Sehemu ya viongozi na wajumbe Shirika la TTCL wakiwa katika hafkla hiyo. |
Wageni mbalimbali walioshiriki katika hafla hiyo. |
TANZANIA itaendelea kushiriki katika kuimarisha mawasiliano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa kuunganisha nchi zote kwenye ukanda huu kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Hadi sasa tayari imeunganisha nchi ya Kenya, Burundi na Rwanda.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Mamlaka ya Teknolojia ya Habari ya Kitaifa ya Uganda (National Information Technology Authority of Uganda (NITA-U)) kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano- NICTBB na Mkongo wa Mawasiliano wa Uganda (National Backbone Infrastructures- NBI).
"Malengo yetu ni kuhakikisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za SADC zinaunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano-NICTBB ili kuharakisha shughuli za maendeleo na kufungua fursa za kibiashara ndani ya Jumuiya zetu na kutafuta fursa nyingine katika masoko ya kimataifa," alisema Waziri Nnauye.
Alisema ni matumani ya Tanzania kuiona Afrika yenye mifumo imara ya Serikali Mtandao, Elimu Mtandao, Afya Mtandao, Biashara Mtandao, Kilimo Mtandao pamoja na mambo mengine yanayorahisisha katika utoaji huduma kwa wananchi kwenye mataifa yao.
"Miundombinu hii ya Mkongo wa Mawasiliano na Vituo vya Kuhifadhia Data kimtandao ndiyo ya msingi kuwezesha matumizi ya TEHAMA kuunganisha nchi za Afrika zetu. Ni matumaini ya Tanzania kuona Afrika ya Kidigital (Africa Digital) inafikiwa na matokeo yake chanya yanasaidia katika kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi na shughuli za kijamii barani Afrika kwa kutumia teknolojia," alisisitiza Mhe. Waziri Nnauye.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga akitoa ufafanuzi juu ya makubaliano hayo kibiashara kati ya Uganda na Tanzania alisema, Hati ya Makubalinao ya kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano –NICTBB na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wa Uganda- NBI unathamani ya kiasi cha Dola za Kimarekani shilingi 28,800,000.00 sawa na fedha za Kitanzania Shilingi Bilioni 71.7 kwa kipindi cha miaka 15, ambapo Mikongo hii itaunganishwa kupitia eneo la Mutukula mpaka wa Tanzania na Uganda, katika Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera.
"Ndugu zetu NITA-U napenda kuwahakikishia kuwa TTCL kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano – NICTBB tuko tayari katika kuhakikisha tunatoa huduma inayostahili kwa Uganda kwa kuzingatia masharti yaliyopo katika Hati hii ya Makubaliano ya kibiashara," alisisitiza Mkurugenzi huyo Mkuu wa TTCL.
Aidha aliongeza kuwa hadi sasa Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL limefanikisha kuunganisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano- NICTBB, ambazo ni Kenya, Burundi, Rwanda na sasa hivi nchi ya Uganda.
Pamoja na hayo, pia katika Jumuiya ya Kusini mwa Afrika tumefanikiwa kuunganisha nchi ya Malawi na Zambia, kwa upande wa Msumbiji tayari tumeishafikisha huduma kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbuji eneo la Mtambaswala tunasubiria wenzetu wa Msumbuji kujiunga.
No comments:
Post a Comment