NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias John Kwandikwa amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi na ubunifu ili kuboresha huduma na kuongeza mapato.
Akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi hizo mjini Shinyanga, Mhe. Kwandikwa amesema Serikali itaendelea kuajiri watumishi wenye weledi na uzoefu wa kutosha katika Taasisi hizo hivyo kazi kubwa ni kuwapa ushirikiano na kufanyakazi kwa malengo yanayopimika.
“Tumejipanga kumaliza changamoto ya uhaba wa wafanya kazi hasa kwa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Wakala wa Majengo Nchini (TBA) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) hivyo ongezeni ubunifu ili kuwe na uwiano kati ya wafanya kazi na tija inayozalishwa katika Taasisi zenu,” amesema kwandikwa.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi, Mibara Ndirimbi amemhakikishia Mhe. Kwandikwa kuwa licha ya upungufu wa wafanya kazi barabara zote kuu na za mikoa zinapitika wakati wote wa mwaka. Amesema mkoa wa Shinyanga una KM zaidi ya elfu moja za barabara ambapo KM 277.41 ni barabara kuu na KM 727.18 ni barabara za mikoa.
Naye Kaimu Meneja wa TBA Shinyanga Mkadiriaji Majenzi Emmanuel Julias amesema ofisi yake inasimamia ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia nafaka vyenye uwezo wa kutunza tani zaidi ya elfu 20 hivyo kukamilika kwa mradi huo licha ya kuongeza mapato pia kutaongeza uzoefu kwa taasisi hiyo na hivyo kuomba wadau wengi mkoani humo kuitumia.
Naibu Waziri Kwandikwa amewataka TEMESA kujitangaza ili kupata kazi nyingi za ufundi wa magari, mitambo na umeme na hivyo kuongeza wateja na mapato.
Muonekano wa moja ya madaraja yaliyojengwa katika barabara ya Kolandoto-Mwangongo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga ili kudhibiti mafuriko yanayotokea mara kwa mara. |
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO, (NOVEMBA 28, 2018).
No comments:
Post a Comment