MAFUNZO MFUMO WA D-Fund MIS ULIOBORESHWA YATOLEWA KWA WADAU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 18 May 2025

MAFUNZO MFUMO WA D-Fund MIS ULIOBORESHWA YATOLEWA KWA WADAU

Mtaalam wa Mifumo kutoka Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Fedha na Tehama, Wizara ya Fedha, Bw. George Nguvava, akieleza urahisi wa matumizi ya Mfumo wa D-Fund Management System (D-Fund MIS) ulioboreshwa kwa washiriki wa mafunzo kutoka Wizara, Taasisi na Idara zinazojitegemea, jijini Dodoma.

Na Josephine Majura na Peter Haule, WF, Dodoma

WIZARA ya Fedha imefanya mafunzo ya Mfumo wa D-Fund Management System (D- Fund MIS) ulioboreshwa unaotumika kuratibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Washirika wa Maendeleo.
 
Akifungua mafunzo hayo jijini Dodoma, Mchumi Mkuu kutoka Idara ya Fedha za Nje, Bw. John Kuchaka, alisema kuwa Wizara ya Fedha imefanya maboresho ya Mfumo wa D-Fund ili kuongeza tija zaidi kwa watumiaji wake ambao ni Wizara, Taasisi na Idara zinazojitegemea.
 
Alisema kuwa kutokana na maboresho hayo, Wizara ya Fedha inatoa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo pamoja na kuelekeza nyaraka zote muhimu zinazohitajika katika uchambuzi wa maombi ya fedha.
 
“Lengo la kikao kazi hiki ni kutoa mafunzo ya mfumo ulioboreshwa na kujadili mafanikio na changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa kutumia mfumo huu kwa ajili ya kuuboresha”, alisema Bw. Kuchaka.
 
Alifafanua kuwa Matumizi ya mfumo huo yanatokana na Waraka Na. 2 wa Hazina wa Mwaka 2019 kuhusu utaratibu wa kuomba na kuhamisha fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kwenda moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo (Direct to Project Funds).
 
Aidha, Waraka huo umeelekeza Maafisa Masuuli wote Tanzania Bara kuomba kibali kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali (Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha), kabla ya kutumia fedha za Washirika wa Maendeleo au kuzihamisha kutoka Benki Kuu kwenda benki za biashara.

No comments:

Post a Comment