Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe.
Mhandisi Isack Kamwelwe (kushoto), akisisitiza jambo kwa Mkandarasi anayejenga
barabara ya Chunya –Makongolosi KM 39 muda mfupi kabla ya kumuamuru aondoke
hapa nchini.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe.
Mhandisi Isack Kamwelwe akitoa maelekezo kwa viongozi wa wilaya ya Mufindi na TANROADS
mkoa wa Iringa namna ya kudhibiti mmomonyoko wa udongo katika kijiji cha
Litero-Nyololo wilayani Mufindi.
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe amewafukuza kazi na kuwataka kuondoka
nchini mara moja wafanyakazi wawili wa kampuni ya China New Railway 15 Bureau
Group Corporation inayojenga barabara ya
Chunya –Makongolosi KM 39 kwa kiwango cha lami kwa kukiuka mkataba na
kudhalilisha wafanyakazi.
Wafanyakazi
hao ni Meneja mradi Pen Pong na Meneja rasilimali watu Liun Migun ambao kwa
pamoja licha ya kukiuka vipengele vya mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo pia
wanatuhumiwa kuwapiga na kuwafukuza kazi wafanyakazi wakitanzania kwa uonevu.
Akizungumza
na wakazi wa kijiji cha Matundasi wilayani Chunya Mhandisi, Kamwelwe amesema
haiwezekani Serikali ikamvumilia mkandarasi asiyezingatia mkataba na anayedhalilisha
wananchi ambao ndio walipa kodi zinazotumika kumlipa na kuwaonya makandarasi
wote nchini kuzingatia mikataba na kutenda haki kwa wafanyakazi wao.
Waziri
Kamwelwe amesema barabara ya Chunya – Makongolosi KM 39, ambayo ujenzi wake ulitakiwa kuanza Oktoba 30
mwaka 2017 na kukamilika Januari 2020 hadi sasa imejengwa kwa asilimia 13
badala ya 20 zilizokubaliwa katika mkataba.
Aidha
amesema mkandarasi China New Railway 15 Bureau Group Corporation amekiuka
mkataba kwani alitakiwa awe na mitambo75 kwaajili ya ujenzi na hadi sasa ni
mitambo 34 tu inayofanyakazi, awe na wataalam saba na hadi sasa ni wataalam
watatu tu wanaofanyakazi licha ya kulipwa asilimia 15 ya malipo ya awali.
“Natoa miwezi
mitatu kwa kampuni hii kujirekebisha na kuzingatia mkataba kabla hatua nyingine
za kisheria hazijachukuliwa,” amesema Waziri Kamwelwe.
Katika
hatua nyingine Waziri Kamwelwe ametoa mwezi mmoja kwa mkandarasi China Civil
Engineering Corporation (CCECC), anayejenga barabara ya Mafinga –Nyigo KM 74.1 na
Nyigo –Igawa KM 63.8 kukamilisha ujenzi huo kwa mujibu wa mkataba.
Naye Meneja
wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Iringa Mhandisi Daniel Kindole amemhakikishia Waziri
Kamwele kuwa ujenzi huo uko katika hatua za mwisho na utakamilika kwa wakati.
Barabara
ya Mafinga –Nyigo –Igawa yenye urefu wa kilometa 137.9 ni sehemu ya barabara
kuu ya TANZAM ambapo katika mkoa wa Iringa ina KM 74, Njombe KM 52 na Mbeya KM
12.
Waziri
Mhandisi Kamwelwe yuko katika ziara ya kukagua miundombinu ya ujenzi, uchukuzi
na mawasiliano katika mikoa ya nyanda za juu kusini.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO,
(OKTOBA 5, 2018).
No comments:
Post a Comment