Na Mwandishi Wetu
BENKI ya NMB
imesema imeanza kuzingatia kwa karibu masuala ya uhifadhi wa mazingira katika
uendeshaji wake na kufadhili miradi mbalimabli kutokana na umuhimu wake katika
kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Alhamisi wiki hii, afisa
mwandamizi wa benki hiyo, Bi Hellen Dalali, alisema kutokana na hilo NMB sasa
inaipa kipaumbele miradi rafiki kimazingira na wakopaji wanaolitambua hilo.
Bi Dalali aliuambia mkutano kuhusu masuluhisho asilia (NBS)
dhidi ya janga la mabadiliko ya tabianchi kuwa ufadhili unaofanywa na benki
hiyo umejikita zaidi kupunguza athari za hewa ukaa na kuongezeka kwa joto
duniani.
Alisema NMB imeweka msimamo huo kutokana na umuhimu wa
miradi ya kijani na ile yenye tija kijamii kuwa na mchango mkubwa katika
maendeleo endelevu.
Aidha, Meneja Miradi Mwandamizi huyo alibainisha kuwa athari
za mabadiliko ya tabianchi si tu ni hali halisi iliyopo bali pia ni hatari
kubwa ambayo madhara yake tayari yanaziyumbisha biashara na chumi nyingi duniani.
Akizungumzia athari za janga hilo wakati wa jopo la
utangulizi la mkutano huo, alisema sekta ya fedha nayo tayari imeahirika hivyo
kuongeza umuhimu wake kushiriki na kuwekeza vilivyo katika hatua za kupambana
na changamoto hizo.
“Hakuna hata mmoja wetu ambaye hajaathirika kwa hiyo wote
tunawajibika kushiriki kikamilifu kupambana na athari hizi,” Bi Dalali
aliwaambia washiriki wa Mkutano wa NBS Tanzania 2023, ambao ulilenga hasa
maendeleo ya biashara ya hewa ya ukaa nchini.
Alisema hatari za mabadiliko ya tabianchi zimeilazimu NMB na
benki nyingine kubuni mbinu mpya za kibenki na uendeshaji ili kupunguza kaboni
hewani na kukidhi matarajio ya kuhifadhi mazingira.
"Mabadiliko ya tabianchi yameathiri biashara nyingi
duniani na kupekea chumi nyingi na sekta ya fedha kuathirika vile vile kutokana
na biashara hizi kufadhiliwa na benki,” alibainisha.
Kwa mujibu wa Bi. Dalali, benki hazijikiti tu kupunguza
shughuli zake kuathiri mazingira bali pia zinaongeza umakini katika tathmini za
athari za kitabianchi na kijamii kwenye michakato ya mikopo.
Hilo linafanyika kuunga mkono juhudi za kitaasisi
kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha miradi na
biashara zinazofadhiliwa zinakuwa na madhara madogo au haziathiri kabisa
mazingira, alifafanua.
Aliongeza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa benki
zipo za aina mbili, moja ikiwa ni zile zinatokana na uharibifu wa mali na
rasilimali kutokana na majanga kama mafuriko
au mvua kubwa.
Kundi la pili ni lile la athari za kimpito ambazo hasa
zinatokana na madiliko ya kikanuni, kisera, kiteknolojia na kimasoko
yanayolenga kuchagiza shughuli za kiuchumi zinazozalisha hewa kidogo ya ukaa na
kupambana na changamoto nyingine za mabadiliko ya tabianchi.
Bi Dalali aliuambia mkutano huo wa siku moja kuwa pamoja na
athari zake nyingi, mabadiliko ya tabianchi pia yana fursa lukuki za
kibiashara, ambazo mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo, Waziri Angela Kairuki,
alisema ni pamoja na biashara ya hewa ukaa ambayo inazidi kuimarika nchini.
Akitolea mifano ya hatifungani ya NMB Jamii Bondi na kampeni
ya kupanda miti iliyozinduliwa na benki hiyo mwanzoni mwa mwaka huu, mtaalamu
huyo wa masuala ya uendelevu alisema benki zinaweza kuongoza kuzifungua fursa
hizo kupitia ufadhili endelevu na ule wa kijani.
"Athari za mabadiliko ya tabianchi zinatoa fursa na
mazingira muafaka ya biashara kwa sekta binafsi na benki kushiriki. Hii ni
kupitia uhamasishaji stahiki wa fedha na mitaji ili kuweza kufadhili miradi ya
kukabiliana na changamoto hizo,” alibainisha na kusisitiza umuhimu wa
uwezeshwaji kimaarifa ili kuwa na kada yenye ufahamu mzuri wa ufadhili wa aina
hiyo.





No comments:
Post a Comment