BENKI ya NMB imetoa msaada wa mahema maalum pamoja na fulana zitakazotumiwa na Taasisi ya Suleman Kova Security and Disaster Management Foundation-Sukos-DMF wakati inazunguka kwa jamii kutoa elimu namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali pindi yanapotekea. Vifaa hivyo ambavyo ni mahema maalum nane pamoja na fulana zitakuwa zikitumiwa siku ya tarehe 6 Octoba ikiwa ni siku maalumu kabisa ya kuadhimisha siku ya maafa /majanga duniani.
Akizungumza katika tukio hilo la kukabidhi msaada huo, Meneja Mradi, Uwajibikaji kwa Jamii wa Benki ya NMB, Lilian Kisamba alisema tukio hilo ni mwendelezo wa benki hiyo katika kuisaidia jamii hivyo wanatambua na kuguswa na majanga na maafa yanayowakumba wananchi ambao ni jamii wanaoihudumia.
"Ni ada yetu NMB kuisaidia jamii inayotuzunguka kupitia kitengo maalumu cha CSR...tumekuwa tukifanya hivi maeneo mbalimbali..hususani sekta ya elimu, afya na huduma nyingine muhimu kwa jamii. NMB inaamini msaada huu utatasidia jamii kupatiwa elimu ya kujikinga na majanga unaweza kupunguza athari ya majanga hayo hata yanapotokea," alisema Bi. Lilian Kisamba alipokuwa akikabidhi msaada huo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Sukos-DMF, Suleiman Kova.
Alisema NMB itaendelea kuisaidia jamii katika maeneo mbalimbali kwa kuwa hakuna maendeleo ya kiuchumi pasipo na jamii salama na pia hakuna biashara inayoweza kufanya vema pasipo na jamii salama.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Sukos-DMF, Suleiman Kova (Kamanda mstaafu wa Jeshi la Polisi) alisema taasisi yake ya Sukos-DMF kwa kushirikiana na Benki ya NMB na wadau wengine imepanga kufanya uzinduzi wa mahema maalum ambayo yatakuwa yakitumika katika shughuli za kutoa hifadhi kwa wahanga wakati yanapotokea maafa.
Alisema zoezi hilo litakwenda sambamba na washiriki kufanya mazoezi (jogging) kuanzia eneo la uwanja wa taifa kuelekea viwanja vya Kituo cha Vijana cha Jakaya Kikwete na pia kutakuwa na tukio la washiriki kuchangia damu kwa ajili ya wahitaji, huku akisisitiza elimu ya kukabiliana na majanga kwa taasisi hiyo utakuwa ni mradi endelevu.
"Tunapenda kuwajulisha wananchi pamoja na wadau mbalimbali wajitokeze kwa wingi Oktoba 6, 2018 katika Viwanja vya Jakaya M. Kikwete kituo cha vijana vilivyopo Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam. Siku hiyo kutakuwa na maadhimisho maalum ya taasisi ya Sukos ambapo tutazindua mahema maalum yenye lengo la kutoa hifadhi kwa wahanga wakati wa maafa," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Sukos-DMF, Suleiman Kova.
Taasisi ya Suleman Kova Security inayosaidia kutoa elimu kwa umma kujikinga na majanga (Suleman Kova Security and Disaster Management Foundation-Sukos-DMF). Taasisi hiyo inajihusisha na usimamizi, utoaji elimu na uhamasishaji jamii kuhusiana na namna ya kukabiliana na maafa mbalimbali ikiwa ni kuunga mkono Serikali harakati za kutoa elimu kwa jamii kuyakabili majanga anuai.
Wadau wengine watakaoungana na Sukos-DMF katika maadhimisho yao ni pamoja na Mpango wa Taifa wa Damu salama, Kampuni ya Coka cola, Kampuni ya Cops Security Ltd na vyombo vya habari kuhamasisha jamii.
Msanii wa uigizaji, Salim Ahmad 'Gabo' ambaye ni Balozi wa Taasisi ya Suleman Kova Security and Disaster Management Foundation, Sukos-DMF akizungumza na wanahabari. Kutoka kushoto ni Afisa Mahusiano Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Raya Hamad, Meneja Mwajiri wa Cops Security (T) Ltd, Ibraahim Mcherecheta, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Suleman Kova Security and Disaster Management Foundation, Sukos-DMF, Bw. Suleiman Kova na Meneja Mradi, Uwajibikaji kwa Jamii wa Benki ya NMB, Lilian Kisamba. |
No comments:
Post a Comment