NAIBU WAZIRI JAPHET ASUNGA ATAKA UFUGAJI NYUKI WENYE TIJA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 5 October 2018

NAIBU WAZIRI JAPHET ASUNGA ATAKA UFUGAJI NYUKI WENYE TIJA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo (kushoto) akisoma taarifa ya ufugaji nyuki katika mkoa wake mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga.

Baadhi ya wananchi wakipunga mikono kwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya utundikaji  mizinga  iliyofanyika kitaifa mkoani Rukwa katika manzuki ya Nawima iliyoko katika Msitu wa Mto Kalambo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akisalimiana na mjumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa Mkoa wa Rukwa wakati alipowasili katika eneo la kutundika mizinga katika manzuki ya Nawima iliyoko katika Msitu wa Mto Kalambo  katika mkoa wa Rukwa.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga amewataka wafugaji nyuki nchini kuendesha ufugaji nyuki wenye tija kwa kuzalisha mazao mengi yenye ubora na kuyaongezea thamani kwa ajili ya kujiongezea kipato.

Pia amewataka wafugaji hao wakubalika kubadilika kwa kuanza kufuga nyuki kwa njia ya kisasa baadala ya kuendelea na uzalishaji mali wa kimazoea usio na tija. Ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya kutundika mizinga nchini Iliyofanyika kitaifa katika mkoa wa Rukwa wilayani Kalambo katika manzuki ya Nawima iliyoko katika Msitu wa Mto Kalambo.

Katika maadhimisho hayo jumla ya mizinga 100 imetundikwa katika Manzuki hiyo hata hivyo manzuki hiyo ina jumla ya mizinga 262 na itakuwa ikihudumiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Katika maadhimisho ya mwaka huu yana kauli mbiu isemayo" Tuwalinde na kuwatunza nyuki ili watunufaishe kwenye kilimo na uhifadhi" Mhe. Hasunga Ameongeza kuwa ufugaji nyuki ni fursa kwa vile mazao yake hutumika kama chakula na malighafi viwandani na jamii mbalimbali zinajua na kuamini kuwa katika asali kuna viambato vya dawa.

Katika hatua nyingine amewahimiza wananchi hao kulinda na kuhifadhi misitu kwa vile nyuki wanaishi katika mazingira ambayo hayajaharibiwa licha ya kuwa ufugaji nyuki ni nyenzo katika kulinda mazingira. Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amewataka wananchi kulinda na kuhifadhi misitu ili kuendelea kupata mazao ya nyuki.

 Wakati huo huo, Mkuu wa mkoa huyo ametaka wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa wale ambao walikuwa hawajaanza kufuga nyuki Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Allen Richard amesema wafugaji nyuki wanahitaji kuelimishwa kuhusu matumizi ya mizinga yenye ubora ili waweze kuachana na mizinga ya kiasili. Ameongeza kuwa Idara yake itahakikisha inafuatilia na kuona ni wafugaji wangapi wanaitumia mizinga ya kisasa kwa ajili ya kuwasaidia kwa kuwaelimisha kwanini watumie mizinga ya kisasa.

 Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo alisema TFS inashirikiana na Mfuko wa Misitu Tanzania (TAFF) katika kujenga viwanda vidogo vidogo na vikubwa katika maeneo mbalimbali ili kuweza kuwasaidia wafugaji nyuki katika kujiingizia kipato. Amesema viwanda hivyo vitasaidia katika kuchakata mazao ya nyuki na pia amesisitiza kuwa serikali inatumia takribani shilingi milioni 100 katika kuhakikisha inalinda ubora wa bidhaa zake za Nyuki.

Prof. Silayo amesema TFS inawapa wafugaji Nyuki fursa ya kujifunza mambo mapya ili kuboresha uzalishaji. Pia, Mtendaji Mkuu huyo amesema kuwa ujenzi wa viwanda hivyo umeanza katika mikoa ya Singida,Tabora pamoja Iringa huku Katavi upembuzi yakinifu unaendelea.

Amezitaja hatua wanazozichukua ili kukabiliana na changamoto kuwa ni kutoa elimu kwa wafugaji, kuboresha teknolojia ya urinaji na uchakataji, uzalishaji wa Malkia wa nyuki na ukamataji wa makundi ya nyuki kwenye mapito na kuyahamishia kwenye mizinga.

 Aidha, Prof. Silayo ameeleza kuwa Serikali iko mbioni kuanzisha maabara yenye viwango vya kimataifa itakayotumika kuhakikisha ubora wa mazao ya nyuki na imeashaanza kujengwa katika Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) jijini Arusha. TFS inasimamia jumla ya manzuki 154 kote nchini, Manzuki hizo zina jumla ya mizinga 11,012 na hutumika kama vituo vya mfano vya uzalishaji wa mazao ya nyuki.

No comments:

Post a Comment