KAMPENI YA ULINZI WA MTOTO DHIDI YA UKATILI WA KINGONO- “1-5-5 NAMLINDA”
“Mlinde mtoto afurahie utoto wake, ujana wake na uzee wake”
Ukatili dhidi ya watoto umekuwa ni sehemu ya maisha ya watoto wengi nchini. Mojawapo ya aina za ukatili unaokumba kundi hili ni ukatili wa kingono.
Mnamo mwaka 2011, nchi yetu ilitoa taarifa ya utafiti uliofanyika kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto, utafiti huo uligundua kuwa karibia mmoja kati ya wasichana watatu na mmoja kati ya wavulana saba wamekutana na ukatili wa kingono kabla ya kutimiza miaka 18.
Hata hivyo, kulingana na utafiti huo, wengi wa watoto hawatoi taarifa juu ya vitendo hivyo, wachache wanatafuta huduma na wachache zaidi wanafanikiwa kupata matibabu au msaada wanapotoa taarifa ya matukio hayo. Pia, ripoti iliyotolewa na Kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) zinaonyesha kuwa matukio ya ukatili wa kingono miongoni mwa watoto yanaongezeka nchini.
Kulingana na ripoti hiyo iliyotolewa Juni 2018, wastani wa watoto 394 wamebakwa kila mwezi katika maeneo mbalimbali Tanzania bara, huku ulawiti wa watoto ukiongezeka kutoka matukio 12 kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2017 hadi matukio 533 kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2018, na mikoa inayoongoza kwa matukio hayo ni Dar es salaam na Iringa.
Vitendo hivi havikubaliki katika jamii kwani ni kinyume cha haki za binadamu na mikataba mbalimbali ya kimataifa, na kikanda iliyoridhiwa na serikali juu ya ulinzi wa mtoto dhidi ya aina zote za ukatili wa kijinsia. Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa haki za mtoto wa mwaka 1989, tamko la Afrika juu ya haki na ustawi wa mtoto la mwaka 1990.
Vitendo hivi vinarudisha nyuma maendeleo ya mtoto na taifa kwa ujumla. Miongoni mwa athari zitokanazo na ukatili wa kingono dhidi ya watoto ni pamoja na watoto kuathirika kisaikolojia, maambukizi ya magonjwa ya zinaa na UKIMWI, mimba za utotoni, na kubwa zaidi ni kuhatarisha ustawi wa taifa na kuchochea uongezeko la vitendo hivi katika jamii.
Kutokana na takwimu hizo, hali ya tatizo ni kubwa sana, jambo ambalo limesukuma TGNP Mtandao kuja na kampeni ya ulinzi wa mtoto iitwayo 1-5-5 Namlinda. Kampeni hii inachangia katika jitihada za serikali kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Kutokomeza dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) unaolenga kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoti kwa asilimia 50 ifikapo 2022.
Kampeni hii inalenga kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za ukatili wa kingono kwa watoto na umuhimu wa kuwalinda dhidi aina hiyo ya ukatili, kutathmini na kuibua mijadala katika jamii juu ya hali halisi ya ukatili wa kingono, kuhamasisha jamii kuzuia vitendo hivi visitokee na kutoa taarifa mara waonapo matukio hayo ya ukatili wa kingono kwa watoto ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Kampeni hii pia inalenga kujenga nguvu za pamoja na wadau mbalimbali nchini katika kuweka mikakati ya pamoja ya ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili wa kingono na kuhakikisha kila mtu katika jamii anajisikia kuwajibika kumlinda mtoto.
Hivyo, kampeni hii imelenga kuwafikia wanawake, wasichana, wavulana, wanaume, viongozi wa dini, serikali, jamii, vyombo vya habari, madawati ya jinsia polisi, asasi za kiraia, wadau wa maendeleo, makungwi, watoa huduma za afya,wanaharakati, watoa huduma za usafiri wa umma kama bodabodaa na daladala pamoja na wabunge, na wanasiasa.
Kampeni hii inatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 27 Februari 2019 ambapo wawakilishi wa wadau mbalimbali ambao ni walengwa wa kampeni watashiriki ili kupitishwa katika kampeni hii na kujadiliana kwa pamoja wajibu wa kila kundi katika ulinzi wa mtoto. Kampeni hii inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na mkuu wa jeshi la polisi Tanzania-IGP Saimoni Sirro.
Jamii inawajibu wa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Hii ni kwa mujibu wa sheria ya mtoto na. 21 ya mwaka 2009 na mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
TGNP Mtandao, inaamini kuwa ikiwa kila mtu katika jamii atatimiza wajibu wake vizuri wa kumlinda mtoto, Tanzania billa ukatili wa kingono kwa watoto inawezekana. Pia, TGNP inaamini kuwa ikiwa watoto watakuwa huru dhidi ya aina zote za ukatili wa kijinsia, tutakuwa na taifa imara lenye viongozi bora, nguvukazi iliyo na afya njema na tutaweza kufikia malengo ya dunia ya maendeleo endelevu. Madai yetu katika kampeni hii ni pamoja na:-
Kuitaka jamii kuguswa na tatizo la ukatili wa kigono kwa watoto wakiwa nje na ndani ya shule Jamii ichukue hatua za kumlinda mtoto popote alipo. Kila mmoja alipo asimamie ulinzi wa mtoto vyombo vya habari vitoe elimu kwa wingi juu ya athari za ukatili wa kingono kwa watoto, faida ya kuwalinda watoto na kuendelea kukemea vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya watoto.
Serikali kuu, serikali za mitaa na vyombo vya dola visimamie kikamilifu sheria ya kudhibiti uchawi na. 12 ya mwaka 1998(The Witchcraft Act). Ambayo imeainisha adhabu kwa watu wanaoendesha vitendo vya kishirikiana vinavyoweza kuwadhuru watoto na kuongeza vitendo vya ukatili wa kingono kama ubakaji.
Tunatoa rai kwa jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola kama wadau wa kutekeleza MTAKUWAA (NPA) kuhakikisha watoto wanakuwa salama kwa kuimarisha ulinzi katika maeneo yote yanayotajwa kuwa sio salama kwa watoto nchini.
Kupitia kampeni hii jamii yote, kupitia mtu mmoja mmoja na kikundi inapaswa kumlinda na kuhakikisha ustawi wa mtoto. Tunaitaka serikali na wadau kuzijengea uwezo kamati za ulinzi wa watoto ili waweze kutimiza majukumu yao ikiwemo kubaini maeneo hatarishi katika kijiji/ mtaa na kupanga mikakati ya kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
No comments:
Post a Comment