MIRADI YA NYUMBA NA MAJENGO YA SERIKALI YAENDELEA KUTEKELEZWA - KASEKENYA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 24 October 2024

MIRADI YA NYUMBA NA MAJENGO YA SERIKALI YAENDELEA KUTEKELEZWA - KASEKENYA

 

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, pamoja na Wakurugenzi wa Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi, Mha. Godfrey Kasekenya (hayupo pichani) alipowasilisha Taarifa ya Ujenzi na Ukarabati wa Nyumba na Majengo ya Serikali unaosimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) jijini Dodoma, Oktoba 24, 2024.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Kakoso akisisitiza jambo mara baada ya kupokea Taarifa ya Ujenzi na Ukarabati wa Nyumba na Majengo ya Serikali unaosimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Septemba, 2024 kutoka kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mha. Godfrey Kasekenya (hayupo pichani), jijini Dodoma, Oktoba 24, 2024.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya akiwasilisha Taarifa ya Ujenzi na Ukarabati wa Nyumba na Majengo ya Serikali unaosimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Septemba, 2024 kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, jijini Dodoma, Oktoba 24, 2024.

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya amesema Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) inaendelea kutekeleza miradi Saba ya ujenzi na ukarabati wa nyumba na majengo ya Serikali kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo fedha za ruzuku kutoka Serikalini.

Akizungumza wakati akiwasilisha taarifa kuhusu ujenzi na ukarabati wa nyumba na majengo ya Serikali unaosimamiwa na Wakala huo kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Septemba, 2024 Naibu Waziri Kasekenya amesema kuwa katika kipindi hicho Wakala ulipanga kutekeleza miradi Nane ambapo mradi mmoja kati ya hiyo umekamilika.

“Katika kipindi hiki cha Julai, 2023 hadi Septemba, 2024 TBA imetekeleza na inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa ghorofa za watumishi wa Umma za Kaloleni Kota jijini Arusha na Ghana Kota jijini Mwanza pamoja na ujenzi wa nyumba nyingine 20 za Viongozi jijini Dodoma”, amesema Kasekenya.

Aidha, Kasekenya ameongeza kuwa miradi hiyo ya ujenzi iliyotekelezwa inahusisha nyumba 356 ambapo nyumba 16 zilizopo Magomeni Kota zimekamilika na ujenzi wa nyumba 340 unaendelea huku jumla ya nyumba 20 zikikarabatiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Kakoso ameitaka Wizara ya Ujenzi kuendelea kuisaidia TBA kukusanya madeni kwa Taasisi za Serikali, Wizara  na watumishi wanaodaiwa Fedha za Pango na Wakala huo ili fedha zinazopatikana ziwezeshe Wakala kutekeleza miradi mingi zaidi. 

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud Kondoro amesema kuwa Wakala utaendelea na zoezi la ukusanyaji wa kodi kwa wapangaji wake na itachukua hatua kwa wadaiwa Sugu kama ambavyo imekwishaanza kufanya kwa baadhi ya mikoa ikiwemo Dar es Salaam.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.

No comments:

Post a Comment