CHUO CHA MIPANGO KUANZISHA KIWANDA CHA KUCHAKATA NGOZI, DODOMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 1 December 2018

CHUO CHA MIPANGO KUANZISHA KIWANDA CHA KUCHAKATA NGOZI, DODOMA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (kulia) akisikiliza maelezo ya namna  Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini inavyotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo vijijini yenye lengo la kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ikiwemo mazingira, wakati wa Mahafali ya 32 yaliyofanyika katika Kampasi ya Dodoma.


Mlau wa Mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Dkt. Christina Mandala, akiongoza maandamano wakati wa mahafali ya 32 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Kampasi ya Dodoma, ambapo wahitimu 2596 wametunukiwa vyeti na shahada mbalimbali. Kulia ni Kaimu Mkuu wa chuo hicho Prof. Hozen Mayaya na kushoto ni Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi chuoni hapo Bi. Mugabe  Mtani.

Na Benny Mwaipaja. WFM, Dodoma

CHUO Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, kimeanza ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Ngozi na Kuzalisha Bidhaa za Ngozi katika Kata ya Idifu, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma kitakacho gharimu zaidi ya shilingi milioni 500 kitakapo kamilika.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Hozen Mayaya wakati wa sherehe za mahafali ya 32 ya Chuo hicho Kampasi ya Dodoma, ambapo wahitimu 2,596 wametunukiwa vyeti na shahada mbalimbali.

"Kupitia mradi wa Eco Act, unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya, Chuo kimetekeleza falsafa ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, ya Ujenzi wa uchumi wa viwanda hiki ambacho kikikamilika kitakuwa na jumla ya wafanyakazi 70, kati ya hao 50 watakuwa wa kudumu na vibarua 20" alisisitiza Prof. Mayaya.

Aidha, Prof Mayaya ameeleza kuwa Chuo hicho kinatekeleza mradi mwingine wa kuhimili mabadiliko ya Tabia nchi kwa kuzijengea uwezo Halmashauri za wilaya ya  Longido, Ngorongoro na Monduli mkoani Arusha ambao umepunguza changamoto za ufugaji katika jamii za wafugaji kwa kujenga mabwawa matatu ya kunyweshea mifugo.

"Mradi huu ni wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Taasisi za kimataifa za mazingira na Maendeleo (IIED), Mfuko wa Umoja wa Mataifa na Maendeleo (UNCDF LoCAL), mashirika yasiyo ya kiserikali ya Haki Kazi Catalyst (HKC) na Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), aliongeza Dkt. Mayaya.

Kwa Upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Bi. Mugabe Mtani, amesema utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo ya wananchi umelenga kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano iliyojipambanua kuimarisha uchumi wa nchi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla

"Katika Kipindi chake cha miaka mitatu Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli, amerudisha nidhamu, uadilifu, uwajibikaji ndani ya utumishi wa umma, kuimarisha sekta ya kilimo, usafirishaji, miundombinu, na nishati" alisema Bi. Mtani

Alisema hatua hiyo ya uwajibikaji wa Serikali ya Awamu ya Tano ni mafanikio yaliyofufua matumaini ya wananchi wanyonge na masikini walio wengi hapa nchini ambao wameanza kunufaika na rasilimali zao.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, amekipongeza chuo hicho kwa kushiriki katika ujenzi wa viwanda hatua itakayochochea na kuiwezesha nchi kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilianzishwa miaka 39 iliyopita na kinatoa mafunzo ya ngazi ya astashahada, stashahada, shahada na shahada ya uzamili.

No comments:

Post a Comment