Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) akiangalia ramani ya jengo la Wizara linalotarajiwa kujengwa katika eneo la mji wa Serikali, Ihumwa, Dodoma. |
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amelitaka Shirika la Nyumba na Taifa, NHC, lililopewa kandarasi ya kujenga ofisi za Hazina katika eneo la Mji wa Serikali-Ihumwa mkoani Dodoma, kuhakikisha kuwa inajenga ofisi hizo kwa umakini, umahiri na viwango vya ubora wa vya juu vinavyokwenda sambamba na hadhi ya Wizara ya Fedha na Mipango.
Dkt. Kijaji ametoa rai hiyo kwa uongozi wa Kampuni ya Ujenzi ya Shirika la Nyumba Tanzania-NHC, baada ya kutembelea eneo zitakapojengwa Ofisi za kudumu za Wizara hiyo katika mji huo wa Serikali ambapo jengo la kwanza litakalo gharimu shilingi bilioni moja, linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2018.
Aidha, Dkt. Kijaji ameielekeza NHC kuhakikisha kuwa inajenga jengo kubwa la Wizara kwa kuzingatia teknolojia inayo hifadhi mazingira ikiwemo kuweka miundombinu ya kuwezesha kupatikana kwa nishati mbadala ya umeme katika jengo hilo.
"Muda wa kukaa mjini Dodoma umemalizika, tunataka ukamilishe jengo hilo kwa wakati na kwa viwango vya juu ili Wizara yote Ihamie hapa Ihumwa na tunataka Bajeti Kuu ya Serikali iandaliwe hapa na ikasomwe Bungeni tukitokea Ihumwa, hilo ni jambo la muhimu sana" aliongeza Dkt. Kijaji
Kwa upande wake, Msimamizi wa Ujenzi wa Jengo la Wizara ya Fedha na Mipango kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mhandisi Haikamen Mlekio, amemhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Ashatu Kijaji, kwamba watahakikisha majengo ya ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango katika Mji wa Serikali wa Ihumwa yanajengwa kwa viwango vya hali ya juu.
No comments:
Post a Comment