SHERIA MPYA YA ZANA ZA KILIMO KUCHOCHEA MAPINDUZI YA VIWANDA – MTIGUMWE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 6 December 2018

SHERIA MPYA YA ZANA ZA KILIMO KUCHOCHEA MAPINDUZI YA VIWANDA – MTIGUMWE

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Zana za Kilimo Wizara ya Kilimo, Mhandisi Joseph Lubilo akitoa maelezo ya utangulizi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe aliyevaa koti la kahawia katikaki akiwa pamoja na Mhandisi Peter Chiswalo kulia kwake ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo,  jana katika ukumbi wa Mvuvi House, Jijini Dar es Salaam.

KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Zana za Kilimo wenye lengo la kupitia rasimu ya maboresho ya Sheria ya Zana za Kilimo nchini na kusisitiza kuwa Sheria mpya itatosaidia kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo ambayo ndiyo malighafi za viwanda vingi nchini.

Akifungua mkutano huo, Mhandisi Mtigumwe amesema kilimo cha Tanzania kimepitia mageuzi mengi ya kisera na kimkakati na kwamba maboresho ya sheria ambayo Wadau wamekutana ili kuiboresha Sekta ya Zana za Kilimo, yana nafasi kubwa ya kuongeza tija na uzalishaji mkubwa katika kilimo na kuongeza kuwa ni vyema Wataalam wakijikita katika kutoa maoni na michango mizuri itakayochangia katika kuboresha.

Mhandisi Mtigumwe amekaririwa akisema “Lengo la mkutano huu ni kuwaleta pamoja Wadau wa zana za kilimo ili kushiriki  katika kuchangia Andiko la Sheria ya Zana za Kilimo nchini kwa kutoa maoni na ushauri kuhusu Sheria inayotaka kupendekezwa”. 

“Aidha, Sheria hii inatarajiwa kuleta uwiano mzuri wa maamuzi kati ya Watengenezaji, Waagizaji, Wasambazaji na Watumiaji wa zana na mashine mbalimbali za kilimo ili kuimarisha na kutambua wajibu wa kila Mdau”. Amekaririwa Katibu Mkuu.

Mhandisi Mtigumwe ameongeza kuwa azma ya Serikali ni kuendeleleza mapinduzi ya kweli ya kilimo yatakayosaidia katika kuongeza uzalishaji, ufanisi na tija katika sekta ya kilimo. 

Lengo likiwa ni kukiwezesha kilimo chetu kiwe cha kisasa na cha kibiashara kupitia Sera ya Kilimo (2013) pamoja na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II) ambazo zinaweka mkazo katika kuongeza tija katika uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kuweka mazingira wezeshi ya kiuzalishaji na kiuwekezaji.

Katibu Mkuu amesema lengo hilo, mkazo umewekwa katika kuhakikisha kunakuwa na uwekezaji zaidi katika Sekta ya Kilimo ili kuongeza bidhaa za viwandani kwa kutumia zana bora za kilimo, pembejeo za kilimo hususan mbegu bora, mbolea na madawa ya kudhibiti visumbufu vya mimea.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Zana za Kilimo, Mhandisi Joseph Lubilo amesema katika kipindi kirefu nchini kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya zana za kilimo.  

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na ubora hafifu wa mashine na zana za kilimo zinazoingizwa na kutengenezwa nchini; Ugumu wa upatikanaji na bei kubwa ya vipuri;  kukosekana kwa Vituo vya kutoa huduma baada ya mauzo karibu na watumiaji wa zana za kilimo na kukosekana kwa ujuzi wa kutosha kwa Waendesha mitambo na  masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo ya zana za kilimo.

Mhandisi Lubilo amesema sheria inayokuja ina lengo la kuboresha changamoto hizo na kwamba Mkulima atakuwa salama na atalindwa Kisheria tofauti na ilivyokuwa hapo kabla.

Mhandisi Lubilo amekaririwa akisema “Baadhi ya faida tunazotarajia kuziona mara sheria hii ikipita ni pamoja na Wakulima watapata zana bora za kilimo zinazokidhi viwango kwa wakati; Kutaongezeka matumizi bora ya zana za kilimo na kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa tija na kibiashara; Kutaimarishwa huduma za zana za kilimo kabla na baada ya mauzo ikiwa ni pamoja na mafunzo, matengenezo na usambazaji wa zana na vipuri na pia itasaidia kuangalia mahitaji muhimu ya zana kwa Wakulima wadogo wa Kati na Wakubwa.

Mkutano huo muhimu wa Wadau wa Zana za Kilimo nchini ulianza jana katika Ukumbi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dar es Salaam na umefungwa leo.

No comments:

Post a Comment