![]() |
| Waziri Mkuu mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa enzi za uhai wake. |
WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa amefariki dunia, Jumamosi ya Februari 10, 2024. Taarifa za kifo cha kiongozi huyo maarufu zimetangazwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango kwa niaba ya Serikali. Dk. Mpango amesema Lowassa amekutwa na umauti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa zinaeleza kuwa, Mhe. Lowassa alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya mapafu na shinikizo la damu hadi alipofariki dunia.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametuma salamu za rambirambi, huku akieleza kuwa amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa kwani Waziri Mkuu huyo mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 – 2008, amelitumikia taifa katika nyadhifa mbalimbali wakati wa uhai wake.
Rais Dk. Mwinyi ameitaka familia ya marehemu Lowassa, ndugu na marafiki kuwa na moyo wa Subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Rais Dk. Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi, Amin.
Mhe. Lowassa ni mwenyeji Monduli mkoani Arusha, aliyezaliwa Agosti 26, 1953 na baadae alifanikiwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo la Monduli na kuingia Bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 1990. Lowassa alisoma shahada ya kwanza katika tamthilia kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, halafu shahada ya pili katika Sayansi ya maendeleo ya Jamii Chuo Kikuu cha Hull nchini Uingereza.
Katika enzi za uhai wake Lowassa amepata nafasi ya kushika nafasi mbalimbali zikiwemo Uwaziri mdogo wa Mazingira na Mapambano dhidi ya umaskini katika Ofisi ya Makamu wa Rais (1988-2000).
Aliwahi pia kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa-AICC(1989-1990), Waziri mdogo wa Haki na Mambo ya Bunge katika ofisi ya Makamu wa Rais (1990-1993), Mbunge wa Monduli tangu mwaka 1990 na Disemba 2005 alipitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na ilipofika mwaka 2015 aligombea nafasi ya Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo na kuwa na ushawishi mkuwa wa wafuasi japo hakufanikiwa kushinda.


No comments:
Post a Comment