WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kati ya Julai na Oktoba, mwaka huu, Serikali imetoa jumla ya sh. bilioni 83.2 ili kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule nchini. Waziri Mkuu amesema, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 38.6 zilipelekwa kwenye shule za msingi na shilingi bilioni 44.6 zilienda kwenye shule za sekondari ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa elimumsingi bila malipo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Novemba 16, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Januari 29, 2019.
“Katika kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule nchini, Serikali inapeleka fedha za elimumsingi bila malipo moja kwa moja shuleni. Kwa mfano, katika kipindi cha Julai hadi Oktoba, 2018 shilingi bilioni 38.6 zilipelekwa katika shule za msingi na shilingi bilioni 44.6 kwenye shule za sekondari,” amesema.
Amesema tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango wa elimumsingi bila malipo, uandikishaji wa watoto wa darasa la awali na darasa la kwanza umeimarika na kwamba kumekuwepo na mwenendo mzuri wa ufaulu kwenye mitihani ya kumaliza darasa la saba.
“Kumekuwepo na mwenendo mzuri wa ufaulu katika mitihani ya kumaliza darasa la saba, ambapo mwaka 2016 ilikuwa wastani wa asilimia 70 na mwaka 2018 ilikuwa ni wastani wa asilimia 78. Hali hiyo, imeongeza mahitaji mbalimbali, ikiwemo miundombinu katika shule zetu za msingi na sekondari,” amesema.
Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu inaendelea na mikakati ya ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu muhimu ya shule.
“Kwa mfano, kupitia programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu (EP4R), shilingi bilioni 53.4 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari. Aidha, shilingi bilioni 9.2 zimeelekezwa katika uimarishaji wa miundombinu ya elimu kupitia programu ya kuboresha elimu ya shule za msingi (EQUIP-T),” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu na kuweka mazingira mazuri katika mfumo mzima wa elimu nchini kwa kushirikiana na wadau wote.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema taasisi zote zinazohusika na usimamizi na uendeshaji wa mitihani ya taifa hazina budi kuhakikisha zinasimamia kikamilifu mitihani hiyo ili kuepuka udanganyifu.
“Natambua kuwa mitihani ya taifa kwa darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne inaendelea. Hata hivyo, katika kipindi cha hivi karibuni kumezuka matukio ya kuvuja kwa mitihani.”
“Naziagiza taasisi zote zinazohusika na usimamizi na uendeshaji wa mitihani ya taifa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu mitihani hiyo ili kuepuka udanganyifu. Itakapobainika kuwepo kwa udanganyifu wa mitihani, hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria dhidi ya yeyote atakayehusika,” amesisitiza.
No comments:
Post a Comment