KRISTO ALIKUJA KUWALETA WATU PAMOJA—PADRI MASANJA - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 11 February 2024

KRISTO ALIKUJA KUWALETA WATU PAMOJA—PADRI MASANJA

Na Adeladius Makwega-MWANZA

WAKRISTO wameambiwa kuwa Kristo amekuja kuwaleta watu pamoja na siyo kuwatenga, maana hata kabla ya Kristo wagonjwa wa ukoma walitengwa na kukaa mbali na jamii na kuwa sasa ni wakati wa kuyatazama makundi yanayotengwa na kuwa nayo karibu na huko ni kuwa karibu na Mungu.

Hayo yamesemwa na Padri Samson Masanja ambaye ni Paroko wa Parokia ya Malya, katika misa ya dominika ya 6 ya mwaka B wa Liturjia ya Kanisa, Jumapili ya Februari 11, 2024 katika kanisa la Bikira  Maria- Malkia wa Wamisionari, Parokia ya Malya Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.

“Katika Jamii zetu, wapo watu wanaofanana na wenye ukoma, ambao tunawatenga; Wao ni kama vile yatima , wafungwa, wajane, wapo watu wenye hali mbaya za maisha, Je tunawajali? Je tunatambua mahitaji yao? Je tunayaona haya yanayowasibu? Je tunayapatia majibu?

Sisi sote tuige mfano wa Kristo wa kutambua changamoto zetu na changamoto za wenzetu kwa kuzitatua”

Misa hiyo pia iliambatana na nia na maombi kadhaa,

“Eee Bwana Yesu, uliwaponya wagonjwa, utusaidie katika shida zetu za roho na mwili. Eee Bwana-Twakuomba Utusikie.”

Katika misa hiyo waamini waliambiwa kuwa wakati wa Kwaresma umekaribia na kama yupo muumini mwenye matawi yaliobarikiwa mwaka jana wayalete kanisa kabla ya Jumatano ya Majivu Februari 14, 2024 na pia kuelezwa kuwa siku ya Jumatano ya Majivu kutafanyika misa mbili asubuhi na jioni. 

Hadi misa hiyo imalizika saa moja ya asubuhi, hali ya hewa ya Malya na viunga vyake ni hali ya joto kali ambalo linakaribia nyuzi joto 29 sentigredi wakati wa mchana, jua kali nyakati za mchana na manyunyu kiasi na hilo likionesha kuwa sasa mvua zinapungua na pengine msimu wa masika ukipunga mkono wa kwaheri.


No comments:

Post a Comment