
Bw.Harran Nyakisa Sanga akionesha fomu ya kuomba ridhaa kugombea Ubunge kupitia CCM, Jimbo la Kigamboni.
Na DUNSTAN MHILU
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (MNEKI) mkoa wa Dar es Salaam,anayewakilisha wilaya ya Kigamboni, Haran Nyakisa Sanga amesema endapo wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM na wananchi wa Kigamboni wakimpa ridhaa ya kugombea na kumchagua kuwa mbunge, atahakikisha kwakushirikiana na serikali atatatua kero zinalolikabili jimbo la Kigamboni.
Mneki huyo ameyasema hayo mwishoni mwa wiki alipoteta na TheHabarii ofisini kwake Posta mkoani Dar es Salaam baada ya kuchukuwa fomu ya ugombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni, ambapo ameonesha nia ya kugombea ubunge jimboni humo.
“Kimsingi Kigamboni inahitaji mtu makini na mahiri atakaye kabiliana na kero za jimbo hili , hivyo basi kwakuwa ni mkazi wa Kigamboni na sehemu ambayo nafanya shughuli zangu za kujipatia kipato ni dhahiri shahiri kwamba si mgeni na madhira ya wanakigamboni, hivyo basi niwaombe wanachama wenzangu na wananchi kunipa ridhaa yakuongoza jimbo hilo lenye utajiri lukuki lakini likiwa na changamoto nyingi sana,” amesema Sanga
Akianisha changamoto na vipaumbele vyake Sanga alisema barabara nyingi za Kigamboni ni za vumbi na baadhi yake hazipitiki kipindi cha masika na vuli hivyo akiwa bungeni atapaza sauti yake serikalini kuhakikisha jimbo hilo linakuwa na barabara madhubuti na bora kwa maslahi mapana ya wananchi wa Kigamboni.
Vilevile Sanga alisema kwamba suala la maji atalivalia njuga ipasavyo aidha kwa maji ya Dawasa ama kukaribisha wawekezaji na yeye mwenyewe kutoa mchango wake mkubwa ili upatikanaji wa maji safi na salama yapatikane kwa uhakika kuliko ilivyo sasa.
Na kero nyingine alizoainisha ni elimu ambapo baadhi ya wanafunzi wa jimbo hilo huenda umbali mrefu kusaka elimu lakini atahakikisha shule za sekondari zinakuwa na mabweni ili kuwaepusha wanafunzi na vishawishi vya ibirisi hususani mtoto wa kike.
Sanjari na hilo atahakikisha vijana wa jimbo hilo wanaunganishwa na fursa mbalimbali za ajira ili wajiukwamue kutoka katika lindi la umasikini unaowakumba vijana wa jimbo hilo.
“Mwandishi, umasikini haukubaliki , kwakuwa unatoa utu wa binadamu na unadhalilisha ntakapo pata ridhaa ya kuongoza jimbo hili ntahakikisha wadogo zangu wa kike na wakiume wanaunganishwa na fursa za ajira katika jimbo hilo na nje ya jimbo hilo kwa ajili ya kukuza uchumi wa pato la kaya na Taifa kwa ujumla” alisema Sanga.
Sanga alikwisha chukuwa fomu na kurudisha nah ii si mara yake ya kwanza ,ni mara yake ya pili kushiriki kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo ambapo 2020 alishika nafasi ya nne kati ya wagombea wengi.

No comments:
Post a Comment