Na Joachim Mushi, Dar
MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Profesa Abel Makubi ameweka bayana mafanikio makubwa ya hospitali hiyo ndani ya kipindi cha miaka 10 ya utendaji, huku ikijivunia kuwa msaada mkubwa kwa matibabu ya ubingwa bobezi wa upandikizaji wa uloto kwa watoto na upandikizaji wa figo kwa wananchi wenye uhitaji.
Profesa Makubdi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na wahariri, Tanzania Bloggers Network (TBN) pamoja na Jumuiya ya Miitandao Tanzania (JUMIKITA), akielezea mafanikio yaliyochangiwa na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu na vifaa takribani ya shilingi bilioni 283, kuhudumia wananchi huduma za kibingwa bobezi.
Alisema Mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, hapo Julai 15, 2026 ambapo safari ya maadhimisho haya ilizinduliwa rasmi mwezi Oktoba mwaka 2025, na hospitali hiyo inahitaji kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 7 ndani ya kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya ubingwa bobezi ya upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu pamoja na upandikizaji wa figo kwa wananchi wenye uhitaji mkubwa wa huduma hiyo. Amebainisha kuwa kwa sasa kuna kuna idadi ya watoto 50 wanaohitaji upondikizaji wa uloto na wengine 50 kwa ajili ya upandfikizaji wa figo,
Aidha ameweka wazi kuwa tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo Oktoba 13,2015, imekuwa na dhamira ya kutoa huduma za kibingwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika kuzuia, kuchunguza, na kutibu magonjwa mbalimbali, pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na kufanya tafiti. BMH kwa inahudumia takribani wananchi milioni 10 kutoka mikoa nane ya Tanzania, huku ikiwa na vitanda 400 na watumishi 1,073, wakiwemo madaktari bingwa na bingwa bobezi zaidi ya 100.
Profesa Makubi anaeleza BMH inatoa huduma 20 za kibingwa na huduma 18 za ubingwa bobezi zikiwemo upandikizaji wa viungo, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uchunguzi wa mishipa ya moyo, huduma za radiolojia ya kisasa, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, ubadilishaji wa nyonga na magoti, upasuaji wa njia ya matundu madogo, pamoja na uchujaji wa damu.
"...Ndani ya miaka 10 ya utendaji, hospitali imepata mafanikio makubwa yaliyochangiwa na uwekezaji wa serikali katika miundombinu na vifaa vya kiasi cha shilingi bilioni 283, huku idadi ya watumishi ikiongezeka kutoka 20 tu mwaka 2015 hadi kufikia 1,076 mwaka 2026. Tumefanikiwa kupanua na kuboresha huduma za matibabu ya kibobezi, ikiwemo uanzishwaji wa huduma muhimu za upandikizaji figo na uloto kwa watoto wenye selimundu, pamoja na kukuza tiba utalii kwa kuhudumia wagonjwa wa kigeni na viongozi mashuhuri, wakiwemo wagonjwa 2,897 kutoka Burundi, 526 kutoka Comoro, na wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Anaeleza kuwa ubora wa huduma umeongezeka kupitia upasuaji wa matundu na uanzishwaji wa Kliniki ya Kifalme (Royal Clinic) mnamo tarehe 10 Julai 2025, ambayo imeshalaza na kuhudumia wagonjwa 18,607, wakiwemo wagonjwa wa kimataifa 390 waliofanyiwa uchunguzi mkubwa wa afya (Master Health Check-up). BMH imefanikiwa kupata ithibati ya kimataifa ya maabara ya ISO 15189:2022, huku ikiboresha mifumo yake ya TEHAMA.
"Tumeweka mfumo wa kisasa wa kuelekeza wagonjwa (queuing system) na kutoa maoni, na imefanikiwa kupunguza muda wa mgonjwa kusubiri huduma kutoka wastani wa saa 8 hadi saa 3 tu. Tunatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya na hasa ndani ya BMH, na ninatoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kuokoa maisha ya wagonjwa huku sisi tukiahidi kuendelea kuishi kwa kauli mbiu yetu ya kuvaa viatu vya mgonjwa, uwajibikaji, na kujituma, " amesisitiza Profesa Makubi katika mkutano wake.
Katika kuimarisha miradi ya kimkakati, hospitali inaendelea na ujenzi wa jengo la matibabu ya saratani lenye thamani ya shilingi bilioni 32, jengo la matibabu ya figo la shilingi bilioni 44.9 linalojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Japani iliyochangia bilioni 28 na Serikali ya Tanzania iliyochangia bilioni 16.9, uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri cha upandikizaji uloto, pamoja na chuo kinachotoa elimu ya ngazi ya Stashahada.
Profesa Makubdi alisema taasisi hiyo kwa miaka 10 ijayo inajipanga kubobea zaidi na kuwa kijiji cha utalii wa matibabu katika Makao Makuu ya nchi, Dodoma.
Kuelekea kilele cha tarehe 15 Julai 2026, matukio mbalimbali yamepangwa kufanyika ikiwemo harambee ya kusaidia mfuko wa matibabu ya upandikizaji uloto na figo, zoezi hili la harambee kusaidia mfuko wa matibabu ya upandikizaji uloto na figo linafanyika kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa lengo la kuwasaidia Watanzania wasio na uwezo.
Harambee hiyo kubwa itakayofanyika tarehe 15 Julai 2026 jijini Dodoma, inatarajiwa kuongozwa na Mgeni Rasmi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Profesa makubdi ameyaomba Mashirika, taasisi, makampuni, wadau, na wananchi wote kuchangia kupitia njia rasmi zilizowekwa ambazo ni namba ya malipo (Control Number) 986930000001 au kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa akaunti namba 102501000407 zote zikiwa kwa jina la BMH Organ Transplant.

No comments:
Post a Comment