AKINA MAMA WATAKIWA KUOSHA MATITI KABLA YA KUNYONYESHA...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 19 February 2025

AKINA MAMA WATAKIWA KUOSHA MATITI KABLA YA KUNYONYESHA...!

Jackline Saulo, Afisa kutoka timu ya Uelimishaji na Uhamasishaji Ofisi ya Mganga Mkuu Mkoa wa Kagera Jacline Saulo.

IMG-20250217-WA0560 (1).jpg
Wanawake kutoka vikundi mbalimbali vya kusaidiana masuala ya kiuchumi na kijamii wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kupata mafunzo kuhusu ugonjwa wa Marburg.

Na Elimu ya Afya kwa Umma

KATIKA mwendelezo wa Jitihada za Serikali za kutoa Elimu ya Afya kuhusu Ugonjwa wa Marburg, jumla ya vikundi 10 vikiwa na akina mama 78 wamepatiwa elimu ya Afya kuhusu ugonjwa wa Marburg Wilayani Biharamulo huku wito ukitolewa kwa akina mama kujenga mazoea ya kuosha matiti kabla ya kumnyonyesha mtoto.

Mafunzo hayo yameratibiwa na Wizara ya Afya, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani(UNICEF) TIP ambao ni Mtandao wa Dini mbalimbali na Washirika wa Mtandao huo ambao ni BAKWATA, TEC,CCT, na Ofisi ya Mufti Zanzibar huku wadau wengine kama vile Afrika CDC wakishiriki katika Mafunzo hayo.

Akitoa Mafunzo hayo, Afisa kutoka timu ya Uelimishaji na Uhamasishaji Ofisi ya Mganga Mkuu Mkoa wa Kagera Jacline Saulo ametoa wito kwa akina mama kujenga mazoea ya  usafi wa mwili ikiwemo kuosha matiti kabla ya kunyonyesha mtoto.

“Kinga ni bora kila tiba, akina mama ni muhimu sana kuzingatia usafi na kabla ya kunyonyesha watoto tuoshe matiti yetu, unakuta sisi akina mama tumeshinda shambani kulima hujanawa ,unaanza kumnyonyesha mtoto tuepuke kufanya hivyo tuoshe kwanza matiti yetu ili kuwalinda watoto wetu”amesema.

Aidha, Saulo amekumbushia umuhimu wa unawaji mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni katika kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Marburg.

“Tukumbuke kunawa mikono mara kwa mara, na tunaponawa mikono tukumbuke kupitisha viganja vya mikono kwa kupishana ili kuweza kutoa uchafu unaoweza kukwama kwenye viganja vyetu vya mikono na pia ni muhimu tuepuke kusalimiana kwa kukumbatiana ”amesisitiza.

Kwa upande wake Regnihadah Mpete kutoka UNICEF amekumbushia umuhimu wa kuzingatia usafi katika kujikinga na magonjwa mbalimbali ya mlipuko kwa kuhakikisha maji ya kunywa yanachemshwa , kunawa mikono wakati wa kuandaa chakula, kabla ya kula au kabla ya kumlisha mtoto na chakula kiliwe kikiwa cha moto.

Japhet Kanoni ni Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Timu ya Msaada wa Kisaikolojia (MHPSS) amehimiza wazazi kuwa waangalifu namna ya utoaji wa adhabu kwa watoto nyakati za majanga na kusisitiza kuwa si kila adhabu inasadia kumbadilisha mtu huku akigusia kuacha tabia ya kuwanyanyapaa wahisiwa wa ugonjwa wa Marburg.

Wakizungumza mara baada ya kupata mafunzo hayo, baadhi ya akina mama hao wamesema watakuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Marburg katika familia na jamii zinazowazunguka.

No comments:

Post a Comment