WANANCHI WASISITIZWA KUTUMIA KWA USAHIHI MIUNDOMBINU YA MAJITAKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 27 March 2024

WANANCHI WASISITIZWA KUTUMIA KWA USAHIHI MIUNDOMBINU YA MAJITAKA

 

MTUMISHI wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Henry Motto, akinyonya majitaka yaliyotuama katika mtaa wa Kitenge kata ya Majengo jijini Dodoma leo Machi 26, 2024. (Picha na Mpigapicha Wetu).

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph (kushoto) akimpa maelezo Diwani wa Kata ya Majengo, Shufaa Ibrahim (wa pili kulia) namna taka ngumu zinazosababisha uzibaji wa chemba za majitaka wakati wa ziara yake leo Machi 26, 2024 ya kutembelea kata hiyo na kujionea hali ya mazingira ilivyo. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma DUWASA, Rahel Muhando (Picha na Mpigapicha Wetu).

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph (wa pili kushoto) akimpa maelezo Diwani wa Kata ya Majengo, Shufaa Ibrahim namna taka ngumu zinazosababisha uzibaji wa chemba za majitaka wakati wa ziara yake leo Machi 26, 2024  ya kutembelea kata hiyo na kujionea hali ya mazingira ilivyo. Kulia ni Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira DUWASA, Mhandisi Bernard Rugayi. (Picha na Mpigapicha Wetu).

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph amewataka wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya utumiaji wa mfumo wa mtandao wa majitaka ili kuondokana na adha ya kuziba mara kwa mara kwa mitandao hiyo.

Ameyasema hayo leo Machi 26, 2024 wakati alipotembelea Kata ya Majengo, Mtaa wa Kitenge eneo lililoathiriwa na kujaa kwa majitaka kwa lengo la kukagua na kujionea hali ya mazingira katika eneo hilo.

“Maendeleo yanaenda na mambo mengi na yanagharama kidogo, na gharama yenyewe ndio kama hii, lakini isingekuwa hivi, kama wananchi wanazingatia matumizi sahihi ya mtandao wa majitaka”. Amesema Mhandisi Aron

Amesema uzibaji wa mara kwa mara katika mifumo ya majitaka sio kwa sababu ya majitaka kuwa mengi, bali ni kuingizwa kwa vitu na taka ngumu ambavyo vinasababisha mfumo huo kuziba.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi watumie kwa sahihi mfumo wa majitaka, mfumo wa majitaka ni kwa ajili ya kutumia majitaka tu hata maji ya mvua hayatakiwi kuingia kwenye mfumo huo”. Amesema Mhandisi Aron

Naye Diwani wa Kata ya Majengo, Mhe. Shufaa Ibrahim ameishukuru DUWASA kwa kupokea malalamiko na kufika eneo lenye changamoto ili kujionea hali halisi na  kuweza kutatua changamoto hiyo na kuahidi kuitisha mkutano wa wakazi wa eneo hilo na kuwaita wataalamu kutoka DUWASA ili waweze kutoa Elimu ya kutosha kwa wananachi.

Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi Wa Mazingira DUWASA, Mhandisi Bernard Rugayi amesema kwa sasa wanaendelea na zoezi la unyonyaji wa majitaka katika eneo hilo na ameahidi kumaliza changamoto hiyo kwa muda wa siku tano.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tawi la Bahi Road, Kapteni Sungura Muhando amesema wananchi wanapaswa kupewa elimu kwa sababu mara nyingi wamekuwa wakiweka vitu vya ajabu katika mifumo ya majitaka.

No comments:

Post a Comment