Ofisa Elimu, Vifaa na Takwimu Wilaya ya Ilala
kwa niaba ya Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Asha Mapunda, akikata utepe kupokea
chumba cha darasa kilichokarabatiwa na wahitimu wa shule hiyo mwaka 2000.
|
Keki maalum ikikatwa katika hafla hiyo. |
WANAFUNZI waliowahi kusoma Shule ya Msingi Boma Wilaya ya Ilala,
jijini Dar es Salaam, ambayo sasa inaitwa Shule ya Msingi Mkoani,
wamekarabati darasa moja kwa lengo la kurudisha fadhila walizozipata wakiwa
wanasoma hapo kwa kuwa ndiyo umekuwa msingi bora wa mafanikio ya wanafunzi
wengi waliosoma katika shule hiyo.
Akizungumza
wakati wa hafla ya hiyo, mgeni rasmi ambaye alikuwa Ofisa
Elimu, Vifaa na Takwimu Wilaya ya Ilala, kwa niaba ya Mkurugenzi wa
wilaya hiyo, Asha Mapunda, aliwapongeza wanafunzi hao kwa umoja wao na fadhila
kwa kukumbuka shule waliyosoma akisema serikali haiwezi kufanya kila
jambo, hivyo wadau mbalimbali ni msingi katika kuhakikisha maendeleo ya
shule yanasonga mbele.
Kwa upande wake, mhitimu wa mwaka 2000 ambaye ndiye Mratibu
Group la WhatsApp, Hawa Barongo, amesema kuwa lengo ni kurudisha fadhila
kwa walimu wao na hata kwa jamii kwa ujumla huku akisema hawatachoka
kuhakikisha kila wakati wanatafuta pesa za kusaidia kukarabati shule hiyo
kutokana na miundombinu ya zamani kuwa si rafiki kwa wanafunzi.
"Maendeleo niliyopata mimi ni kutokana na kupata elimu
katika shule ya Ilala Boma hivyo lazima tuikumbuke kwa kuendelea kuipatia
msaada kadiri tunavyoweza maana ukituangalia hapa unatuona wote tuna vipato
vizuri hivyo ni budi kukumbuka wapi tumetoka na tulikotoka kupoje, hivyo
tutaithimini hii shule kila wakati kama tulivyofanya hivi sasa," alisema
Hawa na kuongeza kuwa:
“Leo tumerudi katika shule hii inayoitwa hivi sasa Shule ya
Msingi Mkoani kuja kusaidia kutatua changamoto ambazo zipo katika shule hii ukizingatia
kuwa shule hii ina uchakavu wa majengo na miundombinu, hivyo sisi
tumeanza kwa kukarabati darasa hili ambalo lilikuwa halina sakafu na
tumepaka rangi ndani ya darasa hili lakini changamoto bado zipo nyingi hivyo
hatutachoka kusaidia shule yetu hii, tutaendelea."
Hawa
amewataka wanafunzi mbalimbali waliosoma katika shule hiyo kurudisha upendo
katika shule hiyo kwa kuwa ndiyo chanzo cha mafanikio yao ya sasa.
Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo, Jane Mganwa, amewapongeza wanafunzi hao kwa
moyo wao wa upendo wa kujitoa kwa ajili ya wadogo zao ili waweze kusomea kwenye
madarasa yaliyo bora.
No comments:
Post a Comment