ni fursa ya kiuchumi


Mgeni rasmi katika mkutano huo, Mbunge wa Viti Maalum Josephine Kapoma, alitoa wito kwa TARI-TORITA kuangalia pia fursa za kiuchumi zinazoweza kutokana na tafiti za carbon.


Akizungumzia Reacted Carbon Product, Kapoma alisema matumizi ya carbon kwenye udongo yanaweza kuwa sehemu ya juhudi za kuboresha afya ya udongo na uwezo wake wa kutoa virutubisho kwa mimea.


Alisema dunia kwa sasa inaweka msisitizo mkubwa katika masuala ya mazingira, hivyo TARI-TORITA inapaswa kuangalia namna teknolojia hiyo inaweza kuwa fursa ya kimazingira na kiuchumi.


Kapoma aliishauri TARI-TORITA kushirikiana na NEMC na taasisi nyingine zinazohusika na mazingira ili kuona namna tafiti hizo zinavyoweza kuunganishwa na fursa za kifedha zinazotokana na uhifadhi wa mazingira na carbon.


Wadau waipongeza TARI-TORITA


Mtaalamu wa Agronomia kutoka kampuni ya JTI, Ayoub Omary, alisema amefurahishwa na mwelekeo wa TARI-TORITA wa kujikita katika kupunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima.


Alisema juhudi za kupunguza matumizi ya pembejeo huku zikilenga kuongeza tija na ubora wa tumbaku zinaweza kumsaidia mkulima kupata bei nzuri na kuongeza uzalishaji katika eneo analolima.


Omary pia alisisitiza umuhimu wa tafiti zinazolenga kufanya kilimo cha tumbaku kuwa endelevu bila kuathiri mazingira na afya ya udongo.


Aliitaka TARI-TORITA kuendelea kufanya tafiti zaidi zitakazosaidia kupunguza athari za kilimo cha tumbaku kwa mazingira na kuhakikisha zao hilo linaendelea kuwa na nafasi katika uchumi wa wakulima.


Mara yawasikia wataalamu wa TARI-TORITA


Meneja Mkuu wa WAMACU, Samuel Marwa, alisema mkutano huo umekuwa fursa muhimu kwao kwa kuwa ilikuwa mara yao ya kwanza kupata mafunzo na kusikia kwa kina kuhusu tafiti zinazofanywa na TARI-TORITA.


Alisema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa kuhusu kazi ya kituo hicho na teknolojia zinazoweza kutumika katika kuongeza tija ya zao la tumbaku.


Marwa alisema wadau kutoka Mkoa wa Mara wataendelea kutumia maarifa hayo kwa lengo la kuimarisha uzalishaji wa tumbaku na ustawi wa wakulima.


Kapoma aahidi kulipeleka suala Bungeni


Kwa upande wake, Kapoma aliwahakikishia wadau kwamba atawasilisha ombi maalum Bungeni la kuitaka Serikali kuongeza bajeti ya TARI-TORITA ili kituo hicho kiweze kuendelea kufanya tafiti na kuleta mapinduzi ya kisayansi katika sekta ya tumbaku.


Kwa utani uliowafanya washiriki kushangilia, Kapoma alisema:


"Msiwe na wasiwasi. Nitakapofika Bungeni, Bunge lijalo nitapiga kama Pacome au Mpanzu; nitaulizia maswali haya yote yaliyowasilishwa na wadau ambayo hayajapatiwa ufumbuzi."


Alisema atazungumzia zao hilo kwa nguvu zake zote na kuwakaribisha wadau kuendelea kumpa maoni ambayo anaweza kuyawasilisha katika Bunge lijalo.


Akihitimisha kwa kuunganisha hoja hiyo na mchezo wa soka, Kapoma alisema kwa utani kuwa:


"Nawahakikishia, kama Yanga vile inavyofanya vizuri, na zao hili litaendelea kufanya vizuri."

Muonekano wa mashamba ya Tumbaku yanayo simamiwa na TARI.

Wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa zao la Tumbaku wakipokea taarifa za utafiti mpya uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa zao hilo TARI-TORITA kilichofanyika Dodoma jana


Wadaau wa Mnyororo wa zao la Tumbaku wakiwa katika picha ya pamoja.
 

No comments:

Post a Comment