Na Eva Ngowi, Kilimanjaro
SERIKALI imewaasa Wastaafu na Wastaafu watarajiwa kuanza kuwekeza kidogo kidogo kabla ya kustaafu kupitia Mifuko ya Uwekezaji wa pamoja ikiwemo UTT AMIS.
Hayo yameelezwa na Afisa Mwandamizi Masoko na Mawasiliano kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga wakati wa semina za Elimu ya Fedha zinazoendelea katika Kata za Ngarenairobi na Karansi, Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro.
Bw. Mwanga alisema Kupitia Mifuko ya Uwekezaji wa pamoja inayoendeshwa na UTT AMIS wawekezaji wanaweza kununua vipande na kuwekeza katika mifuko hiyo ili kukidhi mahitaji yao ya kiuwekezaji na waweze kufikia malengo yao.
“Tungependa kutoa msisitizo zaidi wa kutumia Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja ili kutimiza malengo ya kabla na baada ya kustaafu; kwa mfano, moja ya changamoto kubwa ambayo inawakabili watumishi baada ya utumishi wao na kustaafu ni kuwa na uhakika wa kipato ambacho kitawawezesha kukidhi mahitaji yao ya kila siku. Pamoja na kuwa na mifumo bora ya pensheni na kadhalika bado gharama za maisha ni za juu sana, hivyo inashauriwa kuanza mapema kufikiria na kuanza kuwekeza kidogo kidogo kabla ya kustaafu kupitia mifuko ya Uwekezaji wa pamoja.” Alisema Bw. Mwanga.
Aidha, aliwataka wastaafu na wastaafu watarajiwa kuwa makini na matapeli, kuacha kuanzisha biashara wasizokuwa na uzoefu nazo pamoja na kuepuka washauri wasiokuwa na nia nzuri ambao wanataka kujinufaisha wao wenyewe.
Bw. Mwanga alisema kuwa, kumekuwa na wimbi la matapeli wanaotoa ushauri usiofaa kwa wastaafu na pia kwa wale walioko kwenye mifuko ya kijamii wamekuwa wakitapeliwa kwa kupigiwa simu huku wakiwashawishi kuwekeza fedha kwenye sehemu zisizo rasmi na kuwahadaa kwa ahadi za faida kubwa ndani ya muda mfupi.
“Kumekuwa na wimbi la matapeli wanaotoa ushauri usiofaa kwa wastaafu kwa kuwa wanafahamu sasa wamepata hela nyingi za kiinua mgongo, kwa hiyo kila mmoja anakwenda kumshauri lakini ushauri ule unakuwa kwa ajili ya kuwanufaisha wao wenyewe. Hivyo tunatoa rai kwa wastaafu wawe makini sana na ushauri wanaopewa na hawa watu ili wasiingie kwenye hii kadhia ya kutapeliwa na endapo itatokea ukapigiwa simu ya kudai chochote ili upate mafao yako kwa wakati au kwa haraka tafadhali toa taarifa kwa Mfuko wowote wa Hifadhi ya Jamii uliopo ili suala hilo lifuatiliwe na kuchukuliwa sheria”. Alisema Bw. Mwanga.
Aidha, Bw.Mwanga, aliwashauri wastaafu na wastaafu watarajiwa kuwa wanapaswa kujiandaa kustaafu pindi wanapopata ajira au siku ya kuanza kupata kipato kwa kuwa na tabia ya kujiwekea akiba na kuwekeza kwenye shughuli za kiuchumi na kutumia fursa za masoko ya mitaji kama Hisa, Hatifungani na Mifuko ya Uwekezaji wa pamoja.
Serikali inaendelea kutoa Elimu kwa Umma, ikiwa na lengo la kuwafikia Watanzania wote na kuwajengea uwezo wa uelewa kuhusu masuala ya fedha, kuweka akiba, uwekezaji, usimamizi wa fedha binafsi, kujipanga kuhusu Maisha ya kustaafu pamoja na masuala ya usimamizi wa sheria na kanuni za huduma ndogo za fedha.
No comments:
Post a Comment