TAA YAENDELEA KUJITOLEA KWA JAMII - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 11 December 2018

TAA YAENDELEA KUJITOLEA KWA JAMII

Mkurugenzi wa Chief Promotions Bw. Amoni Mkoga akizungumza mbele ya waandishi wa habari kuhusu Tamasha la Utamaduni la Chato linalotarajia kufanyika Disemba 22, 2018. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa  Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Abdi Mkwizu (kulia) na Mwenyekiti Bodi ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bw. Habbi G;unze (kushoto). Mkutano huo wa waandishi wa habari umefanyika leo katika Kijiji cha Makumbusho.

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha shughuli mbalimbali za jamii, kwa kutoa misaada yenye tija. Hilo limekuwa bayana leo kwenye Kijiji cha Makumbusho Jijini Dar es Salaam, ambapo TAA imetoa msaada wa fulana 100 kwa ajili ya kufanikisha Tamasha la Utamaduni la Chato linalotarajiwa kufanyika tarehe 22 Disemba, 2018 katika Uwanja wa Mazaina Chato.

Akizungumza katika Mkutano wa waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa TAA, Bw. Abdi Mkwizu amesema Mamlaka ina wajibu mkubwa wa kuunga mkono shughuli za kijamii, kwa kutoa misaada ya mbalimbali.

“Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania ina wajibu wa Kusimamia, kuendesha, kuboresha na kuendeleza Viwanja vya Ndege Tanzania lakini pia mbali na kutoa huduma hizo tuna wajibu wa kushiriki katika shughuli za kijamii, kwa wadau ambao wanatufanya sisi tuwepo,” amesema Bw. Mkwizu.

Pia Bw. Mkwizu amebainisha kwamba TAA inahudumia Viwanja 58 vilivyopo Tanzania Bara chini ya serikali, hivyo ni wajibu wao kushiriki katika shughuli za kusaidia jamii sehemu yeyote ile kulingana na uhitaji na bajeti iliyopo.

“Ikumbukwe siku za hivi karibuni TAA tumeshirika katika kufanikisha Tamasha la Urithi Wetu lililofanyika kuanzia Oktoba Mosi mpaka Oktoba 7, 2018 katika Kijiji cha Makumbusho, tumetoa pia msaada wa Mafuta Kinga jua ya Ngozi kwa watoto wenye ulemavu wa Ngozi katika baadhi ya shule hapa Dar es Salaam, lakini pia tarehe 24 Novemba mwaka huu tumekabidhi Shule ya Msingi ya Kisasa huko Bukoba inaitwa Tumaini,  na tunaamini itaongeza ufaulu kwa wanafunzi huko Bukoba na hayo ni macheche kati ya mengi ambayo Mamlaka inafanya kwa Jamii” amebainisha Bw. Mkwizu.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu na niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) Bw. Habbi Gunze ameishukuru Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa mchango wake kufanikisha Tamasha la Utamaduni la Chato.

“Niwashukuru sana Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa mchango wao nap engine bila wao hili la leo lisingeweza kufanikiwa. Utamaduni ndio uhai wa Taifa, kwa hiyo nchi isipokua na Utamaduni nchi inakua sio hai, hivyo kwa Mchango huu wa kusaidia hili nawapongeza sana TAA” amesema Bw. Gunze.

Naye Mkurugenzi wa Chief Promotions ambaye ndie mratibu wa Tamasha hilo Bw. Amon Mkoga amesema kwamba Tamasha litakuwa na mambo yote ya kiutamaduni ili kuenzi asili ya Kitanzania.
“Kauli mbiu ya Tamasha la Utamaduni la Chato inasema “Maendeleo ya Viwanda yasiache Utamaduni nyuma” ambapo Tamasha hili ni maalum kwa ajili ya kuuenzi utamaduni wa Mtanzania.

Katika Tamasha hili kutakua na Vikundi mbalimbali vya Utamanduni. Vikundi vya ngoma vitakuwepo kutoka Simiyu, Shinyanga, Geita, Mwanza, Tabora na Chato wenyewe, hivyo tunawaomba wananchi mtusaidie kufikisha taarifa hizi kwa watanzania” ameeleza Bw. Mkoga.
Tamasha la Utamaduni la Chato ni tamasha kubwa la ngoma ambalo hufanyika kila mwaka nah ii itakua ni mara ya tatu mfululizo likifanyika Chato mkoani Geita.

No comments:

Post a Comment