Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na watendaji wa serikali sambamba na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoani Lindi katika ziara yake ya kikazi aliyoianza leo tarehe 4 Disemba 2018 mkoani humo.
Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Liwale Mhe Sarah Chiwamba, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mhe Rukia Muwango na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe Christopher Ngubiagai wakisikiliza kwa makini hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akizungumza kwenye kikao kazi na watendaji wa serikali sambamba na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoani Lindi katika ziara yake ya kikazi aliyoianza leo tarehe 4 Disemba 2018 mkoani humo.
Na Mathias Canal, Mtwara
WAZIRI wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amemuagiza Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe kumsimamisha kazi mtumishi George
Mboje na kumuondoa kwenye timu ya Operesheni Korosho.
Pamoja na kumundoa kwenye timu hiyo pia Katibu Mkuu ametakiwa
kumuondoa kwenye Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko.
"Katibu Mkuu, nataka umuondoe huyu George kwenye hii timu na
pia sitaki kumuona kwenye Bodi na Taasisi yoyote katika Wizara ya Kilimo"
Alisisitiza Mhe Hasunga
Mhe Hasunga ametoa agizo hilo leo tarehe 4 Disemba 2018 wakati
akizungumza kwenye kikao kazi cha Watendaji wa timu ya Oparesheni korosho kilichofanyika katika ukumbi wa CBT Mkoani Lindi na wakati wa kikao kazi na watendaji wa serikali sambamba na
Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoani Lindi katika ziara yake ya kikazi
aliyoianza leo tarehe 4 Disemba 2018.
George Mboja ambaye yupo kwenye timu ya Oparesheni Korosho
akiwakilisha Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko anatuhumiwa kwa Utovu wa
nidhamu sambamba na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo wakati wa
Oparesheni Korosho inayoendelea nchini.
Aidha, Waziri Hasunga amewahakikishia watendaji hao kuwa serikali
ina fedha za kutosha kuwalipa wakulima wa Korosho lakini lazima wakulima wote
wahakikiwe ili kujiridhisha kwamba anayelipwa ni mkulima wa mwisho na sio
wafanyabiashara maarufu kama Kangomba.
Akizungumzia hatua iliyofikiwa na serikali kuhusu malipo ya
wakulima wa korosho, alisema hadi kufikia Jana tarehe 3 Disemba 2018 uhakiki
ulikwishafanyika kwenye vyama 220 kati ya vyama 504 vilivyopo katika Mkoa wa
Mtwara, Lindi na Ruvuma na kati ya vyama 617 vinavyojihusisha na Korosho
nchini.
Alisema kati ya vyama hivyo vilivyokwisha hakikiwa ni vyama 181
ndivyo ambavyo tayari vimelipwa fedha zao huku Bilioni 41.8 zikiwa zimelipwa.
Aliongeza kuwa wakati zoezi hilo linaanza serikali ilikuwa inalipa
Bilioni Moja kwa siku lakini kwa sasa utaratibu uliowekwa ni kulipa kati ya
Bilioni 5 mpaka 10 kwa siku.
Katika taarifa yake Waziri Hasunga amesema kuwa jumla ya wakulima
40,208 wamekwishalipwa fedha zao.
Mhe Hasunga aliongeza kuwa serikali imeamua kuwalipa wabebaji na
wapakiaji wa mizigo kwenye maghala sambamba na kuanza kuwalipa malipo ya awali
wasafirishaji kutoka kwenye vyama vya msingi kwenda kwenye vyama vikuu.
Kuhusu swala la magunia Waziri Hasunga alisema kuwa serikali
imeamua kuyalipa magunia yote ili kurahisisha uhifadhi wa Korosho.
No comments:
Post a Comment