MHE PINDA AKUTANA NA VIONGOZI WA TUME HURU YA UCHAGUZI YA BOTSWANA NA WADAU WENGINE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 24 October 2024

MHE PINDA AKUTANA NA VIONGOZI WA TUME HURU YA UCHAGUZI YA BOTSWANA NA WADAU WENGINE

 


MKUU wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC -SEOM) nchini Botswana, Mhe. Mizengo Pinda amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti na Uongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Botswana (IEC) na wadau wengine wa Uchaguzi katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Gaborone, Botswana.

Mhe. Pinda amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti na Uongozi wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Botswana Mhe. Jaji Barnabas Nyamadzabo na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw. Jefferson Siamisang ikiwa ni miongoni mwa watu na taasisi mbalimbali anaokutana nao ili kusikiliza na kufahamu kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusu uchaguzi Mkuu wa Botswana uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa IEC Mhe. Jaji Nyamadzabo alielezea Majukumu ya Tume hiyo kama yalivyoainishwa katika Kifungu cha 65A cha Katiba ya Botswana kuwa ni Kusimamia na kuendesha uchaguzi wa Wabunge wa Bunge la Taifa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; Kuendesha kura ya maoni; Kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ufanisi, kwa usahihi, kwa uhuru na kwa haki; Kutoa maagizo na maelekezo kwa Katibu wa Tume kuhusiana na majukumu yao chini ya Katiba na Sheria za Uchaguzi kwa ujumla na Kutekeleza majukumu mengine yoyote kama itakavyowekwa na Sheria ya Bunge la nchi hiyo.


Alisema kuwa IEC pia inajukumu la kuandikisha wapiga kura na kudhibiti gharama za kampeni na kuongeza kuwa Tume hiyo haina mamlaka ya kuamua migogoro ya uchaguzi ambayo inapelekwa Mahakama Kuu. 

Naye Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw. Siamisang alieleza kuwa IEC imejipanga kikamilifu kuendesha zoezi la Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo na iko tayari kuifanya kazi hiyo kwa tija na ufanisi.

Amesema IEC tayari imeendesha zoezi la upigaji kuwa kwa diaspora wa Botswana, watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama na watumishi wa IEC lililofanyika tarehe 18 Oktoba 2024 na kuongeza kuwa IEC imeandikisha wapiga kura sawa na asilimia 80 ya lengo walilojiwekea katika zoezi lililofanyika kwa awamu tatu ikiwa ni ongezoko la asilimia Saba kutoka kwa wapiga kura wa mwaka 2019 walipofanya uchaguzi mkuu.

“IEC imeshaendesha zoezi la kupiga kura kwa hatua ya kwanza, zowezi hilolimehusisha diaspora wetu tuliowaandikisha, vyombo vya ulinzi na usalama n ahata awatumishi wa Tume, nikuhakikishie kuwa tumejipanga na tuko tayari kusimamia na kuendesha zoezi la uchaguzi kwa ufanisi, kila kitu kiko tayari na wahudumu wetu pia wako tayari kwa ujumla maandalizi yamekamilika tunasubiri tu siku ya kupiga kura,” alisema.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya Tume hiyo ya IEC, Mkuu wa misheni ya Uangalizi ya SADC -SEOM Mhe. Mizengo Pinda ameishukuru IEC kwa kukutana nao na kuwalezea jinsi walivyojipanga kuendesha zoezi zima la uchaguzi.

Mhe. Pinda alieleza kuwa SEOM wanajukumu la kuangalia namna uchaguzi huo unavyoeendeshwa ikiwa ni sehemu ya kukuza na kuendeleza demokrasia katika ukanda a wa SADC.

Amesema SEOM imepeleka waangalizi katika wilaya na majiji yote ya Botswana ili kuangalia zoezi zima kabla ya uchaguzi, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi jinsi itakavyokuwa na inatarajia kutoa taarifa ya awali kuhusu hali ilivyokuwa tarehe 1 Novemba 2024. 

Mhe. Pinda na ujumbe wake wamezungumza kwa njia ya mtandao na Kiongozi  wa Chama Kipya cha Siasa cha Botswana Republican Party (BRP) Bw. Biggie Butale. Chama cha BRP  kimesimamisha wagombea 10 katika nafasi ya viti vya Bunge la nchi hiyo.

Mhe. Pinda alieleza dhamira ya ujumbe wake kuzungumza na kiongozi huyo ili kupata maoni na mawazo yake kuhusu namna kampeni za uchaguzi zinavyoenda kwa wakati huu kama mazingira ni mazuri na yanaridhisha.

Bw. Biggie alielezea kuridhishwa kwake na namna shughuli za kuelekea uchaguzi mkuu zinavyoendeshwa na kwamba mazingira yamekuwa salama ila alielezea kutokuridhishwa kwake na wazo la kutoa fedha za uchaguzi kwa vyama vya siasa baada ya uchaguzi na kuongeza kuwa hatua hiyo haitoi nafasi kwa vyama vya siasa kuwa sawa na hivyo kuwapa manufaa vyama vikongwe na vikubwa na kuviacha vyama vichanga njiani.

Katika tukio jingine Mhe. Pinda na ujumbe wake wamekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa wa Taasisi ya African Trust ya jijini Gaborone Bw. Monametsi Sokwe na kusikiliza maoni na mtazamo wake juu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu yanavyokwenda. 

Bw. Sokwe ameshukuru kukutana na SEOM na kusema kuwa vyama vingi ni vichanga na havina nguvu za kifedha kuendesha shughuli zao za kisiasa hasa za kampeni wakati huu wa uchaguzi.

Mhe. Pinda amemuomba Bw. Sokwe na washirika wake kuhakikisha wanaongeza na kuwashirikisha kwa wingi wanawake na vijana katika shughuli za siasa kwani huko ndio kukua kwa demokrasia.

Tarehe 30 Oktoba, 2024 Wananchi wa Botswana watapiga kura katika Uchaguzi mkuu kuchagua Wabunge wa Bunge la 13 la nchi hiyo na wajumbe wa Mabaraza ya Mitaa ambpo Viti 61 vya Bunge la Taifa na viti 609 vya mabaraza ya mitaa vitashindaniwa. 

SEOM imepeleka waangalizi wake wa uchaguzi katika wilaya, miji na majiji yote nchini Botswana.

No comments:

Post a Comment