Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. |
NISHATI ya Umeme kwa wanadamu ni muhimu katika maendeleo ya nchi na taifa
kwa ujumla na ni hitaji la kuaminika
hasa pale bei yake inapokuwa nafuu.
Nishati hiyo inaweza kuboresha na hata kuokoa maisha, nishati ya kuaminika
inasaidia tasnia iliyopanuliwa kama kilimo cha kisasa, kuongezeka kwa biashara
na uboreshaji wa usafirishaji.
Matumizi ya nishati ya umeme yamegawanyika katika
sekta nne za kiuchumi ambazo ni makazi, biashara, usafirishaji na viwanda.
Kazi nyingine ya nishati ya umeme ni kupasha joto na kuweka ubaridi katika nyumba, kuwasha majengo ya
ofisi, kuendesha magari na mizigo inayosonga, na kutengeneza bidhaa
tunazozitegemea katika maisha yetu ya kila siku.
Nikutokana na umuhimu wa nishati hiyo hapa nchini Oktoba 17, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia ombi la kuzindua uwashaji umeme katika vijiji takribani 131 mkoani Singida kupitia mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Kata ya Shelui Wilaya ya Iramba uliotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy. |
Rais Samia aliipongeza REA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kazi
kubwa ya kusambaza umeme mkoani hapa ambapo alisema hadi ifikapo Mwezi Juni,
2024 Mkoa wote wa Singida utakuwa umemepata umeme katika maeneo yote.
Katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alipata
fursa ya kuelezea mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa miradi hiyo ambapo kwa
niaba ya Bodi ya Nishati Vijijini na watumishi wenzake wa REA walimkushukuru Rais
Dkt.Samia kuridhia ombi la kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.
Mhandisi Saidy
anaanza kwa kusema Wakala wa Nishati Vijijini ni taasisi ya umma iliyo chini ya
Wizara ya Nishati yenye jukumu la kuwezesha upatikanaji wa Nishati Bora maeneo
ya vijijini ikiwemo Nishati ya Umeme. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, Wakala
wa Nishati Vijijini kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
umesaidia kuongeza hali ya upatikanaji umeme vijijini kwa upande wa Tanzania
Bara kutoka asilimia 5% mwaka 2007 hadi 70% mwaka 2020 (ambapo tathmini ya
mwisho ilifanyika).
Anasema kupitia
miradi mbalimbali ya umeme vijijini, Serikali kupitia Wakala wa Nishati imeweza
kufikisha huduma za umeme katika vijiji 10,987
sawa na asilimia 89 ya vijiji vyote 12,318 vilivyopo Tanzania Bara.
“Kwa upande wa
vitongoji, kati ya vitongoji 64,760
vilivyopo nchini, vitongoji 28,659
sawa na asilimia 44 vishafikiwa
na huduma ya umeme. Serikali inaendelea na mipango ya kuongeza mafungu katika
Mfuko wa Nishati Vijijini ili kuongeza kasi ya kufikisha umeme katika vitongoji 36,101 vilivyobaki kupitia
Mpango wa Kufikisha Umeme Vitongoji Vyote (Hemlet Electrification Project-HEP),”
anasema Saidy.
Aidha, Saidy
anasema Tanzania chini ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan
imeendelea kupiga hatua kubwa katika kufikisha nishati bora vijijini kama njia
ya kuboresha maisha ya wananchi, kuwezesha shughuli za uzalishaji mali zikiwemo
biashara, viwanda na kilimo pamoja na kuboresha huduma za jamii zikiwemo afya,
elimu, maji, mawasiliano.
Anasema zaidi ya
shughuli za uchumi na huduma za jamii, umeme vijijini umesaidia; kuboresha
ulinzi, kuhifadhi mazingira, kuimarisha usawa wa kijinsia pamoja na kuchangia
azma ya serikali katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ambapo upatikanaji
wa Nishati bora utasaidia kufikia malengo 13 kati ya malengo 17.
“ Hivi
tunavyoongea Serikali inatekeleza miradi mikubwa Saba (7) ya kupeleka umeme
maeneo ya vijijini kupitia kandarasi 112 (Contract/Lots) ambayo kwa ujumla wake
itapeleka umeme katika vijiji na vitongoji takribani 11,000 kwa gharama ya Sh.Bilioni
2,768. Miradi hiyo ni pamoja na:
1.
