MAMLAKA ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwelekeo wa msimu wa mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2018, huku ikiendelea kutoa tahadhali kwa uwezekano wa mikoa kadhaa kupata mvua kubwa hadi juu ya wastani.
Mikoa iliyotabiriwa kupata mvua nyingi ni pamoja na maeneo ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba.
Taarifa hiyo inaainisha upo uwezekano wa mikoa hiyo kukumbwa na mvua za juu ya wastani hususani Mwezi wa Novemba, 2018 kutokana na uwezekano wa kutokea vimbunga katika eneo la Kusini magharibi mwa bahari ya Hindi.
Septemba 6, 2018, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi alitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli ulioanza mapema mwezi Septemba na pia mwanzoni mwa Oktoba, 2018 katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes L. Kijazi alisema mifumo ya hali ya hewa inaonesha uwezekano mkubwa wa mvua za vuli kuwa za wastani na juu ya wastani katika maeneo mengi ya nchi.
Alisema kuwa mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya pwani ya kaskazini katika kipindi cha msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba, 2018, huku akisisitiza wadau sekta mbalimbali kujipanga katika kutekeleza ushauri na tahadhari zinazotolewa na TMA kuepuka madhara makubwa endapo itatokea.
No comments:
Post a Comment