Na Joachim Mushi, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Simu za mkononi nchini Vodacom Tanzania leo imesaini mkataba wa kibiashara na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) wa kutumia Huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) utakaowezesha mkongo kusambaza huduma za mawasiliano maeneo ya vijijini.
Hafla ya makubaliano hayo ya kibiashara imefanyika leo jijini Dar es Salaam, ambapo TTCL Corporation imewakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Ndugu Waziri Kindamba na Vodacom ikiwakilishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Hisham Hendi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kindamba alisema Vodacom amekuwa mteja wa Mkongo wa Taifa tangu Mei Mosi, 2013 na hadi sasa anatumia huduma za ukubwa wa STM-4 (Jumla 7) na STM-16 (Jumla 9), huku akiongeza kuwa Mkataba mpya uliosainiwa unaongeza viwango vya matumizi ya Mkongo kwa Vodacom kwa STM-16 (Jumla 2) na STM-64 (Jumla 1) wenye thamani ya Shilingi bilioni 25.6 bila VAT.
“..Mkataba wa leo unatufanya sisi NICTBB na TTCL kutambua uzito wa majukumu tuliyokabidhiwa na Serikali ya kuhakikisha kuwa huduma za Mkongo zinaimarishwa ili watoa huduma za Mawasiliano hapa nchini waboreshe huduma zao na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema.
“Mkataba wa leo unatufanya sisi NICTBB na TTCL kutambua uzito wa majukumu tuliyokabidhiwa na Serikali ya kuhakikisha kuwa huduma za Mkongo zinaimarishwa ili watoa huduma za Mawasiliano hapa nchini waboreshe huduma zao na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” aliongeza Kindamba.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Ndugu Hisham Hendi akizungumza katika hafla hiyo alisema unalenga kuboresha huduma za mawasiliano za sauti na data kanda ya ziwa kati kaskazini na mikoa ya kusini ya Tanzania kwa kuwezesha kuleta maendeleo kupitia huduma teknolojia ya mawasiliano.
Alisema Vodacom inatumia mkongo kwa takribani zaidi ya miaka 5 na kwa mwaka huu Vodacom inakodisha mkongo huo ambao miundombinu yake imesambaa kwa urefu wa kilomita zipatazo 7,560 nchini kote kwa kipindi cha miaka 10 kwa thamani ya dola za Kimarekani USD11.2 milioni bila VAT.
“miundombinu ya mkongo wa taifa wa mawasiliano imesambaa katika eneo kubwa kwa urefu na unao uwezo mkubwa wa kuwezesha kurusha mawasiliano ya data kwa ufanisi mkubwa, teknolojia hii itawezesha wateja wa Vodacom kupata mawasiliano mazuri zaidi nchini kote,” alisisitiza Ndugu Hisham Hendi.
Hadi sasa wateja wanaohudumiwa na mkongo wa Taifa wa mawasiliano ni pamoja na kampuni ya TTCL, Vodacom, Tigo, Viettel, Airtel, Simbanet, Zantel, Raha, Smile, Sasakwa, eGA na ISP wengine yanatumia Mkongo wa Taifa kufikisha huduma zao kwa wateja. Mkongo wa Taifa hutumiwa pia na nchi za Afrika Mashariki na eneo la Maziwa makuu yaani Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi na Zambia na hivyo kuufanya Mkongo huu kuwa na umuhimu wa kipekee kwa mawasiliano.
No comments:
Post a Comment