NAIBU WAZIRI MWANAIDI AWATAKA WADAU KUJIKITA VIJIJINI, ELIMU YA KUPINGA UKATILI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 1 November 2024

NAIBU WAZIRI MWANAIDI AWATAKA WADAU KUJIKITA VIJIJINI, ELIMU YA KUPINGA UKATILI



Na WMJJWM-Dodoma

NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amewataka wadau wanaotoa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili nchini, kujikita kutoa elimu hiyo katika maeneo ya vijijini ambapo wananchi wengi hawafikiwi na taarifa kwa wakati.

Ameyasema hayo Oktoba 31, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua Mpango wa Maandalizi ya Siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili zinazoadhimishwa kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 ya kila Mwaka.

Naibu Waziri Mwanaidi amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kutekeleza afua za kutokomeza ukatili katika jamiii na inathamini jitihada zinazofanywa na wadau katika maeneo mbalimbali ya nchi, hivyo itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya sekta ya umma, binafsi na wadau, kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kijinsia.

Ameongeza Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kupambana na vitendo vya ukatili ikiwemo kuanzisha Madawati ya Kupinga Ukatili katika Vyuo Vikuu, vya Kati na maeneo ya masoko ambapo hadi sasa jumla ya Madawati 332 yameanzishwa kwenye vyuo vya elimu ya juu na elimu ya kati na jumla ya masoko 187 katika mikoa 14 na Halmashauri 96 yameanzisha madawati hayo.

Aidha ameeleza Serikali inaendelea na utekelezaji wa mpango wa pili wa MTAKUWWA ambapo miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya MTAKUWWA ni pamoja na kuanzishwa kwa kamati 18,186 kati ya 20,750 katika ngazi ya Mikoa, Halmashauri, kata vijiji na mitaa na jitihada zinaendelea kuhakikisha kamati hizo zinaundwa katika maeneo yote ya nchi.

Ameongeza Serikali inaendelea kushirikiana na wadau katika kuratibu kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia nchini ambapo katika kuunga mkono mapambano hayo kampeni mbalimbali za Ukatili wa Kijinsia nchini zimeanzishwa ikiwemo, Zijue Fursa, Imarisha Uchumi, Kataa Ukatili, Kazi Iendelee (ZIFIUKUKI) pamoja na kampeni mbalimbali zinazotekelezwa ngazi ya mamlaka za Serikali za Mitaa.

"Niwapongeze wadau mbalimbali wanaotekeleza afua za kutokomeza ukatili hususani Shirika la Blue Cross, Shirika la Mission 21 pamoja na Kanisa la Moravian. Kazi yenu ni njema na itasaidia kutoa elimu kwa Umma kwa lengo la kuwa na jamii huru dhidi ya ukatili wa kijinsia" amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi.

Naye Meneja Programu wa Shirika la Blue Cross Gloria Vincent amesema Shirika hilo limeona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kuifikia jamii kwa kutoa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili kwa kutumia njia mbalimbali hasa kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa maeneo husika, Kimiila na Kidini ili kuifikia jamii ili iondokane na vitendo hivyo.

Nao baadhi ya wadau walioshiriki Mkutano wa wadau kuelekea Siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wamesema wapo tayari kufika maeneo ambayo Mashirika mengi hayajafika ili kushirikiana na jamii husika kujadiliana na kupata namna bora ya jamii kuondoka na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake Watoto na Wanaume.

No comments:

Post a Comment