Waziri Mkuu Kassim Majaliwa |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia wakazi wa Handeni na Watanzania kwamba Rais Samia Suluhu Hassan yuko imara na amewahimiza watendaji wa Serikali wajipange kumsaidia ili atimize maono yake.
“Nataka niwahakikishie
kwamba Rais wetu yuko imara sana, yuko imara sana, anafanya kazi yake vizuri
ila ni sisi watendaji ndiyo tunamuangusha. Kuanzia sasa hiyo kitu hamna;
tutabanana na Halmashauri mjipange,” alisema.
Waziri Mkuu aliyasema
hayo Septemba 29, 2023 wakati akizungumza na wananchi na viongozi waliohudhuria
uwekaji wa jiwe la msingi kwenye hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni,
iliyojengwa eneo la Mkata-Mbweni, mkoani Tanga.
Akisisitiza juu ya
usimamizi wa miradi ya Serikali, Waziri Mkuu alisema: “Mkurugenzi wewe siyo desk
officer, wewe ni field officer; simamieni watu wenu. Kama
umekuja juzi au mwaka jana au ulikuwepo, nendeni site mkeshe
huko na kuhakikisha kazi zinafanyika. Zamani tuliwasema Wakuu wa Idara lakini
sasa tunataka Wakurugenzi muwajibike.”
Waziri Mkuu alisema
Rais Samia aliingia madarakani mwaka 2021 na kutoa fedha nyingi za miradi
mbalimbali lakini cha kushangaza kuna watu hadi leo hawajamalizia ujenzi wa
hiyo miradi. “Kuna kasoro kubwa imejitokeza ni watu walipata fedha yote lakini
majengo hayajaisha. Yeyote aliyepokea fedha za mwaka 2021 au 2022 na kazi bado
haijaisha, ajue kuwa hayuko salama. Si Handeni wala kwingineko, yeyote ambaye
hajamaliza ujenzi hatutamvumilia,” alisisitiza.
“Natoa agizo kwa Wakuu
wa Wilaya, pitieni kwenye miradi yenu na muangalie ni miradi ipi ilipokea fedha
mwaka 2021 na je leo inatumika? Hivi inakuwaje zahanati ya tangu mwaka 2022
hadi leo haijamalizika? Kwani kujenga zahanati inahitaji matofali mangapi,
mabati mangapi, na inahitaji kuwa na vyumba vingapi?,” alihoji Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi na
watendaji wanaosimamia mradi huo na kuwataka waendelee kuongeza kasi ya ujenzi
ili mradi ukamilike kwa wakati uliopangwa na wananchi waweze kunufaika na
huduma zote muhimu.
“Mkurugenzi wa
Halmashauri hakikisha vifaa vilivyonunuliwa na vitakavyonunuliwa, vinatunzwa
vema pamoja na majengo yote yaliyopo. Tunzeni pia miundombinu mingine yote
iliyopo, kumbukeni mradi huu umegharimu fedha nyingi za kodi za Watanzania
pamoja na fedha za wafadhili,” alisema wakati akimwagiza Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Bw. Saitoti Stephen.
Aliitaka Halmashauri
iweke mkakati wa ukarabati wa miundombinu iliyopo ili kuepusha gharama za
matengenezo makubwa. Pia akawataka waweke mpango mahsusi wa kutunza mazingira
kwa kupanda miti inayokubaliana na hali ya hewa ya mahali hapo.”
Alisisitiza kuwa fedha
inayopelekwa kwa ajili ya kutelekeza miradi iwe ya Serikali au ya wafadhili
itumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa. “Halmashauri mjipange, kazi iendelee, na
iendelee kwa ubora,” alisema.
No comments:
Post a Comment