MDUNDO jukwaa kinara barani Afrika la usambazaji wa muziki, linaendelea kubadilisha tasnia ya muziki kwa kuwawezesha wasanii kusambaza, kutangaza na kupata kipato kupitia kazi zao. Kwa idadi ya watumiaji inayozidi milioni 38.7 kwa mwezi na shughuli katika nchi mbalimbali za Afrika, Mdundo linaendelea kuwa mstari wa mbele katika mapinduzi ya kidijitali ya muziki barani Afrika.
Mwezi Januari 2025, Mdundo lilianza msimu
wake wa malipo ya mirabaha ya kila nusu mwaka, ambayo yanaendelea kwa sasa, na
yananufaisha zaidi ya wamiliki wa haki zaidi ya 100,000 barani kote, wakiwemo
maelfu ya wasanii wa Kitanzania. Tangu kuanzishwa kwake, jukwaa hili limewalipa
wasanii zaidi ya 200,000, huku idadi ya wanufaika ikiongezeka kila msimu wa
malipo. Hii ni hatua kubwa inayoonyesha dhamira ya Mdundo ya kujenga ekosistemi
endelevu ya muziki kwa wasanii wa Kiafrika hasa wasanii wa Kitanzania.
Moja ya nguzo muhimu za mafanikio haya
nchini Tanzania imekuwa ushirikiano madhubuti kati ya Mdundo na Vodacom
Tanzania PLC, kampuni inayoongoza ya mawasiliano nchini. Kupitia ushirikiano wa
kifurushi cha usajili na ubunifu wa bidhaa, Mdundo imewezesha upatikanaji
rahisi wa muziki kwa mamilioni ya Watanzania. Hatua hii imepanua hadhira kwa
wasanii, kuongeza mapato, na kuchangia moja kwa moja malipo ya royalty kwa
maelfu ya wamiliki wa haki nchini.
Sowari Akosionu, Afisa Mkuu wa Masoko wa
Mdundo, alisisitiza nafasi muhimu ya Vodacom Tanzania PLC: “Ushirikiano wetu na Vodacom Tanzania PLC umekuwa msingi mkubwa wa
kuwezesha malipo ya mirabaha nchini. Kupitia mtandao wao mpana, Vodacom
inawawezesha wasanii wa ndani kuongeza kipato na kuimarisha ekosistimu ya
muziki ya Kitanzania.”
Mbali na hayo, katalogi ya Mdundo
inajumuisha muziki wa kimataifa na pia muziki wa Kitanzania kuanzia Bongo Flava
hadi Singeli. Mbinu hii ya kulenga muziki wa ndani inaimarisha uhusiano na
wasikilizaji wa Kitanzania, inaongeza mwonekano wa wasanii wa kanda, na inaunda
vyanzo vipya vya kipato kwa wamiliki wa haki.
Kwa kuangalia mbele, Mdundo inalenga
kugawa jumla ya kati ya Dolla za Kimarekani, milioni 2.1 hadi 2.3 kufikia mwaka
2026, huku msisitizo ukiwa juu ya kuinua wasanii wa ndani na kuonyesha vipaji
vya Kitanzania kwenye jukwaa la kimataifa.
Kupitia teknolojia rahisi kutumia,
mitandao mikubwa, na ushirikiano madhubuti kama huu na Vodacom Tanzania PLC,
Mdundo linaendelea kuwapa wasanii wa Kitanzania fursa ya kukuza muziki wao,
kupanua hadhira, na kuongeza kipato chao.

No comments:
Post a Comment