Miradi wa Ujazilizi
Awamu ya Pili A (mioa 9), 2B (Mikoa 9) na 2C (Mikoa 7) ambayo itafikisha huduma
za umeme katika vitongoji 4,895 katika mikoa 25 ya Tanzania bara kwa gharama za
Sh.Bilioni 654.
2.
Mradi wa kusambaza umeme
katika maeneo 808 (mitaa na vitongoji) yaliyopo pembezoni mwa miji (vijiji
miji) ambayo inatekelezwa katika mikoa 13 kwa gharama ya Sh.Bilioni 189.4.
3.
Ujenzi wa Vituo Vya
Kupoza Umeme eneo la Ifakara (Ifakara Substation) na Mtera (mtera Substation)
vyenye uwezo wa 20MVA kila kimoja pamoja na mifumo ya kusambaza Umeme Vijijini
kwa wilaya za Kilombero na Ulanga mkoani Morogoro na mikoa ya Iringa, Dodoma,
Shinyanga na Tabora ambapo vijiji 136 vimefikishiwa huduma kwa gharama ya Sh. Bilioni
82.
4.
Mradi wa Kusambaza Umeme
Katika Migodi Midogo, Maeneo ya Kilimo na Viwanda; 336 yaliyopo maeneo
mbalimbali hapa nchini kwa gharama ya Sh.Bilioni 115
5.
Mradi wa Kusambaza Umeme
Katika Vituo vya Afya na Pampu za Maji 460 maeneo mbalimbali katika mikoa yote
kwa gharama ya Sh.Bilioni 34.5
6.
Mradi wa Kupeleka Umeme
katika Vitongoji 654 Katika Mikoa ya Songwe na Kigoma (Hamlet Electrification
Project I - HEP I) kwa gharama ya Sh. bilioni 100
7.
Mradi Kabambe wa
Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya III Mzunguko wa II (Turkey Phase III – Round
II) unaotekelezwa kwa mafungu 39 ambapo vijiji 4071 katika mikoa 24
vitafikishiwa umeme kwa gharama ya Sh.1,593,” anasema Mhandisi Saidy.
Mhandisi Saidy
anasema mradi huo Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya 3 Mzunguko wa 2 ndio
unaenda kuhitimisha safari ya kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji
vyote 12,318 Tanzania Bara kama ambavyo imeelekezwa katika Ilani ya uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 kuwa ifikapo mwaka 2025 vijiji vyote viwe
vimefikiwa na huduma za umeme.
Anasema kati ya
vijiji 4071 katika mradi huu, vijiji 2,740 vishafikiwa na huduma za umeme na
vijiji 1,331 vilivyobaki, wakandarasi wanaendelea na shughuli za ujenzi ambao
mpaka kufikia mwezi Juni 2024 mradi huo utakuwa umekamilika kwa mafungu yote 39
na hivyo kufanya vijiji vyote kufikiwa na huduma ya umeme kabla ya mwaka 2025.
Baada ya
kukamilisha safari ya kufikisha umeme katika kila kijiji, na kwa kutambua kuwa
ndani ya vijiji kuna vitongoji ambavyo havijafikiwa na huduma, Wakala
unajipanga kutekeleza mpango mkubwa wa kufikisha umeme katika vijiji 10,000
ndani ya miaka 5 ambapo kwa kuanza, ndani ya mwaka huu wa fedha, serikali
itatangaza zabuni ili kupata wakandarsi watakaojenga miundombinu ya kusambaza
umeme katika vitongoji 3060 ambavyo ni wastani wa vitongoji 15 kwa majimbo yote
204 yaliyo maeneo ya vijijini.
Anasema Mkoa wa Singida una jumla ya vijiji 441. kati ya vijiji hivyo,
vijiji 397 sawa na asilimia 90% ya vijiji vyote katika
mkoa huu vimeshapatiwa umeme kupitia miradi mbalimbali ya umeme vijijini.
