VIJANA wa Chama cha Skauti Tanzania (Tanzania Scouts Association - TSA), Mkoa wa Tanga, wameelezwa kuwa watashiriki Mashindano ya Afrika Mashariki 2026.
Hayo yamebainishwa na Afisa Elimu Mkoa wa Tanga, ambaye pia ni Rais wa chama hicho mkoani humo, Emmanuel Kisongo, ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati akizungumza katika hafla fupi ya kuwapokea Skauti waliokuwa kwenye mashindano ya kitaifa jijini Dodoma. Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Septemba 11, 2026.
Mashindano hayo yalianza Septemba 6, 2026, na kufikia tamati Septemba 10, 2026, jijini Dodoma.
“Tumeambiwa hapa kuwa kuna mashindano ya 'East Afrika', mtakwenda. Mtakwenda kwa sababu na sisi tupo, hatuwezi kubaki nyuma. Mkienda tutapata vitu vingi, mtakuja kutusaidia. Mlienda kwenye umitashunta, hamkufanya vizuri kwa kukosa ukakamavu, kumbe majemedari mpo hapa. Nitahakikisha kila shule inakuwa na vijana wa Skauti,” alisema Kisongo.
Akizungumzia mashindano ya kitaifa na jinsi walivyofanya vizuri, Kisongo alimshukuru Mungu na Skauti hao kwa kazi nzuri waliyoifanya hadi kupata ushindi.
“Mmetimiza wajibu wenu na sisi tumefurahi sana. Mmetupa heshima na matumaini yangu kwamba mtaendelea kuiing’arisha Tanga kokote mtakakosimama. Mtatupigania na hizo kanda nane lazima ziwe na uwakilishi,” alisema Kisongo.
Kisongo alitumia nafasi hiyo kuishukuru Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa mchango wao mkubwa walioutoa na kufanikisha vijana hao kufanya vizuri katika mashindano hayo.
“Kipekee Tanga Jiji asanteni sana na nyinyi Skauti wetu, mmeonesha uzalendo mkubwa, mmewakilisha wenzenu vizuri, mmesimama kwa miguu yenu vizuri. Sisi viongozi wenu tutawaenzi daima, tutawapa ushirikiano wa hali na mali,” alisema Kisongo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Skauti Mkoa wa Tanga, ambaye pia ni Katibu wa Afya wa mkoa huo, Dk. Frank Mhilu, akizungumzia mashindano hayo alisema kuwa kwa utaratibu, mashindano hayo yanaanzia ngazi ya wilaya, ambapo washindi huingia ngazi ya mkoa na hatimaye hupatikana timu inayokwenda kushiriki ngazi ya Taifa.
“Katika ngazi ya Kimkoa walikuja washiriki, wilaya ya Kilindi, Lushoto alikuja mshiriki mmoja tu ambaye hakuwa na sifa ya ushiriki na Pangani pia. Lakini Kilindi, Handeni na Tanga Jiji walileta vikosi vya vijana ambao walikuwa na sifa ya kushindanishwa,” alisema Dk. Mhilu.
Dk. Mhilu alisema Tanga Jiji walifanikiwa kushinda vikosi vinne ambavyo vilikuwa na sifa ya kushiriki ngazi ya kitaifa, pamoja na Handeni walioshinda kikosi kimoja cha Rovers cha wanawake.
Hata hivyo, alisema wakati zimebaki siku moja, wenzao kutoka Handeni walisema hawataweza kushiriki ngazi nyingine iliyofuata, hivyo walibaki na vikosi vinne kutoka Jiji la Tanga ambavyo vilishiriki na kufanikiwa kufanya vizuri katika mashindano hayo.
KUHUSU CHAMA
CHA SKAUTI TANZANIA
Chama cha Skauti Tanzania (Tanzania Scouts Association - TSA) ni shirika kubwa la harakati za vijana nchini Tanzania, lililoanzishwa mwaka 1917 Tanganyika na visiwani Zanzibar mwaka 1912.
Shirika hilo lilisajiliwa rasmi kisheria nchini mwaka 1963 na kuwa mwanachama kamili wa Shirika la Harakati za Skauti Duniani.
Madhumuni makuu ya chama hicho ni kukuza uzalendo, stadi za maisha, maendeleo ya uongozi kwa vijana, moyo wa kujitegemea na utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii.
Nembo rasmi ya TSA ina picha ya kichwa cha twiga, huku kaulimbiu yao kuu ikiwa “Uwe Tayari.”
Viongozi wa Skauti Mkoa wa Tanga wakiwa meza kuu. Katikati ni Afisa Elimu Mkoa wa Tanga, ambaye pia ni Rais wa chama hicho mkoani humo, Emmanuel Kisongo, Kamishna wa Skauti Mkoa wa Tanga, ambaye pia ni Katibu wa Afya wa mkoa huo, Dk. Frank Mhilu (kushoto) na Kamishna wa Skauti Wilaya ya Tanga, Rahimu Ibrahim.Kamishna wa Skauti Wilaya ya Tanga, Rahimu Ibrahim, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Skauti Mwanzema Ally Mwanzema, akitoa taarifa fupi ya mashindano hayo.
Kikosi cha Skauti Rever- Traole wakiwa kwenye hafla hiyo.
Taswira ya hafla hiyo.
Viongozi wa Skauti walioshiriki katika mashindano hayo wakitambulishwa kwenye hafla hiyo.
Kikosi cha Rovers cha Wanawake kikitambulishwa kwenye hafla hiyo.
Utambulisho ukifanyika kwenye hafla hiyo.
Naibu Kamishna wa Skauti Wilaya ya Tanga, Josephine Naaman (kulia) na Mratibu wa Mawasiliano Skauti Mkoa wa Tanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mashindano hayo Jijini Dodoma wakiwa kwenye hafla hiyo.
Mratibu Maendeleo ya Jamii Miradi Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati Skauti Mkoa wa Tanga, Sakina Msafiri Muslihi, akishiriki hafla hiyo.


No comments:
Post a Comment