DIWANI LYOTO KATA MZIMUNI, AOMBA TENA RIDHAA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 30 June 2025

DIWANI LYOTO KATA MZIMUNI, AOMBA TENA RIDHAA

Mheshimiwa Lyoto akihutubia katika moja ya mikutano ya Hadhara kata ya Mzimuni -Kinondoni Dar es Salaam wakati akiwa diwani 2020-2025.
NA DUNSTAN MHILU

ALIYEKUWA Diwani wa Kata ya Mzimuni wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Manfredy Lyoto amesema endapo atarejea madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani atahakikisha miundombinu na elimu ni mambo yatakayopewa kipaumbele cha kipekee.

Lyoto ameyasema hayo jana baada ya kurudisha fomu ya Udiwani aliyochukuwa Juni 28, 2025 kwa ajili ya kata ya Mzimuni miongoni mwa kata za wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, wakati wa mahojiano na Zanzibar Leo na kusema kwamba kwakipindi alichohudumu na kutamatika kwake Juni 20, 2025 ni mengi amefanya kwakushirikiana na wananchi na serikali kwa ujumla lakini anasema bado ana deni kwa wananchi na ndiyo wanaomhasisha achukue fomu ya udiwani kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.

“Kwa nafasi yangu binafsi nimefanya kwa nafasi yangu katika sekta ya elimu, miundombinu na afya na kwakushirikiana pia baina yangu, halmashauri na wananchi katika kuhakikisha huduma za kijamii katika kata yangu zinakuwa bora zaidi lakini kama ujuavyo shughuli za kimaendeleo ni endelevu hivyo ninahitaji kuboresha zaidi katika maeneo hayo niliyoainisha  hapo awali” alisema Lyoto

Aidha Lyoto alisema kwamba hata hivyo maendeleo yaliyofanywa na serikali ya chama cha mapinduzi katika kata yake hayapaswi kubezwa bali yanapaswa kupongezwa kwakuwa kuna jitihada kubwa zimefanyika ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita.

Akizungumzia sekta ya elimu alisema kwamba ufaulu umeongezeka maradufu ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita lakini amesema anahitaji iboreshwe zaidi kwakuwa walimu baadhi wanahama, wanastaafu na wengine wanaenda masomoni kuongeza ujuzi hivyo kuna kila sabababu kuweka mazingira endelevu kwa ajili ya maboresho ya elimu msingi na sekondari ili waweze kufanya vizuri zaidi ikiwemo kushika nafasi yakwanza kitaifa.

Kuhusu afya amesema, si haba Zahanati ya Kata hiyo inafanya vizuri zaidi baada yakupunguziwa mzigo wa kihuduma kwakuwa wananchi wa Kigogo wana Kituo cha afya sasa ambapo awali walikuwa wakitibiwa katika Zahanati hiyo hivyo msongamano wa wagonjwa umepungua zaidi.

Hali ya kiuchumi kwa wananchi wa kata hiyo imeimarika zaidi kutokana na mikopo mbalimbali ya halmashauri ya asilimia kumi, taasisi za kifedha na uwezeshaji ambao Diwani huyo wa zamani aliweza kuwapatia wananchi hao hususani wanawake, wazee na watoto.”alisema Lyoto

“Awamu hii nitaboresha zaidi kwenye eneo la kuwawezesha kiuchumi mama zangu, dada zangu na wazee wangu  na vijana pia ili wafanye biashara zao vyema na nikwasababu tu kale kasungura kadogo nlikowapa wamekatendea vyema hivyo basi nawiwa kuongeza zaidi ili wakuze biashara zao zaidi na kwa ufanisi kwa ajili ya kukuza pato la kaya na Taifa kwa ujumla” alisema Lyoto baada yakurudisha fomu ya udiwani kata ya mzimuni.

No comments:

Post a Comment