Waziri wa ujenzi, Innocent Bashungwa, akifafanua jambo kwa wananchi
wa Kata Mlangali iliyopo Wilayani Ludewa mara baada ya kukagua ujenzi wa
barabara ya Itoni-Lusitu (km 50) kwa kiwango cha zege, Mkoani Njombe.
|
|
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza
kuwa Serikali inatarajia kuanza kujenga upya barabara ya Songea – Njombe -
Makambako kwa kiwango cha lami kutokana na barabara hiyo kuwa nyembamba na muda
wake kuisha.
Bashungwa amesema hayo Wilayani Ludewa,
mkoani Njombe wakati akizungumza na wananchi wa Mlangali katika mkutano wa
hadhara ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza mikakati ya Serikali ya Awamu
ya Sita ya kufungua mikoa na nchi jirani kwa barabara za lami.
Bashungwa amesema hadi kufikia mwezi
Machi mwaka huu Serikali itakuwa imempata Mkandarasi atakayenga upya barabara
hiyo ikiwa ni dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua
mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
“Ukitoka bandari ya Mtwara unakuja kwa
lami hadi Songea, na kutoka Songea kuja Njombe mjini kwenda makambako, lami
ilijengwa miaka ya 80 imechoka, tayari Mheshimiwa Rais ametupatia fedha na
kufika mwezi wa tatu au wa nne tutakuwa tumepata mkandarasi anakuja
kuijenga upya”, amesema Bashungwa.
Bashungwa amewataka wananchi kuendelea
kuheshimu Sheria na kutofanya shughuli katika maeneo ya hifadhi ya barabara ili
kuondokana na usumbufu pale Serikali inapotumia Sheria zilizowekwa kuwaondoa
katika maeneo ili kujenga miundombinu ya barabara.
Aidha, Bashungwa amesema Serikali itatoa
shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya kuunganisha barabara inayotokea Wilaya ya
Busokelo Mkoani Mbeya hadi Wilaya ya Makete mkoani Njombe kwa kiwango cha
changarawe.
Ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais ameagiza
kupelekwa Bilioni 1 kwa ajili ya kufanyia maboresho barabara ya Ikonda – Lupila
– Mlangali ambayo imekuwa na changamoto hasa katika kipindi cha mvua.
Naye, Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga ameiomba
Serikali kujenga barabara ya kilometa moja inayoelekea katika kituo cha Afya
ambacho ndicho kimekuwa kikitoa huduma kubwa kwa wananchi wake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa,
Victoria Mwanziva, ameeleza kuwa wilaya hiyo ni wilaya ya kimkakati hivyo
inahitaji miundombinu bora kwa ajili ya kurahisisha usafiri na usafirishaji wa
mazao, asali na bidhaa ndani na nje ya nchi.


No comments:
Post a Comment