BALOZI MONGELLA AMTABIRIA MAKUBWA DC JOKATE MWEGELO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 27 September 2018

BALOZI MONGELLA AMTABIRIA MAKUBWA DC JOKATE MWEGELO

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akiwa na Balozi Getrude Mongella alipokuwa akiweka jiwe la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata zao la muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe.


NA DANIEL MBEGA, KISARAWE

SPIKA wa zamani wa Bunge la Afrika, Balozi Getrude Ibengwe Mongella, amemtabiria mambo makubwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akisema kwamba anaamini atafika mbali katika uongozi wa nchi hii. Balozi Mongella, ambaye alipata umaarufu kimataifa alipoongoza Mkutano wa Wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995 akiwa mwenyekiti, alisema mkuu huyo wa wilaya atafika mbali katika uongozi na kinachotakiwa ni kuendelea kuchapa kazi bila kusikiliza kelele za pembeni, kwani hata yeye alikumbana na vikwazo vingi.

“Nilifurahi sana ulipoteuliwa, nami nilianza harakati za siasa nikiwa binti mdogo kama wewe, nikakumbana na vikwazo vingi sana, lakini sikugeuka nyuma, kushoto wala kulia, ndiyo maana niliweza kufika mbali.

“Hata wewe unayo nafasi kubwa ya kufika mbali, unaweza kuwa rais wetu katika siku za mbele kwa sababu naamini wanawake tunaweza,” alisema Balozi Mongella wakati wa uzinduzi wa kiwanda kidogo cha kuchakata muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe hivi karibuni, ambapo DC Mwegelo alikuwa mgeni rasmi.

Mama Mongella alipongeza jitihada zilizoanzishwa na DC Mwegelo wilayani Kisarawe za kuhakikisha kwamba hakuna ‘sufuri’ katika elimu, huku akisema kwamba elimu ndio msingi mkubwa unaoweza kulikomboa taifa.

“Unafanya kazi nzuri sana, nimekuona mwenyewe siku moja unakimbia huku umevaa kombati, nilifarijika sana kwa sababu hata mimi nilianza nikiwa binti kama wewe, nakuombea uendelee na kasi hiyo hiyo ya kuwaletea  watu maendeleo na ndiyo itakayoonyesha ufanisi wa utendaji kazi wako,” alisema Mama Mongella.

Kwa upande wake, DC Mwegelo alisema anashukuru kupata nasaha kutoka kwa Balozi Mongella, ambaye kwake amekuwa mwanamke wa mfano katika uongozi kutokana na utendaji wake katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

“Nimefarijika mno kukutana na Mama Mongella ambaye kwangu amekuwa ‘role model’, binafsi ninatamani sana walau kufikia hata nusu ya mafanikio uliyofikia, ingawa ni kazi ngumu,” alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alitumia nafasi hiyo kujitambulisha katika Kijiji cha Kitanga, ambapo aliwataka wananchi kubuni na kushiriki shughuli za maendeleo kwa kuzingatia kwamba Serikali, chini ya Rais Dkt. John Magufuli, imedhamiria kwa dhati kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Alisema kwamba, wilaya hiyo ina ardhi kubwa yenye rutuba na kuwahamasisha wananchi kushiriki kilimo ili kuzalisha malighafi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda ili kwenda na falsafa ya Serikali ya kuifanya Tanzania ya Viwanda.

“Nawaombeni tushirikiane katika maendeleo, tushiriki kilimo hasa cha mihogo na korosho na Serikali inaendelea kuandaa mazingira bora zaidi kuboresha kilimo pamoja na kuwatafutia masoko,” alisema.

Siku hiyo mkuu huyo wa wilaya, akimwakilisha Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo, ambaye ni Mbunge wa Kisarawe, aliweka jiwe la msingi la kiwanda kidogo kinachomilikiwa na akinamama wakiongozwa na Abia Magembe, ofisa kilimo mstaafu ambaye amejikita katika kilimo cha muhogo pamoja na kuchakata na kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Kiwanda hicho, ambacho ni sehemu ya Mradi wa Green Voices unaofadhiliwa na taasisi ya Women for Africa Foundation inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Thereza de la Vega, kinachakata muhogo ili kupata unga ambao unatumika kuzalisha bidhaa mbalimbali. DC Mwegelo aliwapongeza akinamama hao na kuahidi kwamba, Serikali itakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha wanasonga mbele katika kujiletea maendeleo.
“Nawapongeza sana akinamama, pamoja na kiongozi wenu Mama Magembe, hakika hizi ni jitihada zinazotakiwa kuungwa mkono na serikali yangu itafanya kila njia kuona kwamba mnasimama,” alisema.

Aidha, aliwapongeza wafadhili wa Mradi wa Green Voices waliotoa mafunzo kwa akinamama 15 huko Hispania, ambapo akinamama 10 kati yao, akiwemo Mama Magembe, walianzisha miradi ya aina hiyo baada ya kurejea nchini huku wakiwafundisha akinamama wengine.

Miradi mingine ni utengenezaji wa majiko banifu, ufugaji wa nyuki, kilimo cha uyoga, kilimo nyumba (green house) cha mboga mboga, ukaushaji wa matunda na mbogamboga kwa kutumia umeme-jua, kilimo cha matunda, kilimo cha viazi lishe pamoja na utengenezaji wa majiko ya umeme-jua.

Miradi hiyo iko katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Morogoro, Kigoma na Mwanza.

Balozi Getrude Mongella ni Mjumbe wa Bosi ya taasisi ya Women for Africa Foundation.

No comments:

Post a Comment