Mhandisi Saidy anasema katika kuhakikisha vijiji vyote
vinapata huduma za umeme, Serikali kupitia mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini
Awamu ya 3 Mzunguko wa Pili imetenga Shilingi
bilioni 71.6 ili kufikisha umeme katika vijiji 175 mkoani Singida. Mradi huo unatekelezwa na wakandarasi wawili;
kampuni ya Central Electricals International Ltd inatekeleza mradi kwa wilaya
za Singida DC na Ikungi (amepewa
vijiji 94 ambapo amewasha vijiji 70, vijiji 2 keshakamilisha kazi vinasubiri
kukaguliwa na anaendelea na kazi katika 22), na CRJE-CTCE CONSORTIUM kwa wilaya
za Iramba, Manyoni, Mkalama (amepewa
vijiji 81 ambapo amewasha vijiji 61, vijiji 3 kesha maliza kazi vinasubiri
kukaguliwa na anaendelea na kazi katika 17) ambapo hadi kufikia Oktoba 15.2023
vijiji 131 vishafikishiwa huduma za umeme ambavyo leo unazindua rasmi
uwashwaji wake na kuwa vijiji 5 kazi ishakamilika vinasubiri ukaguzi na 39
vilivyobaki vitafikiwa kabla ya kuisha mwezi Disemba mwaka huu (2023).
Mhandisi
Saidy anasema pamoja na mradi huo, Serikali pia inatekeleza miradi
mingine Mitatu (3) katika mkoa wa Singida ambayo ni:
· Mradi wa Kupeleka umeme Pembezoni mwa Miji (Peri-Urban
III) ambapo maeneo 34 yatafikishiwa huduma za umeme (Sh.Bilioni 7.1)
· Mradi wa Kupeleka umeme kwenye migodi midogo 22 (Sh.Bilioni
5.5)
·
Mradi
wa kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya 5 na Pampu za Maji 23 kwa lengo la
kuboresha huduma hizo pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali katika
kupambana na magonjwa ya kuambukiza (Sh.Bilioni 1.6) na jumla ya gharama ya miradi
yote ni Sh. Bilioni 85.8.
Mhandisi Saidy kwa niaba ya Bodi na
Watumishi wenzake wa Wakala wa Nishati Vijijini alitumia nafasi hiyo kutoa
shukrani kwa serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea
kutoa fedha za kuwezesha utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini ambayo kama
nilivyosema awali miradi ya takriban Sh. Trilioni 2.8 inatekelezwa nchi mzima.
Aidha, alimpongeza Rais Samia kwa, azma, maamuzi na jitihada zake za
kuhakikisha nchi yetu inaondokana na matumizi ya Nishati isiyo salama na
kuhamia katika Nishati Bora ya Kupika.
“Tunatambua jitihada zako hizo zimejengwa na dhamira yako ya dhati katika;
kulinda afya za watanzania, kulinda misitu yetu, kuzuia mabadiliko ya tabia
nchi, kuepusha unyanyasaji wa kijinsia, na kuwapa unafuu wa maisha, wananchi
waishio vijijini hasa kina mama na watoto,” anasema Saidy.
Anasema Wakala wa Nishati Vijijini zaidi ya miradi ya umeme, unawezesha pia
upatikanaji wa Nishati Bora ya Kupikia Vijijini ambapo kwa mwaka huu wa fedha
tunatekeleza miradi minne (4) ikiwemo; usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia
(LPG), usambazaji majiko banifu, ufungaji wa mifumo bora ya kupikia katika
taasisi zaidi ya 100 zinazohudumia watu zaidi ya 300 pamoja na usambazaji wa
gesi asilia kwa ajili ya kupikia katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara. Miradi
hii ni endelevu na Wakala utaendelea kupanua wigo wa utekelezaji pamoja na aina
za nishati kila mwaka kutegemea na upatikanaji wa fedha.
Mhandisi Saidy
anasema mwisho ila sio kwa umuhimu, wana
mkushuru tena Rais kwa kuendelea kuwaupa
dhamana ya kuongoza taasisi hiyo muhimu ambapo pamoja na watumishi wenzake wa
Wakala, wanafahamu ukubwa na umuhimu wa jukumu walilopewa na wanaahidi
kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uadilifu ili kutimiza matamanio
na azma yake ya kuona kila mtanzania hasa wa vijijini anafikiwa na huduma za
nishati bora.
Anasema kwa kuzingatia hilo, Wakala wa nishati vijijni (REA) na kwa uongozi
mzuri uliopo katika Wizara ya Nishati, wanamuhakikishia Rais Samia kuwa wataendelea
kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati vijijini pamoja na kuwasimamia kwa
karibu wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi hiyo ili
kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na wa ubora unaotakiwa ili iweze
kuwanufaisha wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment