TAFITI VETA KANDA YA KATI ZALETA TIJA KWA WAJASIRIAMALI NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 24 September 2023

TAFITI VETA KANDA YA KATI ZALETA TIJA KWA WAJASIRIAMALI NCHINI

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, John Mwanja akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa mafunzo kwa wajasiriamali wanaojishughulisha na utoaji wa huduma ya chakula na vinywaji Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma yaliyoandaliwa na VETA.

 Na Dotto Mwaibale,  Bahi

TAFITI zinazofanywa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati zimeanza kuonesha tija kwa wajasiriamali hapa nchini kwa kuboresha huduma zao na kujikwamua kiuchumi.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa mafunzo kwa wajasiriamali wanaojishughulisha na upikaji wa vyakula Mama na Baba Lishe wa Bahi mkoani Dodoma alisema mafunzo wanayoyatoa yameanza kuonesha tija kwa walengwa hasa baada ya kupata mwanga.

"Sisi VETA Kanda ya Kati tumekuwa tukifanya utafiti katika maeneo mbalimbali zinapofanyika shughuli za kijasiriamali ili kuona kama zinatija ambapo tunaona sinasifa za kuweza kuwaongezea kipato kikubwa lakini inashindika kutokana na wahusika kushindwa kujipambanua na kuendelea kufanya ujasiriamali usiowaingizia kipato kinono licha ya maeneo yao ya kazi kuwa na wateja lukuki," alisema Mwanja.

Alisema mpaka hivi sasa wamekwishafanya tafiti tatu ambapo kwa awamu ya kwanza walianza mwaka jana wilayani Ikungi mkoani Singida na baada ya utafiti wao walibaini kumekuwa na kuku wengi wa asili ambao wanahitajika kwa kiwango kikubwa katika mikoa mbalimbali ukiwemo wa Dodoma ambao ni makao makuu ya nchi lakini wananchi wanashindwa kufuga kwa wingi nakuendelea na ufugaji ule wa kizamani usiokwenda na soko kubwa la uhakika.

Mwanja alisema utafiti wa awamu ya pili waliufanya tena katika wilaya hiyo hiyo baada ya kuzindua Chuo cha VETA na kubaini kuwa kumekuwa na soko kubwa la mbuzi na kondoo wakati wa Sikukuu ya Eid Al Adha ya kuchinja ambao wanyama hao wamekuwa wakinunuliwa kutoka mikoa mingine kutokana na Singida kutokuwanao wa kutosha.

Kwa awamu ya tatu Mwanja alisema walifanya utafiti Wilaya ya Bahi na kugundua ni wilaya ambayo inamwingiliano mkubwa wa watu, wageni na wasafiri wanaotumia barabara kutoka nchi za jirani kupitia mikoa ya kanda ya ziwa kwenda Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam ambao wamekuwa wakipata chakula katika wilaya hiyo.

“Hapa Bahi sio kwamba hakuna wajasiriamali wanao uza vyakula na vinywaji wapo lakini bado hawafanyi vizuri katika soko licha ya kuwa katika eneo lenye wateja wengi,madereva wa malori wanaegesha magari yao hapa kwa ajili ya kupumzika na kupata mahitaji ya chakula na vinywaji achilia mbali mabasi, magari madogo na watu wengine lakini wanafanya chini ya kiwango na kupata kipato kidogo ndio maana kufuatia utafiti wetu tukaona tuwaite na kuwapa mafunzo hayo yatakayowasaidia kubadilika na kukiingia katika ujasiriamali wa viwango na wenye tija.

Alisema mafunzo hayo yanagharamiwa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na VETA kazi yao ni kufanya utafiti na kuwatoa wataalamu ambao uwafundisha wajasiriamali hao kulingana na mahitaji ya eneo husika.

“Kipee nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa kuliona jambo ili jema analolifanya kwa wananchi wake kwa kutoa fedha nyingi ambazo zinakwenda kubadilisha maisha yao kwani wengi wao wanauwezo mkubwa wa kujitafutia riziki lakini hawana uelewa mpana wa kufanya shughuli zao ili wasonge mbele kimaisha na ndio maana tunakutana nao na kuwapata mafunzo haya bure,” alisema Mwanja.

Alisema VETA Kanda ya Kati ambao wanahudumia mikoa ya Singida, Manyara na Dodoma wamejipanga kuendelea kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia za kuhakikisha wananchi wanabadilika kiuchumi kwa kujitegemea kutokana na fedha anazozitoa kwa ajili yao.

Mwanja alitumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa wananchi wa wilaya ya Bahi kuwahimiza watoto wao ambao wamemaliza masomo yao ya shule ya msingi, sekondari na vyuo vikuu lakini wapo nyumbani kwa sababu moja au nyingine kwenda kujiunga na Chuo cha VETA kilichojengwa wilayani humo kupata stadi za ufundi ambao unaweza kuwasaidia kujiajiri badala ya kuajiriwa na kuondokana na changamoto ya soko la ajira ambao baadhi yao wakekuwa wakipata msongo wa mawazo na kufikia hatua ya kujiua kwa kukosa kazi.

Alisema chuo hicho ujenzi wake umekwisha kamilika kwa asilimia 100 na kuwa kitaanza kuendesha mafunzo ya kozi ndefu na fupi na kuwa ya muda mrefu yatachukua muda wa miaka miwili hadi mitatu ambayo yatatolewa katika fani zipatazo sita katika awamu ya kwanza ambazo ni Uhazili na Kompyuta (Secretarial and Computer Application),Ushonaji (Design Sewing and Cloth Technology), Uashi (Masonry and Bricklaying),Umeme wa Majumbani (Electrical Installation),Ufundi Magari (Motor Vehicle Mechanics) na Uchomeleaji Vyuma (Welding and Metal Fabrication).

Alisema chuo kitaanza kudahili wanafunzi januari mwakani na kuwa nafasi zipo za kutosha.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Zaina Mlawa akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo aliwataka washiriki kuzingatia yale ambayo watafundishwa kwani ni mafunzo yenye tija na yana kwenda kuinua maisha ya familia za wana Bahi na taifa kwa ujumla.

"Mahitaji ya chakula katika hili eneo letu la Bahi ni makubwa mno kutokana na kuwa na wageni wengi na muingiliano wa watu mbalimbali zingatieni mafunzo haya yatawaongezea kipato na kuweza kujikimu kimaisha na familia zenu kutokana na huduma nzuri mtakazo zipata na halmashauri yetu itapata mapato kutokana na kodi mtakayokuwa mkilipa,” alisema Mlawa.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo Mwalimu wa Fani ya Upishi VETA Kanda ya Kati Dodoma, Adelina Edward, alisema mafunzo hayo kwa wapishi na watoa huduma ya chakula ni ya muhimu sana na kuwa wameyafanya kufuatia utafiti walioufanya katika wilaya hiyo.

Alisema katika utafiti huo waligundua kuwa watoa huduma wa chakula wa wilaya hiyo katika maeneo kadhaa ya ufanyaji kazi zao wamekuwa na changamoto za hapa na pale zikiwemo za namna ya kutunza kumbukumbu, usafi wa chakula,lugha nzuri kwa wateja, uvaaji wenye staha na mambo mengine mengi ambayo yanafanana na hayo ambayo wanapaswa kuyafanya.

Alitaja baadhi ya maeneo waliyoyafundisha kwenye mafunzo waliyotoa kuwa ni huduma bora kwa wateja na mbinu zitakazotumika ili mteja aridhike na huduma zao, kumjua mteja anayemuhudumia na eneo ambalo huduma zao zilipo.

Edward alisema eneo lingine walilowafundisha ni namna ya kumjua mteja kama atakuwa ameridhika baada ya kuhudumiwa chakula na aina ya mteja anayehudumiwa.

“Ni muhimu kwa mtoa huduma wa chakula na vinywaji akaifahamu vizuri bidhaa au huduma anayoitoa kwa mteja wake kwani wapo baadhi ya wateja wanahitaji maelezo ya kina ili aweze kushawishika na huduma yako,” alisema Edward. 

 Washiriki  wamafunzo hayo Semeni Athumani, Nicholaus Machimo, Charles Aman na Christina Wilson waliishukuru sana VETA kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yamewaongezea uelewa mkubwa wa utunzaji wa kumbukumbu za mauzo yao jambo ambalo walikuwa hawalifanyi.

“Tulikuwa tunafanya ujasiriamali wetu bila ya kutunza kumbukumbu lakini sasa tunakwenda kununua madaftari matatu kama tulivyoelekezwa kwa ajili ya ya utunzaji wa kumbukumbu zetu ambayo ni la mauzo, manunuzi na gharama nyinezo kama matumizi ya umeme, kodi, usafiri na mengineyo na kuwa biashara bila ya daftari hupotea bila ya habari,” alisema Wilson.

Semeni Athumani alisema anaishukuru VETA kwa kuwapelekea mafunzo hayo kwani sasa wamejua namna ya kuwahumia wateja wa muda mfupi kama wanaofanya kazi za ukandarasi ambao wanatakiwa kulipa papo kwa papo baada ya kuhudumiwa kwani walikuwa wakiwakopesha na mradi ukiisha wanaondoka bila ya kuwalipa jambo ambalo lilikuwa likiwapa changamono ya kuwatafuta viongozi ambao mradi husika upo ili wawasaidie kupata fedha zao bila ya mafanikio.

Washiriki hao kwa pamoja walitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka watu wenye vipato vya chini kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya mafunzo hayo walipewa kupitia wataalam kutoka VETA.

Aidha walimshuru Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja na watumishi wenzake tendaji wake kwa jinsi walivyojitoa kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yanakwenda kubadilisha maisha yao kupitia fursa za utoaji wa huduma kwa wateja wao na wakaomba mafunzo hayo yawe endelevu kwani kuna wenzao wengi ambao hawajabahatika kuyapata. 

Mwezeshaji wa mafunzo hayo Mwalimu wa Fani ya Upishi VETA Kanda ya Kati Dodoma, Adelina Edward, akitoa mafunzo hayo.

Afisa Masoko na Utafiti VETA Kanda ya Kati, Sadan Komungoma, akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Bahi, Dani Zakayo akizungumza wakati wa mafunzo hayo.

Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Bahi wakiwa kwenye mafunzo hayo.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Semini Athumani akichangia jambo.

Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.

Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea. Kulia ni kiongozi wa washiriki wa mafunzo hayo, Nicholaus Machimo.
Mafunzo yakiendelea.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Christina Wilson akichangia jambo.
Mshiriki wa mafunzo hayo Charles Amani akichangia jambo.
Taswira ya mafunzo hayo.
Mshiriki wa mafunzo hayo akichangia jambo ambapo alisema changamoto kubwa walionayo ni mitaji na elimu ya biashara zao.
Michango mbalimbali ikitolewa.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.

Taswira ya mafunzo hayo.
Muonekano wa Jengo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
 

No comments:

Post a Comment